Tafuta

Pope Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini  katika Uwanja wa Mtakatifu Petro  Pope Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro  

Papa Francisko:Ni uvumilivu kwa adui na Mungu atatoa malipo kwa waovu!

Yesu anatufanya tutambue uvumilivu wa Mungu kwa kutufungulia moyo wetu matumaini. Bwana anatualika kuwa na mtazamo kama wake unaotazama juu ya ngano nzuri na ambaye anajua kuitunza hata katikati ya magugu.Ndiyo tafakari ya Papa,Jumapilitarehe 19 Julai 2020 kabla ya sala ya Malaika wa Bwana kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro,Vatican.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Kabla ya sala ya Malaika wa Bwana Papa Francisko, Jumapili, tarehe 19 Julai  2020 kwa  kwa mahujaji na waamini waliofika katika uwanja vya Mtakatifu Petro amewasalimia na kuanza kusema “Katika Injili ya leo kutoka Matayo 13,24-34 tunakutana tena na Yesu akiwa makini kuzungumza kwa watu kwa kutumia misemo yake kuhusu  Ufalme wa mbingu. Nitajikita katika neno la kwanza tu linalohusu magugu, ambapo Yesu anatufanya tutambue uvumilivu wa Mungu kwa kutufungua moyo wetu katika matumaini. Akiendelea Papa anasema “Yesu anasimulia kuwa katika konde lililopandwa mbegu njema katikati yake ikatokeza hata magugu, yaani neno ambalo linajumuisha magugu yote mabaya, ambayo uharibu ardhi”. Na kati yetu, tunaweza kusema kwamba hata leo hii, udongo umeharibiwa na mimea ya kuuliwa na dawa ya wadudu na ambayo mwishowe huumiza nyasi, ardhi na afya. Lakini hii ni katika mabano”, Papa Francisko amesisitiza.

 Lazima kusubiri wakati wa mavuno

Papa amesema “Watumwa kwa maana hiyo walikwenda kwa bwana ili kujua magugu yametoka wapi na yeye akawajibu:“Adui ndiye aliyetenda hivi”(13,28). Kwa kuongezea, ni kwa sababu tumepanda ngano nzuri! Adui, ambaye anashindana, amekuja kufanya hivi. Kwa maana hiyo watumwa hawa wangependa kwenda mara moja kung’oa magugu ambayo yanakua; badala yake mmiliki anasema hapana, kwa sababu kuna kuhatarisha kukusanya magugu na kung’oa ngano. Ni lazima tusubiri wakati wa mavuno: hapo ndipo vitatengenishwa na magugu yatachomwa. Papa Francisko ameongeza hadithi hii ina maana. Inawezekana kusoma mfano huu katika maono ya historia. Karibu na Mungu mmiliki wa shamba na ambaye daima hupanda mbegu nzuri tu, kuna hata adui, ambaye hueneza magugu ili kuzuia ukuaji wa ngano. Bwana hutenda kazi yake akiwa wazi, kwa mwanga wa jua, na kusudi lake ni mavuno mazuri; na mwingine, mpinzani, kinyume chake, anatumia fursa ya giza la usiku na kufanya kazi kwa wivu, kwa ajili ya vizingiti na uadui ili kuharibu kila kitu.

Sisi wanadamu tunaweza kumfuata Mungu au shetani

Papa Francisko amesema,  mpinzani ambaye Yesu anamtaja analo jina, yaani  ni Ibilisi, mpinzani dhidi ya uzuri wa Mungu. Kusudi lake ni kuzuia kazi ya wokovu, na kuhakikisha kwamba Ufalme wa Mungu unazuiliwa na wahudumu wasio waadilifu, na wapandaji wa kashfa. Kiukweli, mbegu nzuri na magugu haviwakilishwi  na wema na ubaya katika mfano usio halisi, hapana; lakini ni kwetu sisi wanadamu, ambao tunaweza kumfuata Mungu au shetani. Kwa kutolea mfano mwingine Papa Francisko amesema “Mara nyingi, tumesikia kwamba familia ambayo ilikuwa ya amani, baadaye ilianza kuwa na vita na wivu … kitongoji ambacho kilikuwa na amani, baadaye unasikia yameanza  mambo mabaya ... Na sisi tumezoea kusema: “Eh, kuna mtu amefika huko kupanda magugu”, Au “ mtu huyu wa familia, na maneno yake, anapanda magugu”. Daima ni kupanda uovu unaoharibu. Na hii hufanywa kila wakati na shetani au kishawishi chetu: wakati tunapoingia katika majaribu ya kusengenya ili kuwaangamiza wengine.”

Yesu alikuja kutafuta wenye dhambi badala ya wenye haki

Lengo la watumwa ni kuondoa uovu mara moja, yaani watu waovu, lakini bwana ni mwenye busara, anaona mbali zaidi: lazima ajue jinsi ya kungojea, kwa sababu kuvumilia mateso na uadui ni sehemu ya wito wa Kikristo. Ubaya, kwa hakika lazima ukataliwe, lakini waovu ni watu ambao lazima mtu awe na uvumilivu. Hii haimananishi jambo la uvumilivu kinafiki ambao huficha maelewano, bali ni wa haki itokanayo na huruma. Ikiwa Yesu alikuja kutafuta wenye dhambi badala ya wenye haki, kuponya wagonjwa hata kabla ya wenye afya (cf Mt 9,12-13), hata kwa hatua yetu sisi wanafunzi wake, lazima pia kutokukandamiza waovu, bali kuwaokoa. Na hapo ndipo panahitajika uvumilivu

Tuwe na mtazamo moyoni mwetu wa kutazama ngano nzuri hata katikati ya magugu

Papa Francisko akisisitiza zaidi amesema “Injili ya leo inawakilisha njia mbili za kutenda na historia ya kuishi, kwa upande mmoja ni kuwa na mtazamo wa bwana, ambaye anaona mbali na kwa upande mwingine, kuwa na mtazamo wa watumwa ambao wanaona shida. Watumwa moyoni mwao wanajali shamba lisiwe na magugu na wakati huo huo mmiliki moyoni mwake ni kuona ngano nzuri. Bwana anatualika kuwa na mtazamo huo huo unaotazama juu ya ngano nzuri na ambaye anajua kuitunza hata katikati ya magugu.

Wale wanaotafuta vizingiti na kasoro za wengine

Wale ambao wanatafuta vizingiti na kasoro za wengine hawashirikiani vizuri na Mungu, badala yake wale ambao wanajua jinsi ya kutambua wema ambao unakua kimya kimya katika shamba la Kanisa na katika historia, huku wakipalilia hadi ukomavu. Na kwa maana hiyo atakuwa Mungu, na ni Yeye tu, ataweza kutoa malipo mema na kuwaadhibu waovu. Bikira Maria atusaidie kuelewa na kuiga uvumilivu wa Mungu, ambaye hataki mtoto yeyote apotee na ambaye anampenda kwa upendo wa Baba.

20 July 2020, 07:38