Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo bado ni donda ndugu katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo bado ni donda ndugu katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. 

Biashara ya Binadamu Ni Donda Ndugu kwa Utu Wa Binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni donda ndugu linaloendelea kuathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anasema, watu wanapaswa kuwaangalia jirani zao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kila mtu akiwa ni kiumbe cha pekee sana machoni pa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sababu nzito zinazopelekea watu kujikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato, unaowawadanganya watu hawa kwamba, watapata fursa za ajira na hivyo kuondokana na hali yao duni. Lakini ukweli wa mambo, wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao. Ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya: kiuchumi, kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili na kiutu, kutokana na kuelemewa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na madaraka! Mapambano haya yamepewa kipaumbele cha pekee katika utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Biashara ya binadamu si wazo la kufikirika bali ni hali halisi inayogusa mamilioni ya watu duniani.

Hawa ni wale watu wanaotumbukizwa kwenye biashara na utalii wa ngono; biashara ya viungo vya binadamu; ndoa shuruti na kazi za suluba kwa watoto wadogo ambao wakati mwingine wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita. Watoto hawa wakati mwingine wamekuwa ni kafara wa imani za kishirikina sehemu mbali mbali za dunia. Wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa mara nyingi wamejikuta hata wao pia wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe alioandika kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Wajunbe wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina waliokuwa wanashiriki katika Semina maalum kuhusu Mapambano Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu na Mifumo ya Utumwa mamboleo, tarehe 30 Julai 2020 amesema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni donda ndugu linaloendelea kuathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, watu wanaojishughulisha na utumwa mamboleo wanapaswa kuwaangalia jirani zao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kila mtu akiwa ni kiumbe cha pekee sana machoni pa Mwenyezi Mungu. Ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, iwe ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, biashara hii inatoweka katika uso wa dunia. Wahanga wasaidiwe kwa hali na mali, ili hatimaye, waanze kuandika historia mpya katika maisha yao hapa duniani. Kipaumbele cha pekee ni kuhakikisha kwamba,  waathirika hawa wanajengewa uwezo wa kiuchumi, kijamii na maisha ya kiroho, ili waweze kujielekeza zaidi katika mchakato utakaowawezesha kusimama kidete kulinda, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi, ili hatimaye, kupata utimilifu wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria Lujàn anayeheshimiwa sana nchini Argentina, aweze kuwaombea baraka na neema ya kuweza kupambana kikamilifu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Semina hii imewashirikisha wajumbe zaidi ya 600 walioshiriki kwa njia ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii. Wajumbe walioshiriki ni pamoja na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama; mahakama na wanasiasa pamoja na Asasi Zisiko za Kiserikali pamoja na viongozi wa Kanisa kutoka nchini Argentina. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, halikuwa kikwazo katika mahudhurio ya semina hii, kwa sababu, watu wengi zaidi wameshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Imekuwa ni fursa pia kwa Kanisa kuendelea kuragibisha madhara ya biashara ya binadamu pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2020, imeadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya Utumwa mamboleo. Hii siku iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ili kusaidia juhudi za Jumuiya ya kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha ya binadamu, haki msingi, utu na heshima yake. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaoendelea kusimama kidete ili kuwasaidia na kuwahudumia wahanga wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Kuna hatua kubwa ambazo zimekwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, lakini, bado kuna haja ya kuendelea kupambana ili hatimaye, kashfa hii dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu iweze kufutika machoni pa uso wa dunia! Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipokuwa anahutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mapambano haya lazima kwanza kabisa yalinde na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu.

Papa: Utumwa Mamboleo Argentina
06 August 2020, 07:18