Vatican News
Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki, CPA., anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki, CPA., anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (Vatican Media)

Papa: Ujumbe Kwa Shirikisho la Waandishi Habari Wakatoliki, CPA.

Shirikisho lina wachapaji 225 na wanachama hai 600, wanaojishughulisha kutoa machapisho mbali mbali yanayowafikia watu zaidi ya milioni 10 huko nchini Marekani. Lengo na utume wa Shirikisho hili ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kauli mbiu inayoongoza mkutano wa mwaka 2020 ni “Wamoja katika tofauti”. Mazingira ya Virusi vya COVID-19!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioathirika kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Anawakumbuka na kuwaombea wale wote wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Anapenda kuchukua fursa hii, kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Hii ni  sehemu ya utangulizi wa ujumbe wa Baba Mtakatifu aliowaandikia washiriki wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki, “Catholic Press Association, CPA” kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 2 Julai 2020.

Mkutano huu kwa mara ya kwanza unafanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii. Shirikisho hili lilianzishwa Mwezi Agosti 1911. Leo hii, Shirikisho lina wachapaji 225 na wanachama hai 600, wanaojishughulisha kutoa machapisho mbali mbali yanayowafikia watu zaidi ya milioni 10 huko nchini Marekani. Lengo na utume wa Shirikisho hili ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kauli mbiu inayoongoza mkutano wa mwaka 2020 ni “Wamoja katika tofauti”. Hili ni wazo ambalo limeibuliwa wakati wa utekelezaji wa itifaki ya mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa kunako mwaka 2019 uliongozwa na kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25): Kutoka Jumuiya ya mtandaoni kwenda kwenye Jumuiya halisi ya watu!

Hii ni changamoto ya ujenzi wa Jumuiya halisi ya binadamu!  Baba Mtakatifu alikazia mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano ili kudumisha mtandao wa urafiki. Katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19, watu wengi wameguswa na kufurahia juu ya ukweli huu. Katika kipindi hiki ambacho watu wengi walikuwa wamewekwa karantini, wamegundua umuhimu na mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vyombo vya mawasiliano vimeweza kuwaunganisha watu na kufupisha umbali uliokuwepo na kuendelea kuwapatia habari muhimu na hivyo kuwasaidia watu kufungua nyoyo zao ili kuweza kuupokea ukweli huu.

Kwa mara ya kwanza gazeti nchini Marekani lilichapishwa kunako mwaka 1822 yaani Gazeti la “Charleston Catholic Miscellany” lililoanzishwa na Askofu John England na tangu wakati huo, kukafuatia mnyororo wa magazeti na majarida yaliyochapishwa nchini Marekani. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko mwelekeo wa Jamii bado unaendelea kutegemea habari kutoka kwenye magazeti, radio, luninga na mitandao ya kijamii, ili kuweza kukoleza “beneke” la mawasiliano, kwa kuhabarisha na kuwaunganisha watu. Wazo la “E pluribus unum” yaani: “Wamoja katika tofauti” ni changamoto kwa watu wa Mungu nchini Marekani kujizatiti katika huduma pamoja na kutafuta, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuondokana na kinzani na uvunjifu wa haki msingi binadamu. Jamii inahitaji vyombo vya mawasiliano ya jamii, vyenye uwezo wa kujenga madaraja ya kuwaunganisha watu.

Vinahitajika vyombo vya mawasiliano vyenye nguvu ya kuvunjilia mbali kuta zinazoonekana na zile zisizoonekana, lakini bado zinawatenganisha watu. Jamii inahitaji vyombo vya mawasiliano vitakavyowasaidia watu na hasa vijana kuunda dhamiri nyofu, yaani uwezo wa kupambanua mema na mabaya, kwa kuangalia ukweli wa mambo bila kupindisha pindisha. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, watu wa Mungu wanahitaji vyombo vya mawasiliano ya jamii vitakavyosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; maridhiano ya kijamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jamii inawahitaji wadau wa mawasiliano watakaosimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya mawasiliano bora ya jamii, dhidi ya watu wachache wanaotaka kuharibu sheria, kanuni na taratibu hizi kwa mafao yao binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau katika sekta ya mawasiliano ya jamii, kuungana na kushikamana wao wenyewe, kwani Kanisa linathamini sana mchango wa vyombo vya upashanaji habari. Hii inatokana na ukweli kwamba, ndani ya Kanisa, waamini wote wamebatizwa katika Roho Mtakatifu na wote wanaunda Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni katika muktadha huu, kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anachangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa njia ya weledi unaofumbatwa katika ukweli katika upendo, ili hatimaye, Kanisa liweze kukua na kushamiri katika Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, wanahabari wa kweli wasiokuwa na hila ndani mwao ni wale wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao, kama mtu binafsi, jamii na familia ya binadamu katika ujumla wake. Hawa ni watu wanaozama  katika shughuli zao, ili kushuhudia ukweli wanaotaka kuutangaza. Mawasiliano yanabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, linalowashirikisha waja wake amana na utajiri wa Kimungu, ili hata wao, waweze kuwashirikisha wengine, amana na utajiri huu. Baba Mtakatifu anawaombea wajumbe wote karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa na hekima, uelewa wa kutosha, ili hatimaye, waweze kutoa ushauri mwema. Wawe ni vyombo vya faraja na matumaini kwa watu wanaotafuta ukweli kwa wote.

Huu ni mwaliko wa kuvunjilia mbali saratani ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki na amani; hali ya kutowajali na kuwathamini wengine; mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na familia ya binadamu. Kwa njia ya sadaka na majitoleo yao katika kazi, wawasaidie jirani zao kuweza kutafakari matukio mbali mbali ya maisha kwa macho ya Roho Mtakatifu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa Katoliki wajitahidi kuzungumza lugha inayopania kukuza na kudumisha ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wawe mstari wa mbele kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali na mazingira yao. Wawe ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti; watu wanaohitaji huruma na hatimaye, kuweza kueleweka. Amewataka wadau wote kuendelea kuungana pamoja katika sala na utume huu nyeti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Papa: Vyombo vya Habari

 

01 July 2020, 13:45