Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. 

Tanzia: Kardinali Zenon Grocholewski: 1939 - 2020!

Kardinali Zenon Grocholewski, alizaliwa tarehe 11 Oktoba 1939 huko Bròdki, nchini Poland. Tarehe 27 Mei 1963, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 21 Desemba 1982 akateuliwa kuwa Askofu na kumweka wakfu tarehe 6 Januari 1983. Tarehe 16 Desemba 1991 akateuliwa kuwa Askofu mkuu. Tarehe 21 Februari 2001 akateuliwa kuwa Kardinali. Tarehe 17 Julai 2020 akafariki dunia. RIP Baba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambirambi Bwana Władisław Grocholewski, kufuatia kifo cha kaka yake, Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kilichotokea tarehe 17 Julai 2020, mjini Roma, akiwa na umri wa miaka 81. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatumia salam za rambirambi wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito wa Kardinali Zenon Grocholewski. Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Kardinali Grocholewski kwa moyo wa shukrani kutokana na sadaka na majitoleo yake kama Jaalimu wa Sheria za Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran. Alibahatika kuwa na karama ya kutunga vitabu vya kisayansi.

Lakini kwa namna ya pekee kabisa, Kardinali Zenon Grocholewski alijipambanua kwa ajili ya huduma mjini Vatican kwanza kabisa kama Katibu Mkuu na baadaye kama Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kanisa. Baadaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. Katika nyadhifa zote hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Zenon Grocholewski ameshuhudia ile ari ya Kipadre, Uaminifu kwa Injili ya Kristo pamoja ujenzi wa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu anapenda kumwombea Marehemu Kardinali Zenon Grocholewski, kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ili sasa aweze kumkirimia mtumishi wake mwaminifu tuzo la maisha na uzima wa milele alilowaandalia wafuasi wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanao omboleza msiba huu mzito.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki alizaliwa tarehe 11 Oktoba 1939 huko Bròdki, nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 27 Mei 1963, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Poznan. Baada ya utume wake Parokiani katika kipindi cha miaka mitatu, alitumwa kwenda Roma ili kujiendeleza zaidi katika elimu ya juu na hatimaye, akajipatia shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian. Kazi yake ya utafiti aliiandikwa kwa lugha ya Kilatin na kuibuka kuwa ni mwanafunzi bora kwa mwaka 1972. Tangu mwaka 1972 hadi mwaka 1999 kwa nafasi mbali mbali aliweza kuitumikia Mahakama Kuu ya Kanisa hadi kufikia ngazi ya kuwa ni Mwenyekiti wake.

Hayati Kardinali Zenon Grocholewski aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Kati ya wajumbe saba walioandika Muswada wa Gombo Jipya la Sheria za Kanisa la Mwaka 1983. Aliendelea kufundisha Sheria za Kanisa kwenye Vyuo Vikuu vya Kipapa mjini Roma pamoja na Chuo cha “Studio Rotale”. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 21 Desemba 1982 akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kumweka wakfu tarehe 6 Januari 1983. Tarehe 16 Desemba 1991 akateuliwa kuwa Askofu mkuu. Tarehe 15 Novemba 1999 akateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na kung’atuka kutoka madarakani tarehe 31 Machi 2015. Tarehe 21 Februari 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali. Tarehe 17 Julai 2020 akafariki dunia na Ibada ya mazishi kufanyika tarehe 18 Julai 2020 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Papa: Tanzia: Kardinali Zenon

 

 

18 July 2020, 14:13