Tafuta

Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa Imani kwa Mwaka 2020 amemtumia ujumbe wa matashi mema Papa Francisko. Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa Imani kwa Mwaka 2020 amemtumia ujumbe wa matashi mema Papa Francisko. 

Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa Kwanza Kwa Papa Francisko!

Patriaki Bartholomeo wa kwanza amemwandikia ujumbe Papa Francisko, akionesha mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kilio cha waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 na ushuhuda wa Kanisa. Matatizo ya maisha ya kijamii na kiuchumi yanayopaswa kushughulikiwa kwa kujikita katika haki jamii na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2020, aliwakumbusha waamini kwamba, hawa ni Mitume walioyamimina maisha yao kama sadaka safi na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika mahubiri yake alikazia: Umoja unaofumbatwa katika upendo na utofauti; katika mateso, sala na ushuhuda wa imani. Alifafanua maana ya Pallio takatifu wanazovishwa Maaskofu wakuu. Pili, aligusia unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu. Upendo unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu amesema, watakatifu Petro na Paulo, walikuwa wamoja, lakini ni watu waliokuwa na taaluma tofauti kabisa. Mtakatifu Petro alikuwa ni mvuvi na muda wake mwingi aliutumia kutengeneza nyavu zake, wakati ambapo Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa, alikuwa anafundisha kwenye Masinagogi. Katika maisha na utume wao, Petro aliwaendea Wayahudi, wakati ambapo Paulo, alijielekeza zaidi kwa wapagani na watu wa Mataifa.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kumekuwepo na utamaduni wa ujenzi wa umoja na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Makanisa haya mawili yanatambua kwamba, Mitume Petro na Andrea walikuwa ni ndugu wamoja. Pale mazingira yanaporuhusu, kumekuwepo na mabadilishano ya wajumbe na wawakilishi wa Makanisa haya mawili katika hali ya udugu wa kibinadamu, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya watakatifu Petro na Andrea. Lengo ni kuwawezesha waamini wa Makanisa haya mawili kutembea kwa pamoja, huku wakiwa wameungana ili hatimaye, siku moja, kadiri ya mapenzi ya Mungu waweze kuwa na umoja kamili. Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amemwandikia ujumbe Baba Mtakatifu Francisko, akionesha mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kilio cha waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 na ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili kutoka kwa Kanisa.

Mwishoni ni matatizo na changamoto za maisha ya kijamii na kiuchumi zinazopaswa kushughulikiwa kwa kujikita katika haki jamii na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Mtakatifu Petro alikuwa ni kiongozi mkuu wa Mitume wakati ambapo Mtume Paulo alikuwa ni Mwalimu wa Mataifa na Mtume wa uhuru kamili, ambao kwa pamoja wametangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, chemchemi ya kazi nzima ya Ukombozi, iliyowapelekea hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Patriaki Bartholomeo wa kwanza anasema, katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume kwa mwaka 2020 imeshindikana kuwateua na kuwatuma wajumbe kutoka katika Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol ili kuhudhuria sherehe hizi kutokana na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Anasema, hata hivyo wameweza kuungana na Kanisa Katoliki kuadhimisha Sherehe ya Watakatifu hawa, pamoja na kushukuru kwamba, kwa sasa wanayo masalia ya Mtakatifu Petro, ambayo kwa sasa ni chemchemi ya nguvu mpya. Wanatambua uzito wa maombezi ya Mtakatifu Andrea, aliyebahatika kuteuliwa na kuitwa kuwa ni Mtume wa kwanza wa Yesu.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene sanjari na matamko ya pamoja yanayogusia matatizo na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Ni matamko ambayo yanakita mizizi yake katika “mwamba wa imani” na fadhila mbali mbali za Kikristo zinazofumbatwa katika upendo na haki. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kutoka katika dhambi na mauti na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Mwanadamu anayo heshima kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha mateso na madhara makubwa kwa maisha ya mwanadamu. Watu wa Mungu wameshuhudia sadaka na majitoleo ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya. Kanisa limesikiliza kilio cha wagonjwa, ndugu na jamaa zao. Linaendelea kushuhudia ukosefu mkubwa wa fursa za ajira na matokeo yake kutokana na kuyumba na hatimaye kuporomoka kwa mfumo wa uchumi na fedha kitaifa na kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, Kanisa linatakiwa kutoa ushuhuda wa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Agano Jipya limesheheni mifano kedekede ya uponywaji uliofanywa na Kristo Yesu, ambaye ni daktari wa roho za watu, aliyekuja kuwakirimia waja wake ukombozi wa kweli. Kristo Yesu alitoa pepo wachafu na kuwaponya wengi, mwenyewe aliutwaa udhaifu wa binadamu, na kuyachukua magonjwa yake. Rej. Mt.8:17. Katika lugha ya kitaalimungu, magonjwa yanahesabika kuwa ni dhambi. Kumbe, Mama Kanisa anawajibu wa kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani kama kielelezo cha upyaisho wa maisha ya kiroho na kimwili. Kanisa ni hospitali ya huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Kumbe, kwa Wakristo tiba na uponyaji wa udhaifu wa mwanadamu ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi, kifo na mauti. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa madaktari, wauguzi na makada wa sekta ya afya, kwamba, huu ni “wito mtakatifu”. Kanisa linakazia umuhimu wa kujenga mahusiano na mafungamano ya uaminifu kati ya daktari na mgonjwa na hivyo “kufyekelea mbali” dhana ya mgonjwa kuwa kama mzigo au kichokoo! Ni katika muktadha huu anasema Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, Kanisa linayakabili matatizo na changamoto za kiuchumi na kijamii, kwa kubainisha mambo hasi katika mfumo wa shughuli za fedha, uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa bahati mbaya shughuli hizi zote zimekuwa zikitoa kipaumbele cha kwanza kwa faida kubwa.

Katika hali na mazingira ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19, familia ya binadamu itajikuta ikiwa inakabiliwa na hali ngumu sana. Leo na kesho ya mwanadamu haiwezi hata kidogo kufumbatwa katika uchumi na fedha peke yake, bila kugusa uchumi shirikishi unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu. Kanisa linawahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanaibua sera na mikakati ya ujenzi wa uchumi fungamani unaofumbatwa katika kanuni ya haki jamii,  umoja na mshikamano wa kibinadamu, ili kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii na wala si kwa ajili ya kupata zaidi. Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ujenzi wa mahusiano badala ya “biashara”. Ni matumaini ya Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwamba, kipeo cha janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kitaweza kupita kwa haraka, kwani ni janga ambalo limewagusa na kuwatikisa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Mwishoni amemwombea, Baba Mtakatifu Francisko: heri na baraka; furaha, afya tele na miaka mingi ya huduma, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo, Ushuhuda wa Kikristo ulimwenguni na kwa binadamu wote!

Ujumbe kwa Papa Francisko

 

05 July 2020, 10:16