Tafuta

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Agosti, anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Agosti, anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu. 

Kumbukumbu Ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu! Tumaini la Waamini

Kumbukumbu ya B.Maria Malkia wa Mbingu inachota utajiri wake katika Biblia, Liturujia, Sanaa ya mambo matakatifu pamoja na Ibada ya watu wa Mungu kwa Bikira Maria. Kwa mara ya kwanza sikukuu hii iliadhimishwa tarehe 31 Mei, lakini baada ya mageuzi ya Liturujia yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, siku kuu hii ikapangwa iadhimishwe tarehe 22 Agosti ya kila mwaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 22 Agosti, kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, Sikukuu iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1954. Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Ad Caeli Reginam” anabainisha kwamba, ingawa Sikukuu inaonekana kana kwamba, ni mpya, lakini inachota utajiri wake katika Maandiko Matakatifu, Liturujia ya Kanisa, Sanaa ya mambo matakatifu pamoja na Ibada ya watu wa Mungu kwa Bikira Maria. Kwa mara ya kwanza siku kuu hii iliadhimishwa tarehe 31 Mei, lakini baada ya mageuzi ya Liturujia yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, siku kuu hii ikapangwa iadhimishwe tarehe 22 Agosti ya kila mwaka. Hii ni kumbukumbu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, siku chache tu baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti.

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho  kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”.

Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 alitangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Bikira Maria Malkia wa Mbingu anashiriki utukufu wa ufalme wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, alama na mfano wazi kabisa ya matumaini ya Wakristo ambao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo nao pia wanashiriki: ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo. Papa Pio XII, tarehe 1 Novemba 1954 aliwaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika shida na mahangaiko yao. Bikira Maria ni kikao cha hekima na faraja kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo.

Hii ni faraja inayobubujika kutoka katika msingi wa imani, matumaini na mapendo, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Bikira Maria alishiriki hatua kwa hatua mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani na hatimaye, kushirikishwa utukufu wa Mwanaye mpendwa kwa kupalizwa mbinguni mwili na roho. Kwa waamini walioko huku bondeni kwenye machozi, wasisite kukimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Bikira Maria anashiriki kwa namna ya pekee upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya walimwengu. Ni kielelezo cha unyenyekevu na huduma ya upendo, inayofumbatwa katika kuhudumia, kusaidia na kupenda kwa dhati. Kristo Yesu aliposulubiwa pale mlimani Golgota, palikuwa na anuani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, “Mfalme wa Wayahudi”. Huu ni ufalme unaokita mizizi yake katika unyenyekevu, mateso na upendo wa dhati. Ni kwa njia hii, Ufalme wa Kristo Yesu unakuwa ni chemchemi ya ukweli, upendo, haki na amani. Ni ufalme unaofumbatwa katika huduma, kama ambavyo Bikira Maria alivyomjibu Malaika Gabrieli kwamba, yeye ni mjakazi wa Bwana na katika mwanga huu, Kanisa linamwona Malkia aliyezama katika huduma, sala na upendo.

Katika Litania ya Bikira Maria, waamini wanamsifu Bikira Maria kuwa ni Malkia wa Malaika, Malkia wa Mababu, Malkia wa Manabii, Malkia wa Mitume, Malkia wa Mashahidi na Waungama dini; Malkia wa Watakatifu wote na mwishoni anatajwa kuwa ni Malkia wa familia. Waamini wanamkimbilia Maria kwa sala na salam, wakisema, Salam Malkia wa mbingu! Heshima ya Bikira Maria kuitwa Malkia ni kielelezo cha imani, furaha, mapendo na msaada wa daima. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Ibada kwa Bikira Maria ni sehemu muhimu sana katika maisha ya kiroho. Hata katika shida na mahangaiko yao ya kiroho na kimwili, wawe na ujasiri wa kumkimbilia Bikira Maria Malkia wa mbingu, anayewapenda, kuwasikiliza na kuwaombea kwa Mwanae mpendwa Kristo Yesu! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Bikira Maria asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni pamoja na mwili na roho yake, akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, ili afananishwe kikamilifu zaidi na Mwanawe, aliye Bwana wa mabwana. Rej. LG. 59.

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu nchini Poland, ulikuwa ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, kwa wema na ukarimu wake na kwamba, matunda ya miaka 1050 ya Ukristo nchini humo yanaonekana! Miaka hii yote imekuwa ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Poland kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kuambata Mafundisho tanzu ya Kanisa na Neno la Mungu, mambo ambayo yamesaidia kujenga utamaduni wa Familia ya Mungu nchini Poland, ushuhuda unaojionesha katika medani mbali mbali za maisha ya watu.

Kanisa nchini Poland anasema Baba Mtakatifu Francisko limeonesha mshikamano wa upendo na wananchi wa Poland katika hija ya maisha yao kwa kufurahi pamoja nao wakati wa furaha; kwa kulia nao wakati wa shida na majonzi, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake! Katika kipindi chote hiki, waamini wamejenga na kukuza matumaini kwa Mwenyezi Mungu, wamekuza Ibada kwa Bikira Maria wa Czestochowa, Mama na Malkia. Wameimarisha imani na sasa wako tayari kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa zaidi, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji. Waamini wanaalikwa kujenga na kuimarisha mahusiano yao na Kristo Yesu, tayari kuwashirikisha jirani zao ile furaha ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Malkia wa Mbingu

 

21 August 2020, 14:05