Tafuta

Msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko vimewasili nchini Brazil. Msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko vimewasili nchini Brazil. 

Msaada wa Papa Kwa Wagonjwa Wa COVID-19 Nchini Brazil

Kati ya mashine 18 za kupumlia zilizopelekwa nchini Brazil, mashine 8 zimetolewa kwa ajili ya hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na watawa nchini Brazil, kati yake ni Hospitali ya Don Orione iliyoko huko Araguaìana, Kaskazini mwa Brazil. Zote hizi ni juhudi za Askofu mkuu Giovanni D’Aniello, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Brazil. Watawa wa Don Orione, wanamshukuru sana Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 19 Agosti 2020 amekita tafakari yake hasa kuhusu: Upendeleo kwa maskini na fadhila ya upendo. Katika roho ya Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, upendeleo wa pekee ni lazima utolewe kwa maskini, wenye njaa, wagonjwa, kwa wageni, kwa wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa, kwa wafungwa, kwa wahamiaji ambao wanadharauliwa, kwa wakimbizi au waliofukuzwa makwao (Rej. Mt .25:31-46). Kujibu katika haki na upendo mbele ya mahitaji ya watu hawa ni jukumu la kila mtu. Upendeleo kwa ajili ya maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake kwenye Heri za Mlimani, Ufukara wa Kristo Yesu pamoja na huduma yake kwa maskini wanaojionesha katika sura zake mbali mbali. Kristo Yesu mwenyewe alijilinganisha na maskini!

Kumbe, Kanisa ni chombo cha faraja, utetezi na ukombozi kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa amesema, wasamaria na watu wenye mapenzi mema, wanaendelea kuitikia wito wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 hasa kwa kusaidia nchi maskini zaidi duniani. Ni katika muktadha huu anasema Kardinali Konrad Krajewski, Baba Mtakatifu Francisko ameguswa sana na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Brazil na kuamua kuwapatia zawadi ya mashime 18 za kupumlia, kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa waliowekwa kwenye uangalizi maalum.

Huu ni msaada uliotolewa na Asasi ya kujitegemea ya “Hope Onlus” inayotekeleza dhamana na wajibu wake hasa katika sekta ya elimu na afya, kwa kutoa vifaa tiba ili kuokoa maisha. Kati ya mashine 18 za kupumlia zilizopelekwa nchini Brazil, mashine 8 zimetolewa kwa ajili ya hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na watawa nchini Brazil, kati yake ni Hospitali ya Don Orione iliyoko huko Araguaìana, Kaskazini mwa Brazil. Zote hizi ni juhudi za Askofu mkuu Giovanni D’Aniello, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Brazil. Watawa wa Don Orione, wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaangalia kwa jicho la huruma na upendo hasa wakati huu, Brazil inapoendelea kupambana na kipeo cha maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tocantins ni kituo maalum kilichotengwa Kaskazini mwa Brazil kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Vifaa tiba hivi, msaada kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko vitasaidia sana katika huduma kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum!

Vifaa Tiba Brazil
31 August 2020, 13:46