Papa Francisko asema likizo ni muhimu sana kwa wanafamilia ili kujipatia nafasi ya mapumziko- Lakini wanasiasa, wachumi na watunga sera watoe kipaumbele cha kwanza kwa kazi kama utimilifu wa binadamu. Papa Francisko asema likizo ni muhimu sana kwa wanafamilia ili kujipatia nafasi ya mapumziko- Lakini wanasiasa, wachumi na watunga sera watoe kipaumbele cha kwanza kwa kazi kama utimilifu wa binadamu. 

Papa Francisko: Likizo: Changamoto ya Umaskini na Fursa za Ajira

Hata baada ya kumalizika kwa janga la COVID-19: umaskini na ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya matatizo na changamoto zitakazoendelea kuitesa Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika kipaji cha ugunduzi, ili kupata suluhu ya matatizo na changamoto zote hizi. Mshikamano ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Likizo ya Kipindi cha Kiangazi kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kujipatia tena nguvu za kuweza kusonga mbele katika mapambano ya maisha ya kila siku. Ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na kazi kubwa ya uumbaji. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani mazingira bora ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu. Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu kwa sababu mazingira bora ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu.

Likizo ni wakati muafaka wa kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia.

Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu! Hatari kubwa sana! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020, amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, pamoja na wale wote waliokuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, likizo njema ya kipindi cha kiangazi kwa mwaka 2020. Ni matumaini yake kwamba, watu wa Mungu wataweza kupata nafasi ya kujipumzisha walau kidogo; kwa kutembelea na kutafakari kazi ya uumbaji, daima wakiwa na mwelekeo wa maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwamba, wanasiasa, wachumi na watunga sera, wataweza kujizatiti vyema zaidi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiekolojia. Katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia rafiki. Baba Mtakatifu anakaza kusema, bila fursa za ajira, familia na jamii katika ujumla wake, haitaweza kusonga mbele hata kidogo. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na wale wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea nafasi za ajira kwa watu wengi zaidi. Hata baada ya kumalizika kwa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19: umaskini na ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya matatizo na changamoto zitakazoendelea kuitesa Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika kipaji cha ugunduzi, ili kupata suluhu ya matatizo na changamoto zote hizi.

Papa: Likizo 2020
02 August 2020, 14:26