Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha umoja, upendo na mshikamano wa pekee na watu wa Mungu nchini Mongolia. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha umoja, upendo na mshikamano wa pekee na watu wa Mungu nchini Mongolia.  (Afmc (Archivio fotografico Missioni Consolata))

Papa Francisko: Upendo kwa Familia ya Mungu Nchini Mongolia

Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake na Askofu Marengo, amemhakikishia kwamba, watu wa Mungu kutoka Mongolia wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wake. Wajibu wake wa kwanza ni: Kujitamadunisha katika maisha ya watu wake, ili aweze kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Anatumwa kuwa ni daraja linalounganisha watu wa Mungu na: Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Giorgio Marengo I.M.C. wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, tarehe 2 Aprili 2020 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwakilishi wa Kitume nchini Mongolia na kuwekwa wakfu tarehe 8 Agosti 2020. Ibada hii ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Consolata, Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, iliyoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Huyu ni mmisionari wa kwanza wa Shirika la Waconsolata kutumwa kwenda kuinjilisha nchini Mongolia na huko amekwisha kujisadaka kwa muda wa miaka kumi na saba! Askofu Giorgio Marengo I.M.C, Jumatano, tarehe 12 Agosti 2020 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake na Askofu Marengo, amemhakikishia kwamba, watu wa Mungu kutoka Mongolia wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wake.

Wajibu wake wa kwanza ni kuhakikisha kwamba, anajitamadunisha katika maisha ya watu wake, ili aweze kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Atambue kwamba, anatumwa na Mama Kanisa kuwa ni daraja linalounganisha waamini na Kristo Yesu, Kanisa na viongozi wa Serikali, Kiraia na Kitamaduni. Atambue kwamba, hata kama kuna idadi ndogo sana ya wakleri, watawa na waamini walei, lakini hawa wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Baba Mtakatifu amempatia baraka zake za kitume kwa ajili yake binafsi na watu wa Mungu nchini Mongolia. Amemtia shime, ili aweze kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, matatizo, changamoto na fursa mbali mbali ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Askofu Giorgio Marengo I.M.C, anakaza kusema, kuna tofauti kubwa baada ya kuteuliwa, kuwekwa wakfu na baadaye kukutana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko na kupata nafasi ya kuweza kubadilishana mawazo, mang’amuzi na changamoto za maisha. Kati ya changamoto ambapo Askofu Giorgio Marengo I.M.C, anataka kuzifanyia kazi ni uwepo wake wa karibu kati pamoja na watu wa Mungu nchini Mongolia.

Itakuwa ni nafasi ya kutembelea Jumuiya mbali mbali za Kikristo ili kusali, kutafakari kwa pamoja Neno la Mungu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, anashirikiana kwa karibu zaidi na wamisionari wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa watu wa Mungu nchini Mongolia. Ni vyema kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na viongozi wa Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Mongolia. Hili ni eneo ambalo linahitaji kwa namna ya pekee kabisa, kwa Kanisa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, huku utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Ni nafasi ya kuendeleza mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali kwa kusaidiana na kutegemezana.

Kumbe, mambo makuu kwa wakati huu ni ukaribu kwa watu wa Mungu, majadiliano ya kidini na kitamaduni, ili kweli Injili iweze kukita mizizi yake katika maisha na tamaduni za watu wa Mongolia. Hii ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, ambao watu wa Mataifa mengine wanaweza kujifunza na kuiga. Hawa ni watu wenye moyo wa upendo na mshikamano, wanaoguswa na mahitaji msingi ya jirani zao. Kwa kweli watu wa Mungu nchini Mongolia ni watu wa sala , amani na utulivu wa ndani. Itakumbukwa kwamba, Askofu Giorgio Marengo I.M.C. wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, alizaliwa tarehe 7 Juni 1974 huko Cuneo, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, tarehe 24 Juni 2000 akaweka nadhiri zake za daima na hatimaye, tarehe 26 Mei 2001 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kwa miaka kumi na saba, amekuwa akitekeleza dhamana na utume wake wa kimisionari nchini Mongolia. Tarehe 2 Aprili 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu na mwakilishi wa kitume nchini Mongolia. Tarehe 8Agosti 2020 akawekwa wakfu na kuwa ni Askofu na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Papa: Mongolia

 

 

 

13 August 2020, 13:30