Tafuta

Vatican News
Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria ni shule ya upendo wa dhati, imani na utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa kila siku! Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria ni shule ya upendo wa dhati, imani na utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa kila siku!  (ANSA)

Watakatifu Joakim na Anna: Shule ya Upendo, Imani na Utakatifu!

Vijana watambue na kuthamini nafasi na dhamana ya wazee katika jamii na kamwe wasiwaache kuelemewa na upweke. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kutumia uzoefu na mang’amuzi yao ili kuwaonjesha upendo kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Wawasikilize na kuwatembelea

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai, ametoa mwaliko kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatenda tendo jema la huruma na mapendo kwa wazee wanaowazunguka. Upendeleo wa pekee utolewe kwa wazee wanaoishi peke yao au kwenye nyumba za kutunzia wazee, ambao kwa muda mrefu uliopita hawajapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki zao. Vijana watambue na kuthamini nafasi na dhamana ya wazee katika jamii na kamwe wasiwaache kuelemewa na upweke. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kutumia uzoefu na mang’amuzi yao ili kuwaonjesha upendo kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu ameyasema hayo mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 26 Julai 2020.

Vijana watenge muda wa kuweza kuwasikiliza kwa dhati na pale ambapo inawezekana kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wawatembelee ili kuwajulia hali. Baba Mtakatifu Francisco anasema, Bwana Luis Bernárdez, Mshairi maarufu kutoka Argentina aliwahi kusema, mti ambao mizizi yake imeng’olewa, hautaweza kukua, kuchanua na hata kutoa matunda. Ni katika mantiki hii, Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwapongeza wazee kwa uwepo na ushiriki wao katika maisha na utume wa jamii. Upendo ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu utaweza kukua na kuzaa matunda. Hakuna familia inayoweza kukua na kustawi, ikiwa kama inasahau mizizi yake, yaani asili yake. Watoto na vijana wajifunze kutoka kwa wazee, ili hatimaye, mizizi yao iweze kuzama zaidi katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake Askofu mkuu Walmor Oliveira de Azevedo wa Jimbo kuu la Bel Horizonte, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB., anasema, wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Sherehe hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Brazil. Hawa ni mashuhuda amini wa imani. Matukio kama haya ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wa maisha. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yanachukua nafasi ya pekee sana kwa wazee ambao wamekumbwa, wameguswa na kutikiswa sana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Wengi wao wameitupa mkono dunia, katika hali ya upweke na majonzi makuu. Wazee wanahitaji faraja, upendo na mshikamano wa dhati.

Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani, wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbali mbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” anasifu heshima inayotolewa na familia ya Mungu Barani Afrika kwa wazee wao, kwani wao ni utajiri, hawatengwi wala kudharauliwa bali wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza namna ya kuheshimu na kuwathamini wazee kutoka Afrika. Umaskini na magonjwa visiwe ni sababu ya kuwatenga na kuwakosea heshima wazee katika jamii. Anaichangamotisha jamii kwa ujumla kutambua kuwa wazee ni msingi wa uhai na maendeleo fungamani ya binadamu.

Watakatifu Joakim na Anna
26 July 2020, 13:22