Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, Jubilei ya Miaka 100 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Maria Margherita Caiani: 2020-2021 Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, Jubilei ya Miaka 100 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Maria Margherita Caiani: 2020-2021 

Miaka 100 Tangu Alipofariki Mwenyeheri M. Caiani: 2020-2021

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anawataka kuzingatia mambo yafuatayo: Kumbukumbu endelevu ya maisha na mafundisho ya Mwanzilishi wa Shirika lao, Unyenyekevu katika maisha na utume wao; Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na maisha ya sala kwa ajili ya malipizi ya dhambi za walimwengu. Kusoma alama za nyakati

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyeheri Maria Margherita Caiani (1863-1921), kunako mwaka 1896 akisaidiana na watawa wenzake wawili kutoka katika Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, walianzisha Shirika na Masista Wadogo Wafranciskani wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, M.S.C.; “Suore Francescane Minime del Sacro Cuore” mjini Poggio huko Caiano. Watawa hawa wakajikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, kwa kufundisha na kutembelea wagonjwa pamoja na kusaidia huduma mbali mbali za kichungaji Parokiani. Tarehe 15 Desemba 1902, Shirika likatambuliwa rasmi na Mama Kanisa. Na tarehe 3 Februari 1926, Vatican ikalitambua Shirika hili na kulipatia hadhi ya Mashirika ya Kipapa na baada ya kipindi cha majaribio, tarehe 21 Novemba 1933 likatambuliwa moja kwa moja na Kanisa. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Shirika na Masista Wadogo Wafranciskani wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, M.S.C. likajipambanua kwa kutoa huduma kwa waathirika wa vita. Hadi Mwenyeheri Maria Margherita Caiani alipokuwa anafariki dunia, tarehe 8 Agosti 1921, aliacha akiwa ameanzisha Jumuiya kumi na tatu zilizokuwa na watawa 124, waliokuwa wanajisadaka kila kukicha katika huduma ya kufundisha watoto wadogo kwenye shule za awali, kutunza watoto yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na huduma kwa wagonjwa hospitalini.

Kunako mwaka 1989, Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Maria Margherita Caiani kuwa ni Mwenyeheri. Watawa wa Shirika hili wameendelea kumwilisha na kutamadunisha karama yao sehemu mbali mbali za dunia, hadi wakafika mjini Bethlehemu, Misri, Brazil na Sri Lanka na huko wakafungua Jumuiya zao. Ni katika muktadha huu, hapo tarehe 8 Agosti 2021 Shirika la Masista Wadogo Wafranciskani wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, M.S.C., litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Maria Margherita Caiani. Jubilei hii imezinduliwa rasmi Jumamosi tarehe 8 Agosti 2020 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Fausto Tardelli wa Jimbo Katoliki la Pistoia, Kaskazini mwa Italia. Ni mwaka ambao, watawa hawa wanapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani pamoja na kuhakikisha kwamba, wanaendelea kupyaisha na kumwilisha karama ya Shirika, kwa watu wanaowahudumia, huku wakiendelea kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anawataka kuzingatia mambo yafuatayo: Kumbukumbu endelevu ya maisha na mafundisho ya Mwanzilishi wa Shirika lao, Unyenyekevu katika maisha na utume wao; Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na maisha ya sala, kwa ajili ya malipizi ya dhambi za walimwengu. Baba Mtakatifu analitaka Shirika la Masista Wadogo Wafranciskani wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, M.S.C. kufanya kumbukumbu endelevu ya maisha, utume na mafundisho ya mwanzilishi wa Shirika lao, huku wakiiangalia historia ya Shirika lao, kipindi cha miaka 120 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao. Wawe na ujasiri na moyo wa shukrani kwa kujipatanisha na historia yao iliyopita, huku wakiyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini, bila kutaka kukimbilia na kujificha katika historia ya yale yaliyopita kwani si ndwele, wanapaswa kuganga yaliyopo na yale yajayo, kwa kuishi na kutenda, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni muda wa kumwilisha karama ya Shirika, zawadi ya Roho Mtakatifu. Ni muda wa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia nguvu mpya na uwezo wa kuendelea kutoa harufu nzuri duniani kwa njia ya zawadi ya maisha yao. Mwenyeheri Maria Margherita Caiani alipenda kuwaita Masita wadogo “Minime” kama kielelezo cha maisha yao katika hali ya udogo ambao ni kielelezo cha unyenyekevu, daima kwa kuendelea kujifunza kutoka katika Shule ya Familia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, ili kuweza kumfuata kwa ukamilifu zaidi, Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, aliyeamua kufuata njia hii, kiasi hata cha kujinyenyekesha hata kifo Msalabani. Unyenyekevu ni njia ambayo watawa wa Shirika hili wanapaswa kuifuata kila kukicha, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ambaye Mwenyezi Mungu katika udogo wake, akamwangalia na hatimaye akamteuwa kuwa ni Mama wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uwe ni chemchemi ya upendo, kielelezo cha upendo na uaminifu wa hali ya juu kabisa uliooneshwa na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Alionesha upendo kwa wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; akawanyanyua wale ambao utu, heshima na haki zao msingi zilikuwa zinasiginwa, na hivyo kuwarejeshea tena imani. Kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wawili wa Emau, walioandamana na Kristo Yesu, akabahatika kuwafafanulia Maandiko Matakatifu. Alivyotwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbiliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Baba Mtakatifu anawaalika watawa hawa kumpenda Kristo Yesu kwa moyo wao wote na kwa matendo yanayofumbata utajiri wa huruma na mapendo. Moyoni mwao ni mahali pa kwanza kabisa pa kuweza kuuishi upendo huu kwa dhati kabisa na kama Jumuiya ya kitawa!

Moyo Mtakatifu wa Yesu, uwe ni utambulisho wa maisha na utume wao, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu amejisadaka, akawazaa katika imani na kuwaita kwa ajili yake na kuwaweka wakfu katika Moyo wake Mtakatifu. Utambulisho huu unajidhihirisha kwa namna ya pekee kabisa anasema Baba Mtakatifu Francisko katika sala. Maisha yao yote kwa njia ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu yanapaswa kuwa ni sala, ili kuweza kuungana daima na Kristo Yesu. Ni kwa njia ya mshikamano na mafungamano haya, Kristo Yesu ataweza kuwapyaisha kila siku ya maisha yao, na hivyo kuzifanya nyoyo zao zifanane na Moyo wake Mtakatifu. Nyakati za Sala zinazoweza kujenga mafungamano haya ni katika: Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sala za Kanisa, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Masomo ya Maisha ya Kiroho. Ni kwa njia hii, kama watawa wataweza kumwendea Kristo Yesu kwa furaha na shangwe kubwa kama afanyavyo mtoto mdogo anapowakimbilia wazazi wake, ili wamkumbatie na kumpatia busu! Kukaa na kumtafakari Kristo Yesu ni jambo la msingi zaidi katika maisha ya kitawa. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu pale Bustanini Gethsemane, Kristo Yesu, anawaalika watawa kuwa karibu pamoja na kukesha naye, ili aweze kuungana pia pamoja nao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, karama ya Shirika inakita mizizi yake pia kwa ajili ya toba na maondoleo ya dhambi za walimwengu, huduma kubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, dhambi inaharibu kazi nzuri ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu. Watawa kwa njia ya sala, matendo ya huruma na malipizi, wanasaidia kupandikiza mbegu ya upendo wa Mungu inayopyaisha yote na kuwa na mapya. Huu ndiyo ushuhuda unaojionesha katika shughuli mbali mbali za kitume wanazotekeleza nchini Italia, Brazil, Misri, Sri Lanka na Bethlehemu, hasa zaidi kwa ajili ya huduma kwa watoto na vijana. Haya ni matendo ambayo yanausaidia ulimwengu kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa njia ya mng’ao wa upendo wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia maadhimisho mema ya Jubilei ya Miaka 100 tangu alipofariki muasisi wa Shirika lao Mwenyeheri Maria Margherita Caiani. Amewahakikishia sala na sadaka yake kwa ajili ya maisha na utume wao sanjari na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Anawaomba hata wao kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Wafranciskani

 

 

08 August 2020, 14:38