Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema Uponyaji wa Ulimwengu unapaswa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Baba Mtakatifu Francisko anasema Uponyaji wa Ulimwengu unapaswa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii  (Vatican Media)

Papa Francisko: Uponyaji wa Ulimwengu: Kipaumbele Maskini!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendeleo kwa ajili ya maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake kwenye Heri za Mlimani, Ufukara wa Kristo Yesu pamoja na huduma yake kwa maskini katika sura zake mbali mbali. Kristo Yesu mwenyewe alijilinganisha na maskini! Kumbe, Kanisa ni chombo cha faraja, utetezi na ukombozi kwa ajili ya maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye, ili kutafakari kuhusu janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Tafakari hii makini, inaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja, wataweza kushiriki tafakari hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Baba Mtakatifu katika mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 19 Agosti 2020 amekita tafakari yake hasa kuhusu: Upendeleo kwa maskini na fadhila ya upendo. Katika roho ya Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, upendeleo wa pekee ni lazima utolewe kwa maskini, wenye njaa, wagonjwa, kwa wageni, kwa wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa, kwa wafungwa, kwa wahamiaji ambao wanadharauliwa, kwa wakimbizi au waliofukuzwa makwao (Rej. Mt .25:31-46). Kujibu katika haki na upendo mbele ya mahitaji ya watu hawa ni juu ya kila mtu. Upendeleo kwa ajili ya maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake kwenye Heri za Mlimani, Ufukara wa Kristo Yesu pamoja na huduma yake kwa maskini katika sura zake mbali mbali. Kristo Yesu mwenyewe alijilinganisha na maskini! Kumbe, Kanisa ni chombo cha faraja, utetezi na ukombozi kwa ajili ya maskini.

Katekesi hii imeongozwa na tafakari ya Neno la Mungu kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho 8: 1-2.9 mwaliko wa kulitimiza changizo kwa wanajumuiya wa Yerusalemu, kwa neema ya Mungu waliyopewa Makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao... Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake amesema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limepelekea umaskini mkubwa kuanikwa bayana na ukosefu wa usawa sehemu mbali mbali za dunia kudhihirika hadharani. Gonjwa hili halibagui wala kuchagua kati ya maskini na tajiri, wale wote wanaokumbana nalo “uso kwa uso wanakiona cha mtema kuni.”

Jambo la kuhuzunisha ni kuona kwamba, kumekuwepo na pengo kubwa kati ya maskini na matajiri na ubaguzi umeongezeka maradufu. Changamoto ya Virusi vya Corona, COVID-19 inahitaji kwanza kabisa kupatiwa tiba muafaka, kwani Virusi vya Corona, COVID-19 hata kama ni vidogo kiasi gani vimeipigisha dunia magoti! Lakini, kirusi kikubwa zaidi kinachopaswa kuvaliwa njuga, ili hatimaye, kupatiwa tiba muafaka ni ukosefu wa haki jamii na fursa sawa; ubaguzi pamoja na ukosefu wa ulinzi kwa maskini na wanyonge katika jamii. Jibu makini linalotolewa mintarafu mwanga wa Injili ni kukataa uchoyo na ubinafsi; kwa kuonesha uzuri wa Injili unaotoa upendeleo na kipaumbele cha pekee kwa maskini, walio wadogo kabisa, wale ambao jamii inawatupilia mbali na kuwageuzia kisogo. Rej. EG. Namba 195.  Upendeleo kwa maskini si suala la kisiasa bali ni kiini cha Injili ambacho kinachota utajiri wake kutoka katika Fumbo la Umwilisho na kama kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ambaye hapo mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu. Akazaliwa katika familia ya watu wanyenyekevu na kufanya kazi ya mikono. Mwanzo mwa maisha na utume wake wa hadhara, akatangaza na kusema kwamba, kwenye Ufalme wa Mungu, maskini wana heri. Akaendelea kuwaganga na kuwaponya wagonjwa; maskini akawarejeshea utu na heshima yao; waliosukumizwa pembezoni mwa jamii, akawakumbatia na kuwaonesha upendo wa huruma ya Mungu, kiasi hata cha kubezwa na watu kwa sababu ya mshikamano wake na maskini. Kwa njia hii, Kristo Yesu, amehatarisha hata maisha na utume wake kwa kuwa karibu zaidi na maskini.

Ni katika muktadha huu, Wakristo wanapaswa kujiainisha na kuwa karibu zaidi na: maskini, wanyonge, wagonjwa, wafungwa na wale wote wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; watu walio uchi na wale wote wanaoteseka kwa baa la njaa. Huu ndio ufunguo maalum wa Ukristo wa kweli, utume wa Kanisa zima na wala si kwa ajili ya wateule wachache tu! Wakristo wakiwa wameungama pamoja na Mwenyezi Mungu wanaweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kila Mkristo mmoja na kila jumuiya inaitwa kuwa chombo cha Mungu kwa ajili ya ukombozi, ustawi wa maskini sanjari na kuwawezesha kuwa kikamilifu sehemu ya jamii. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kipimo cha hukumu ya Siku ya Mwisho. Rej. EG. Namba 187. Fadhila za Kimungu ambazo ni imani, matumani na mapendo zinawasukuma na kuwahamasisha waamini kujikita katika kanuni ya upendeleo kwa maskini na wanyonge zaidi, hali inayovuka mipaka ya mahitaji msingi ya binadamu. Waamini wanaitwa kutembea kati pamoja na maskini, kwani katika magumu na changamoto za maisha yao waamini wanamtambua Kristo mteseka.

Waamini wajiruhusu wainjilishwe na maskini, kwani uinjilishaji mpya ni mwaliko wa kutambua nguvu mpya ya kuokoa inayotenda kazi katika maisha ya maskini kwa kuwapatia kipaumbele cha kwanza. Waamini wanahamasishwa kumkuta Kristo Yesu ndani ya maskini na kuyapatia masuala yao sauti ya Kanisa; kwa kuonesha urafiki, kwa kuwasikiliza na kuwatetea sanjari na kukumbatia hekima ya ajabu ambayo Mwenyezi Mungu anataka kuwashirikisha Wakristo kupitia kwa maskini. Kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini ni mwaliko wa kusimama kidete kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuponya na kubadili miundo mbinu ya kijamii ambayo inaelemewa na magonjwa jamii. Hii ndiyo hija inayowapeleka katika upendo wa Kristo Yesu aliyewapenda upeo, kiasi cha kugota mwishoni mwa mipaka ya mambo msingi ya kibinadamu. Kristo Yesu pamoja na maskini, wapewe umuhimu wa pekee, kwa maana neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Jumuiya ya Kimataifa imeingiwa na wasi wasi mkubwa kutokana na madhara makubwa ya kijamii ambayo yamesababishwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Watu wengi wanaonesha ari na mwamko wa kutaka kurejea tena katika shughuli zao za kila siku pamoja na kuendeleza shughuli za uchumi na uzalishaji. Lakini, haki jamii na utunzaji bora wa mazingira ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa, ili kujenga na kudumisha uchumi fungamani na shirikishi hata na maskini. Lengo ni kuondokana na “falsafa ya misaada isiyokuwa na tija wala mashiko”. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji uchumi bora utakaosaidia mchakato wa kuzalisha nafasi za ajira na wala si uchumi ambao unageuka kuwa ni sumu na hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Uchumi usaidie maboresho katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, upendeleo kwa maskini ni hitaji la maadili kijamii linalopata chimbuko lake kutoka kwenye upendo wa Mungu unaopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa sera na mikakati ya kiuchumi, ambapo binadamu na mahitaji yao msingi wakipewa kipaumbele cha pekee na maskini wakiwa ni kiini cha sera hizi.

Kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wahitaji zaidi katika sera na mikakati ya kinga na tiba dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Mambo makuu ya kuzingatiwa na viwanda vitakavyozalisha kinga na tiba dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Ushirikishwaji, Kipaumbele kwa maskini, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, itasikitisha sana, ikiwa kama chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 matajiri watapewa kipaumbele cha pekee. Hii ni kashfa ya mwaka, kuona rasilimali fedha ya umma inaelekezwa zaidi katika kufufua uchumi na hivyo kuendelea kuchangia ukosefu mkubwa wa fursa za ajira badala ya kujenga uchumi fungamani, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Ikiwa kama janga la homa kali ya mapafu litaendelea kuongezeka maradufu na waathirika wakuu wakawa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kuna haja ya kusimama kidete, ili kufanya mageuzi makubwa kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, daktari na mganga wa upendo wa Mungu ambao ni fungamani, yaani huu ni upendo unaotibu na kumganga mwanadamu: kimwili, kiroho na kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha katekesi yake kwa kusema, huu ni wakati muafaka wa kujifunga kibwebwe ili kuganga na kuponya magonjwa makubwa ya kijamii yanayoonekana na ambayo yamesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kumwilisha sehemu Injili ya Mathayo, Sura ya 25 kama sehemu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Mchakato wa kuganga na kuponya magonjwa haya, upate chimbuko lake katika upendo wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini kama kielelezo cha matumaini yanayokita mizizi yake katika imani na kwa njia hii, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na ulimwengu bora zaidi. Mwenyezi Mungu awajalie watu wake neema, nguvu na baraka ya kuweza kutoka katika janga hili wakiwa wameboreka zaidi, kwa kusoma alama za nyakati na kujibu mahitaji msingi ya watu katika ulimwengu mamboleo.

Papa: Upendeleo kwa Maskini

 

19 August 2020, 14:21