Tafuta

Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wote wa Lebanon kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wote wa Lebanon kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Mlipuko wa Beirut, Lebanon: Umoja na Mshikamano wa Upendo

Papa analiomba Kanisa nchini Lebanon kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu katika mahangaiko yao. Kanisa liwe ni alama na kielelezo cha: umoja, mshikamano, huruma na upendo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtindo wa maisha wa viongozi wa Kanisa uwe ni ushuhuda wa ufukara wa Kiinjili kwa kutambua na kuguswa namahangaiko makubwa ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 9 Agosti 2020, amesema, mawazo yake yana rejea mara kwa mara mjini Beirut nchini Lebanon ambako mlipuko uliotokea kwenye eneo la bandari ya Beirut, Jumanne, tarehe 4 Agosti 2020 umekwisha kusababisha watu zaidi ya 150 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 hawana makazi maalum baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo. Janga hili kwa namna ya pekee kabisa lina wahusu watu wa Mungu nchini Lebanon wanaopaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lebanon, anasema Baba Mtakatifu, kwa miaka mingi imeendelea kujipambanua kuwa ni mahali pa tamaduni mbali mbali kukutana na kielelezo cha watu kuishi kwa amani na utulivu. Hata kama mafungamano haya kijamii yalikuwa dhaifu sana, lakini, kwa msaada na neema ya Mwenyezi Mungu sanjari na ushirikiano wa wote mafungamano haya yanaweza kupyaishwa tena upya na kuibuka yakiwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali. Baba Mtakatifu aliomba Kanisa nchini Lebanon kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu katika mahangaiko yao ya kiroho na kimwili. Kanisa liwe ni alama na kielelezo cha: umoja, mshikamano, huruma na upendo, huku likiwa na mikono na nyoyo wazi, tayari kushirikishana hata kile kidogo kinachopatikana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mtindo wa maisha wa viongozi wa Kanisa, Mapadre na Watawa uwe ni ushuhuda wa ufukara wa Kiinjili kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Kamwe wasiwe ni watu wa kupenda tafrija na anasa! Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha upendo na huruma kwa kuwasaidia wananchi wa Lebanon ambao kwa sasa wanapambana na hali ngumu ya maisha. Wakati huo huo habari kutoka Beirut, zinasema kwamba, kumekuwepo na machafuko ya hali ya kisiasa na kijamii nchini Lebanon kufuatia mlipuko uliojitokeza nchini humo hivi karibuni na hivyo kuvilazimisha vyombo vya ulinzi na usalama kutumia mabomu ya kutupwa na mkono ili kuwasambaratisha waandamanaji. Wananchi wamekuwa wakilalamikia kuhusu vitendo vya kigaidi, uongozi dhaifu; rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Kutikisika kwa uchumi na hivyo kuongezeka kwa watu wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na umaskini; janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na urasimu wa kutisha ni kati ya mambo ambayo yamewachefua sana wananchi wa Lebanon kiasi cha kutokuwa na imani tena na viongozi wa Serikali na wanasiasa waliko madarakani kwa wakati huu.

Lebanon kwa miaka ya hivi karibuni, imekuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu waliokuwa wanatafuta hifadhi ya kisiasa milioni moja. Hatima ya watu hawa wote kwa sasa iko mashakani. Itakumbukwa kwamba, Serikali ya Lebanon, imetangaza hali ya hatari kwa muda wa majuma mawili, huku maofisa 16 wa mji wa Beirut, wakiwa wamezuiliwa kwa kifungo cha ndani, ili kusubiri uchunguzi wa tuhuma zinazowahusu kufuatia mlipuko huo ambao umesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Rais Michel Aoun alisema kwamba mlipuko huo ulisababishwa na tani 2,750 za madini ya “Amonium Nitrate” yaliyokuwa yamehifadhiwa katika ghala moja huko Beirut. Hasara iliyojitokeza hadi wakati huu inakadiriwa kufikia bilioni 5 za dola za Kimarekani. Rais Michel Aoun wa Lebanon ametupilia mbali uchunguzi wowote wa kimataifa kuhusu mlipuko mbaya uliyotokea katika bandari ya Beirut, ambao umepelekea watu zaidi ya 150, kupoteza maisha na kubaini kwamba uchunguzi huo unaweza kupotosha ukweli.

Papa Lebanon 2020
09 August 2020, 14:24