Vatican News
Kumbukumbu ya Miaka 75 ya Shambulizi la Hiroshima nchini Japan: Papa asema, ni wakati muafaka wa kusikiliza kilio cha "Hibakusha" ili kujizatiti katika mchakato wa haki, amani na utulivu Kumbukumbu ya Miaka 75 ya Shambulizi la Hiroshima nchini Japan: Papa asema, ni wakati muafaka wa kusikiliza kilio cha "Hibakusha" ili kujizatiti katika mchakato wa haki, amani na utulivu  (AFP or licensors)

Papa: Miaka 75 ya Mashambulizi ya Hiroshima: Amani Duniani

Baba Mtakatifu anasema, ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi yaani: silaha za nyuklia zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbali mbali duniani. Baba Mtakatifu anasema ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema! AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 ilipambwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za atomiki; maafa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ukapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Haya ni mambo ambayo bado yameacha kumbu kumbu hai katika maisha ya wananchi wa Japan.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2020 linasema: Linda maisha yote, Amani ni safari ya Matumaini. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 6 Agosti 2020 imeadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu mji wa Hiroshima uliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, hadi wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Gavana wa Hiroshima, nchini Japan katika maadhimisho haya anasema,  wakati wa hija yake ya Kitume nchini Japan Mwezi Novemba 2019, alipata bahati ya kutembelea Uwanja wa Kumbu kumbu ya Amani mjini Hiroshima na huko akasikiliza shuhuda za “Hibakusha” yaani wahanga wa shambulizi la nyuklia,  huko Hiroshima kunako mwaka 1945.

Baba Mtakatifu anasema, alibahatika kuweza kutembelea miji ya Hiroshima na Nagasaki wakati wa hija yake ya kitume nchini Japan, Novemba, 2019. Alipata pia nafasi ya kutafakari maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao wakati wa mashambulizi ya  miji hii miwili, miaka 75 iliyopita. Baba Mtakatifu anasema kwamba, alikwenda Japan kama hujaji wa amani, hija ambayo ameihifadhi katika sakafu ya moyo wake, kiu ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Watu na hasa vijana wana kiu ya amani na wanataka kuendelea kujisadaka kwa ajili kulinda na kudumisha amani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anabeba kilio cha maskini ambao daima wamekuwa ni waathirika wakuu wa kinzani, mipasuko mbali mbali pamoja na vita.

Baba Mtakatifu anasema, ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi yaani: silaha za nyuklia zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbali mbali duniani. Kwa mara nyingine Baba Mtakatifu anasema bila kupepesapepesa macho kwamba: ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ushuhuda wa “hibakusha” yaani wahanga wa mashambulizi ya mabomu ya nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki utaendelea kuwa ni sauti inayotoa onyo kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa kizazi kijacho. Hapa kuna haja ya kujikita katika mchakato wa upatanaisho ya kitaifa, ili, hatimaye, kuweza kubinafsisha maneno ya Mzaburi  yasemayo: “Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu niseme sasa, “Amani ikae nawe”. Zab. 122: 8. Na kwa ujumbe huu wa amani, Baba Mtakatifu Francisko, amewapatia washiriki wote wa maadhimisho ya Miaka 75 tangu mji wa Hiroshima uliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia baraka zake za kitume.

Papa: Hiroshima

 

07 August 2020, 13:43