Baba Mtakatifu Francisko: Bikira Maria wa Mlima Karmeli: Utuombee! Baba Mtakatifu Francisko: Bikira Maria wa Mlima Karmeli: Utuombee! 

Papa Francisko: Bikira Maria wa Mlima Karmeli: Utuombee!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anamwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia waamini kuwa na mikono isiokuwa na mawaa pamoja na mioyo safi. Wawe makini katika kutumia vyema ndimi zao, ili wasiwe ni watu kusema mabaya ya jirani zao. Waamini wanaweza kupanda juu ya mlima wa Bwana, ili kujipatia neema na baraka; haki na wokovu wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Julai, anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Mama huyu anaheshimiwa na wengi kama Malkia, Mlinzi na Mhudumu wa Injili ya Upendo kwa Mungu na jirani. Bikira Maria wa Mlima Karmeli ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika: maisha ya sala endelevu na dumifu; katika hali ya kimya kikuu na tafakari ya kina. Ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kufunga, kujinyima na kujisadaka kwa ajili ya jirani na umuhimu wa kudumisha ufukara kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anamwomba Bikira Maria wa Mlima Karmeli ili aweze kuwasaidia waamini kuwa na mikono isiokuwa na mawaa pamoja na mioyo safi. Wawe makini katika kutumia vyema ndimi zao, ili kamwe wasiwe ni watu kusema mabaya wala kuwaseng’enya jirani zao. Katika hali na mazingira kama haya, waamini wanaweza kupanda juu ya mlima wa Bwana, ili kujipatia neema na baraka; haki na wokovu wake! Tunawakatia heri na baraka Mapadre na Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu popote pale walipo, wanapoendelea kuchakarika kila kukicha kama wamisionari walioitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; huku wakiendelea kujizatiti katika mchakato wa utakatifu wa maisha, kwa kudumisha upendo wa kidugu. Daima wawe tayari kusoma alama za nyakati kwa kutambua utajiri wa changamoto za tamaduni na ari ya kumpeleka Kristo Yesu hasa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii kadiri ya roho na karama ya waasisi wa Mashirika yao.

Papa: Bikira Maria wa Mlima Karmeli
16 July 2020, 13:53