Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amechangia kiasi cha Euro 250, 000 kwa Kanisa nchini Lebanon ili kusaidia juhudi za kutoa huduma ya afya, chakula na malazi kwa wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu Francisko amechangia kiasi cha Euro 250, 000 kwa Kanisa nchini Lebanon ili kusaidia juhudi za kutoa huduma ya afya, chakula na malazi kwa wahitaji zaidi. 

Mlipuko wa Beirut, Lebanon: Msaada Kutoka Kanisa Katoliki

Papa Francisko amechangia kiasi cha Euro 250, 000, ili kulisaidia Kanisa kuweza kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kutokana na mlipuko uliotokea huko mjini Beirut, Jumanne, tarehe 4 Agosti 2020 na kusababisha watu zaidi ya 150 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 hawana makazi maalum baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kupitia Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu ametoa kiasi cha Euro 250, 000, ili kulisaidia Kanisa kuweza kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kutokana na mlipuko uliotokea kwenye eneo la bandari ya Beirut, Jumanne, tarehe 4 Agosti 2020 na kusababisha watu zaidi ya 150 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 hawana makazi maalum baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo. Hadi kufikia Jumamosi asubuhi, tarehe 8 Agosti 2020, watu 60 walikuwa hawajulikani mahali walipo. Msaada kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni ushuhuda wa uwepo wake wa karibu kwa watu walioguswa na kutikiswa na mlipuko huo ambao umeacha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Msaada huu umewakilishwa kwa viongozi wa Kanisa nchini Lebanon kupitia kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Lebanon. Lengo ni kusaidia juhudi za Kanisa katika huduma ya afya, makazi ya muda pamoja na kuendelea kuwapatia watu mahitaji msingi. Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Lebanon, Caritas Lebanon, yameanza kampeni ya kuratibu misaada kutoka kwa Wasamaria wema sehemu mbali mbali za dunia, ili iweze kuwafikia walengwa kwa wakati. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa kiserikali, kisiasa, kijamii na kidini wataweza kushirikiana na kushikamana, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mlipuko huu, kwa msaada pia kutoka Jumuiya ya Kimataifa.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limechangia kiasi cha Euro milioni moja kwa ajili ya kusaidia watu kupata huduma na mahitaji msingi kama vile: dawa na vifaa tiba, chakula, maji na malazi kwa wahitaji zaidi. Katika kipindi cha mwaka mzima, Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Italia, “Caritas Italiana” itashirikiana na Caritas Internationalis pamoja na Caritas Lebanon ili kusaidia ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya huduma msingi kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasikitika kusema kwamba, janga hili limekuja wakati ambapo, Lebanon inaendelea “kuchechemea” kutokana na ukata mkubwa wa rasilimali fedha, kuyumba kwa uchumi pamoja na kinzani za kisiasa na kijamii ambazo zimepelekea ongezeko la watu maskini nchini Lebanon.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa waliotikiswa na kuguswa na janga hili pamoja na kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Nalo Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Kaskazini mwa Italia, Caritas Ambrosiana limechangia kiasi cha Euro 20, 000, ili kuwasaidia watu walioathirika huko nchini Lebanon. Kutokana na kuharibiwa kwa maghala ya nafaka huko Beirut, bei ya mazao ya chakula imepanda maradufu na baa la njaa linawanyemelea watu wengi kwa sasa nchini humo! Nalo Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hungaria, Caritas Hungary limechangia kiasi cha Euro 28, 000 ili kusaidia jitihada za kuokoa maisha ya watu walioathirika na mlipuko huo. Kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni; dawa na vifaa tiba, maji, chakula na makazi ya muda.

Na Habari zaidi zinasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limeitikia mwito kutoka kwa Kardinali Bechara Boutros Rai, ili kuisaidia Lebanon kwa hali na mali kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu na wananchi wa Lebanon. Kanisa linajipanga ili kuweza kupeleka msaada wake haraka iwezekanavyo, lakini pia Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, limeiomba Serikali ya Marekani kupeleka msaada wa dharura nchini Lebanon ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kwa magonjwa na njaa huko Beirut. Serikali ya Marekani imesema, itachangia dola za kimarekani milioni 15, ili kusaidia watu kwa chakula na dawa.

Naye Kardinali Jean Claude Hollerich, Rais wa Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, COMECE anasema, angependa kutoa wito kwa familia ya Mungu nchini Lebanon, kudumisha amani, utulivu na uvumilivu wakati huu ambapo wanakabiliwa na changamoto kubwa zilizosababishwa na mlipuko huko Beirut. Kwa miaka mingi, Lebanon imeonesha ukarimu kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu waliokuwa wanatafuta hifadhi ya kisiasa. Kwa muda wa miaka thelathini Lebanon imekuwa ni kimbilio la watu wengi kutoka Mashariki ya Kati. Huu ni wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano upendo na udugu wa kibinadamu. Kuna changamoto kubwa mintarafu maisha ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kwa upande wake, Rais Michel Aoun amesikika akisema kwamba, mlipuko huo ulisababishwa na tani 2,750 za madini ya “Amonium Nitrate” yaliyokuwa yamehifadhiwa katika ghala moja huko Beirut. Wachunguzi wa mambo wanasema, gharama ya madini yote haya inakadiriwa kuwa ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 15. Hasara iliyojitokeza hadi wakati huu inakadiriwa kufikia bilioni 5 za dola za Kimarekani. Wananchi wengi wa Lebanon wanaishutumu serikali yao kwa: kwa uzembe, kutowajibika pamoja na kuendelea kupekenywa na rushwa na ufisadi hali ambayo imepelekea mji wa Beirut kukumbwa na maafa haya makubwa.

Papa: Msaada Lebanon

 

 

08 August 2020, 14:17