Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kumwomba Kristo Yesu awakirimie neena na baraka za kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kumwomba Kristo Yesu awakirimie neena na baraka za kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka! 

Mapadre Ombeni Neema ya Ushuhuda wa Huruma na Upendo!

Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, mwaka 2019, Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya mshikamano na upendo wa kibaba, akiguswa na huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya!

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2019 aliadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney. Papa Pio XI kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani. Ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 40 akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa sala, toba na wongofu wa ndani, uliofumbatwa katika maisha ya unyenyekevu. Akajitahidi kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Katika maadhimisho ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani. Huu ukawa ni muda wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Ukuu, Utakatifu, Wito na Maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa. Mapadre walikumbushwa kwamba, utambulisho na uhuru wa wafuasi wa Kristo Yesu ni mambo makuu mawili yanayowawezesha hata Mapadre katika maisha na utume wao, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani.

Mapadre kama binadamu wanatambua udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, changamoto ya kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu. Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbali mbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini. Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya kisakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu.

Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao.

KUHUSU MATESO: Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni mapadre wamekuwa wasikivu kwa kilio na mateso ya ndugu zao na wakati mwingine katika hali ya ukimya. Hawa ni watu waliokumbwa na nyanyaso za kijinsia zilizosababishwa na matumizi mabaya ya madaraka. Wahanga, familia pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao, wameteseka sana. Kanisa limedhamiria kujikita katika utamaduni wa shughuli za kichungaji kwa kukazia mfumo wa kukinga ili kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa watu wote wa Mungu kuwajibika barabara. Baba Mtakatifu anakazia wongofu wa ndani, ukweli na uwazi sanjari na mshikamano kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kujenga utamaduni wa kuwa sikivu kwa shida na mahangaiko ya walimwengu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mateso haya yamewagusa hata Mapadre wenyewe, kiasi cha kuona kwamba, si mali kitu mbele ya watu wanaowahudumia kwa sadaka na majitoleo makubwa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa imegusa na kutikisa maisha na utume wa Mapadre. Kwa hakika, mapadre wengi, wamesikitishwa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa na wanaendelea kupandikiza mbegu ya matumaini mapya. Kuna madhara makubwa ambayo yametendwa na Mapadre katika nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Lakini, bado kuna maelfu ya mapadre wanaoendelea kutekeleza dhamana na wito wao kwa ukarimu na uaminifu mkubwa. Ni watu ambao wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baadhi yao wanafanya utume katika mazingira magumu na hatarishi sana. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kwa ushuhuda wao katika nyakazi hizi za mateso na magumu yanayoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Mapadre. Mapadre waendelee kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kipindi hiki cha utakaso katika maisha na utume wa Kanisa, kitawawezesha Mapadre kuwa wanyenyekevu na watu wenye furaha, kwa kutarajia kuyakumbatia ya mbeleni kwa matumaini makubwa. Kipindi hiki cha mateso, kisiwakatishe tamaa, bali iwe ni fursa ya kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu, kwani bila yeye ni Mapadre si mali kitu. Kristo anapenda kuwaokoa kutoka katika unafiki na tabia ya kutaka kujikweza, ili kuonekana mbele ya watu, lakini Yesu anataka kuwarudishia ule uzuri na utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre. Toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika unyenyekevu na machozi ya uchungu, yapate kibali cha ukuu wa Mungu unaofumbatwa katika msamaha, mwanzo wa hija ya utakatifu wa maisha.

SHUKRANI KWA MAPADRE: Baba Mtakatifu anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana! Huu ni wakati wa kusimama tena na kusema, Mimi hapa Bwana, nipe nguvu ya kusimama tena ili nitoe huduma kwa watakatifu majirani; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre wazee wagundue tena ndani mwao, ile furaha waliyokuwa wanapata walipozitembelea familia za Kikristo; walipokuwa wanakwenda kutoa Sakramenti za Kanisa kwa wazee na wagonjwa.

Mapadre watambue kwamba, wamepakwa mafuta ya wokovu, ili kuwahudumia jirani zao na kamwe wasikate tamaa, ndiyo maana anasema, kamwe haachi kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa ajili yao. Mapadre watambue udhaifu wao wa kibinadamu, karama na neema walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuamua na kutenda kwa ukarimu. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa sababu huruma ya Mungu yadumu milele. Moyo wa shukrani ni silaha madhubuti inayowawezesha kutafakari ukarimu wa Mungu katika maisha yao, mshikamano, msamaha, subira, uvumilivu na upendo, kiasi hata cha kuthubutu kusema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”, lakini Kristo Yesu akamwambia “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” kwa sababu huruma yake yadumu milele!

Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre kwa uaminifu na sadaka wanayotoa kila kukicha, kielelezo cha utekelezaji wa Agano la Mungu lisilokuwa na kikomo. Ni wakati wa kusherehekea uaminifu wa Mungu usiokuwa na kikomo, kwani bado anaendelea kuwaamini licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, kwa kutambua kwamba wanabeba wito huu mtakatifu katika vyombo vya udongo. Wanatambua kwamba, hata katika udhaifu wao, Mwenyezi Mungu anaweza kuonesha ukuu na ushindi kwa sababu huruma yake yadumu milele! Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika shughuli mbali mbali za kichungaji. Kwa hakika Mapadre wamekuwa ni vyombo vya mshikamano na upendo wakati wa raha na shida; hata pale Mapadre walipokosa na kukosoana kwa upendo, kwani huruma yake yadumu milele.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa udumifu wao katika shughuli mbali mbali za kichungaji, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wao kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu, kwa sababu huruma yake yadumu milele. Mapadre wanashukuriwa kwa kuadhimisha Sakramenti za huruma ya Mungu; kwa kuwaongoza na kuwasindikiza waamini wao katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kiasi cha kuruhusu ile ngazi ya huruma ya Mungu iweze kushuka katika udhaifu na dhambi zao, tayari kuonja utakaso, daima wakitambua kwamba, wanapaswa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma, tayari kuwaongoza waamini wao kwenye mwanga angavu kwa sababu huruma yake yadumu milele!

Mapadre wanashukuriwa kwa kuendelea kuwa ni Wasamaria wema ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake wanaoteseka na kuogelea katika dimbwi la dhambi. Hali hii iwakumbushe Mapadre kwamba, wametwaliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kuambata unyenyekvu pasi na makuu, kwa ajili ya Injili, kwani huruma yake yadumu milele! Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kumtolea Mungu sifa na shukrani kwa ajili ya utakatifu wa watu wa Mungu; awakirimie zawadi ya kutafakari dhamana na utume unaotekelezwa na watu wa Mungu katika hija ya maisha yao, katika hali ya mateso, mahangaiko na hata wakati mwingine wa kutoelewana. Baba Mtakatifu anasema, katika maisha ya waamini, anaona utakatifu wa Kanisa, katika ushuhuda wa maisha na utakatifu wao, watiwe shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

NENO LA FARAJA KWA MAPADRE: Baba Mtakatifu anataka kuwafariji Mapadre wote ili kupyaisha tena ari na moyo wa kipadre, ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani mwao. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, kuna haja ya watu kufarijiana na kutiana shime, ili kuweza kuzipokea changamoto hizi kwa unyenyekevu na kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuzigeuza na kuzitumia kadiri anavyotaka, mambo yanayosimikwa katika sala pamoja na kutambua udhaifu wa kibinadamu. Mapadre kama wachungaji wachunguze ndani mwao, jinsi ambavyo wanakabiliana na mateso yanayowasonga katika maisha na utume wao! Je, ni watu wanaothubutu “kufunika kombe, ili mwana haramu apite? Je, ni watu wanaokimbia matatizo na changamoto za maisha?

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwelekeo huu wa maisha unaweza kupachikwa majina mengi kama vile: Ubinafsi, upweke hasi pamoja na hali ya mtu kujifungia katika undani wa ulimwengu wake. Madonda ya maisha na utume wa Mapadre, yawasukume kukimbilia ili kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na faraja ya Mungu kwa watu wake! Kamwe Mapadre wasikubali kukata wala kukatishwa tamaa, bali waonje uwepo mwanana wa jirani zao, ili wasitumbukie katika upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza hata katika kifo! Uchungu wa moyo utawanyima Mapadre kutekeleza utume wao kwa ari na moyo mkuu; watashindwa kuona umuhimu wa sala na hapo kwa hakika maisha yatakuwa ni magumu na machungu sana! Uchungu wa moyo ni adui mkubwa wa maisha ya kiroho! Mapadre kamwe wasitende kwa mazoea, bali waanze hija ya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Mapadre wawe na ujasiri wa kuwa na mwono mpya katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kila siku, daima wakimsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Wakati wa shida na magumu, waamini wanapaswa kufarijiana na kutiana shime anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake kwa Mapadre wote Duniani, Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko duniani!

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote inayobubujika kutoka kwenye ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, vinginevyo, watajikatia tamaa na kuanza kuchanganyikiwa! Mapadre waendelee kupyaisha furaha ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe anajitaabisha kuwaombea. Mapadre wawe na ujasiri wa kuingia na kuzama katika sala kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pale Bustanini Gethsemane: kwa kuona huzuni,  kufadhaika sana pamoja  na kuonja uchungu moyoni. “Kusali si lelemama wala maji kwa glasi”. Sala inawakumbusha Mapadre kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu, daima wanahitaji msaada wake na kamwe hawawezi kujitosheleza kwa nguvu zao wenyewe. Kwa wale wote wanaosumbuka na kuelemewa na mizigo, wanaalikwa kumwendea Kristo Yesu, ili aweze kuwapumzisha. Kwa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu, Mapadre wanaweza kumwita Mungu, “Abba”, yaani “Baba”. Maisha na utume wao kama Mapadre ni majadiliano endelevu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sala ya Makuhani inaboreshwa kwa kumwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu katika furaha, shida na mahangaiko yao ya kila siku. Mapadre wawe daima ni vyombo vya sala kwa ajili yao wenyewe na watu wa Mungu wanaowahudumia! Mapadre wasiwe na majibu ya mkato kwa waamini wao, bali sala iwe ni nguvu inayoongoza maisha yao, kwa kutambua karama na udhaifu wao wa kibinadamu. Mapadre wakuze mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, ili kuungana naye daima, vinginevyo watakuwa kama taa zisizokuwa na mafuta. Mapadre wajichagulie washauri wa maisha ya kiroho; watu ambao wanaweza kuzungumza nao katika misingi ya ukweli na uwazi; wakashirikishana: changamoto, uzoefu na magumu ya maisha. Huyu ni kiongozi atakayewaonesha dira ya maisha, kuwasindikiza pamoja na kuwapatia ushauri, kama njia ya kutekeleza utashi wa Mungu katika utume wao. Kwa njia hii, Mapadre wataweza kusumbukiana na kunyanyuana pale wanapojikuta wakiwa wanaogelea katika mawimbi mazito ya maisha.

Mapadre wajenge mahusiano mema na adili na watu wanaowahudumia, kamwe wasikimbilie kujificha katika makundi ya wasomi. Padre awe kati pamoja na watu wake, awatie shime na kukubali kupokea ushauri kutoka kwao kwani wao pia wana utambuzi wa imani “Sensum fidei”. Kristo Yesu anawahamasisha Mapadre wake kuwa kati kati ya watu wa Mungu, kwa kuhakikisha kwamba, wanawajali watu wao, mtindo wa maisha ambao Yesu aliutumia kama njia ya kuinjilisha! Mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu yawakumbushe Mapadre uzito wa Msalaba wa Kristo uliosababishwa na dhambi za binadamu. Utume wa Mapadre uwawezeshe kuwa karibu zaidi na watu wanaoteseka; watu wanaosumbuliwa na madonda katika maisha, ili kwamba, uzoefu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, usaidie kujenga na kudumisha mahusiano, umoja na mshikamano; kwa kuaminiana sanjari na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa. Kwa njia hii, waamini wa Kanisa la mwanzo walionja msamaha, wakaweza kuwa ni mashuhuda amini kwani huruma yake yadumu milele!

UTUKUFU NA UKUU WA MUNGU: Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Barua kwa Mapadre Duniani kwa kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha ya Mapadre kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa na kwamba, maisha yao yote yawe ni wimbo wa utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre wajifunze kujiaminisha na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Juan Diego, aliyetambua umama wa Bikira Maria na kujiachia ili azamishwe katika tunza na faraja yake ya Kimama. Kumtafakari Bikira Maria kunawawezesha Mapadre kuonja upendo na huruma kutoka kwa Mama Bikira Maria, kielelezo cha unyenyekevu na upendo. Watambue kwamba, wao ni sehemu ya watu wa Mungu. Mateso, magumu na changamoto za maisha ziwafanye Mapadre kuwa vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, tayari kutubu na kumwongokea Mungu.

Bikira Maria, ni msaada na kimbilio la daima hata pale wanapotindikiwa divai, atawaombea; pale wanapochomwa mkuki katika maisha na utume wao, atawafariji; pale wanapokosa imani na matumaini, atawaonjesha matumaini mapya! Baba Mtakatifu anasema,  anaendelea kumshukuru Mungu kwa ajili ya Mapadre wanaojisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ana uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu atawarejeshea tena matumaini pamoja na kuwaondolea kizingiti cha maisha ili kukutana na Kristo Yesu, Jiwe hai, aliyefufuka kwa wafu. Kristo Yesu ni msingi wa Kanisa lake yuko tayari kupyaisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo vya shukrani, kwa kupyaisha ari na mwamko wa shughuli za kichungaji, ili kuwapaka watu wa Mungu mafuta ya matumaini; sanjari na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Papa: Barua Kwa Mapadre

 

 

04 August 2020, 13:27