Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 30 Julai 2020 Inaadhimisha Siku ya Mapambano Dhidi ya Biashara haramu ya Binadamu na Mfumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 30 Julai 2020 Inaadhimisha Siku ya Mapambano Dhidi ya Biashara haramu ya Binadamu na Mfumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. 

Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Kimataifa, Julai 30!

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kupambana na saratani ya biashara ya binadamu na mifumo yote inayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mtandao wa Mashirika ya Kikristo Dhidi ya Utumwa Mamboleo, COATNET.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2020 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Hii siku ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ili kusaidia juhudi za kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha ya binadamu, haki msingi, utu na heshima yake. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Lakini, huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, hii ni saratani inayowatumbukiza watu wengi katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo hata hapa mjini Roma. Hawa ni watu wanaohusishwa na biashara na utalii wa ngono sehemu mbali mbali za dunia, biashara ya viungo vya binadamu, kazi za suluba, wizi na ujambazi wa kulazimishwa. Wakati mwingine, wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, limetumiwa ili kuwatumbukiza watu katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete, kupambana na vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Jambo la msingi ni wateja wa biashara ya ngono kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kubadilisha mtindo wa maisha na kwa njia hii, biashara ya binadamu, ngono na utumwa mamboleo vitaweza kusitishwa kutoka katika uso wa dunia. Tabia ya watu kukengeuka na kutopoea katika dhuluma na nyanyaso mbali mbali, inaweza kurekebishwa kwa mtu binafsi kuzama katika undani wake na kuanza kuchunguza dhamiri, hali hii inaweza pia kuwa katika ngazi ya kijamii na hatimaye, Kanisa katika ujumla wake. Aina yoyote ile ya ukahaba ni tendo linalonyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu, kiasi cha kuwatumbukiza wahusika katika dimbwi la utumwa. Huu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu na ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha vilema vya dhambi. Huu ni ukatili unaovishwa “gunia la upendo”.

Matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu yanaacha ukakasi katika dhamiri za watu, kwa kuwageuza wasichana na wanawake kuwa kama bidhaa zinazouzwa na kununuliwa sokoni. Huu ni ugonjwa unaoendelea kuwaandama walimwengu na kwa hakika ni mwelekeo potofu wa maisha. Mchakato wa kuwakomboa wasichana na wanawake hawa kutoka katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni tendo la huruma, ni dhamana na wajibu wa watu wote. Kilio cha wasichana na wanawake waliotumbukizwa katika biashara ya ngono, hakiwezi kuendelea kugonga mwamba, bali kinapaswa kusikilizwa na kupewa jibu makini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake. Asiwepo mtu awaye yote anayewageuzia wasichana na wanawake hawa kisogo au “kunawa mikono” kama ilivyokuwa kwa Pilato, kwamba, hayamhusu hata kidogo. Hii ni damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika kwenye barabara mbali mbali ulimwenguni anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa uchungu mkubwa!

Wakati huo huo, Bwana Aloysius John, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, sauti na mtetezi wa wanyonge anasema, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kupambana kufa na kupona na saratani ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo yote inayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mtandao wa Mashirika ya Kikristo Dhidi ya Utumwa Mamboleo, COATNET kutoka katika nchi 39 inasema, takwimu za Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa mwaka 2016 zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 24.9 ambao wametumbukizwa katika biashara na mifumo ya utumwa mamboleo.

Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu, UNODC inasema, asilimia 71% ya waathirika wote ni wanawake na watoto. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 usiwe ni kisingizio cha kushindwa kuwahudumia waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuunda na kujenga mitandao ya kijamii itakayosaidia kudumisha ulinzi na usalama na waathirika, kwa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi sanjari na msaada wa huduma ya afya, kisheria na kisaikolojia, ili kuwasindikiza hatua kwa hatua katika mchakato wa kuandika tena historia mpya ya maisha yao.

Wakimbizi, wahamiaji na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika sekta isiyokuwa rasmi, wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ya kuweza kutumbukizwa katika biashara na mifumo ya utumwa mamboleo. Caritas Internationalis inawataka viongozi wa Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, wahanga hawa wanatendewa haki pamoja na kupatiwa huduma msingi kwa ajili ya maisha yao. Watoto walindwe dhidi ya nyanyaso za kijinsia pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; nyanyaso zinazo tekelezwa kwenye internet na mitandao ya kijamii. Hii ni dhamana ya watu wote wenye mapenzi mema kuwa macho na makini dhidi ya wale wote wanaotaka kuendeleza biashara na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Utumwa Mamboleo 2020
29 July 2020, 13:25