Tarehe 2 Agosti 2020 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Msamaha wa Assisi. Waamini wanaweza kujipatia rehema kamili kwa kutekeleza masharti yaliyotolewa na Mama Kanisa. Tarehe 2 Agosti 2020 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Msamaha wa Assisi. Waamini wanaweza kujipatia rehema kamili kwa kutekeleza masharti yaliyotolewa na Mama Kanisa. 

Papa Francisko: Msamaha wa Assisi: Rehema Kamili na Huruma

Msamaha wa Assisi ni zawadi ya maisha ya kiroho ambayo Mt. Francisko wa Assisi alipewa na Mwenyezi Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria. Kwa njia ya Msamaha wa Assisi, waamini waliojiandaa vyema, wanaweza kujipatia Rehema kamili. Kipaumbele ni huruma ya Mungu inayowakirimia maisha na uzima wa milele, kwa ajili yao binafsi na hata kwa wale wanaowazunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho ya imani na ibada ya Rehema katika Kanisa Katoliki yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake, hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata Rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza masharti yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa Rehema kamili. Nne; asali Kanuni ya Imani na Sala ya Baba Yetu, kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu.

Mwishoni, atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa Rehema Kamili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 amezungumzia kuhusu “Msamaha wa Assisi” ni zawadi ya maisha ya kiroho ambayo Mtakatifu Francisko wa Assisi alipewa na Mwenyezi Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria. Kwa njia ya Msamaha wa Assisi, waamini waliojiandaa vyema, wanaweza kujipatia Rehema kamili. Baba Mtakatifu anasema, kipaumbele cha kwanza ni huruma ya Mungu kwa waja wake, inayoweza kuwakirimia maisha na uzima wa milele, kwa ajili yao binafsi na hata kwa wale wanaowazunguka. Msamaha wa Assisi ni tukio linaloadhimishwa na Kanisa kuanzia Usiku wa kuamkia tarehe 1 Agosti hadi Usiku wa tarehe 2 Agosti. Katika kipindi, waamini waliojiandaa kikamilifu wanaweza kupokea Rehema kamili.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Agosti 2016 alifanya hija binafsi mjini Assisi ili kusali kwenye Kikanisa cha “Porziuncola” ambacho kwa mapenzi ya Mungu na ugunduzi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, katika kipindi cha miaka 800 kimekuwa ni chemchemi ya neema na baraka kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hija hii binafsi ya Baba Mtakatifu, ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi. Wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani katika maadhimisho hayo waliwaomba wanashirika wote pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuwa na aibu takatifu kutokana na ukweli kwamba, jitihada za kutaka kukuza na kudumisha amani, usalama, ustawi na maendeleo kati ya watu zinaendelea kugonga mwamba.

Katika hali na mazingira kama haya, Wafranciskani waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuwa na kipaji cha ugunduzi, ili kuweza kuimba utenzi utakaoeleweka na watu wa kizazi hiki, katika jitihada za kutaka kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani katika ujumbe wao kwa ajili ya maadhimisho haya walisema tarehe 2 Agosti 2016 ilikuwa ni siku maalum ya kujipatia Rehema kamili kwa wale wote waliokuwa wametimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa mintarafu rehema kamili. Pili, Jubilei hiyo ilikwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu iliyotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, aliyemchagua Mtakatifu Francisko wa Assisi kuwa ni msimamizi wake katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Jubilei hiyo ikawa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana dhana ya huruma ya Mungu na msamaha mintarafu tasaufi ya maisha ya Wafranciskani. Huruma ni neno muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, changamoto kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, lakini pia kuwa na huruma kwa jirani zao kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Huruma na msamaha ni chanda na pete kwani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha ya kiroho. Kimsingi, huu ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu yanayojikita katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Hata katika nyakati hizi za matatizo na changamoto zilizoibuliwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bado kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika fadhila ya huruma, upendo, mshikamano na ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu!

Ni kutokana na muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", kwa maelezo ya Baba Mtakatifu Francisko imeagizwa kutoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Idara ya Toba ya Kitume, “Penitenzieria Apostolica” inatoa Rehema Kamili kwa watu walioshambuliwa na Virusi vya Corona, COVID-19; kwa waamini ambao wamewekwa chini ya kalantini wakiwa wamelazwa hospitalini au majumbani mwao. Ikiwa kama kutoka katika undani wa mioyo yao wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana.

Rehema hii inatolewa pia kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na wanafamilia wote wanaowahudumia wagonjwa kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema. Rehema hii inatolewa kwa waamini watakaoweza pia kuabudu Ekaristi Takatifu, watakaoweza kusoma walau Neno la Mungu kwa muda wa nusu saa, au kusali Rozari, kufanya Njia ya Msalaba au kusali Rozari ya Huruma ya Mungu, ili kuomba huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, ili kuwaondolea watoto wake balaa la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anaendelea kusali kwa ajili ya waamini ambao hawataweza kupata fursa ya kupokea Mpako wa Wagonjwa, kwa kuwaweka chini ya huruma ya Mungu, nguvu na umoja wa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupokea fumbo la kifo kwa amani na utulivu wa ndani. Tamko hili linawahusu wagonjwa wote kwa sababu kunahitaji zito ambalo limeletwa na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Msamaha wa Assisi
02 August 2020, 14:01