Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Idara ya Afya Jimbo Kuu la Roma kwa sadaka na utume wao wakati wa kipeo cha janga la COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Idara ya Afya Jimbo Kuu la Roma kwa sadaka na utume wao wakati wa kipeo cha janga la COVID-19. 

Papa Awashukuru Wajumbe wa Idara ya Afya Jimbo la Roma

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha moyo wa shukrani kwa wawakilishi wa Idara ya Afya, Jimbo kuu la Roma. Amewakumba wakleri, watawa na waamini walei waliojisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Papa Francisko katika barua yake kwa mapadre wa Jimbo la Roma, ameshukuru!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya Utume wa Bahari, iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2020, aliwasalimia waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia waliofika uwanjani hapo na wale wote waliokuwa wanafuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu ameonesha moyo wa shukrani kwa wawakilishi wa Idara ya Afya, Jimbo kuu la Roma. Amewakumba wakleri, watawa na waamini walei waliojisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake kwa Mapadre wa Jimbo la Roma aliwashukuru kwa ushuhuda wenye ujasiri na ukarimu uliowawezesha kujenga na kudumisha Injili ya upendo na ukarimu kwa wagonjwa na maskini. Aliwataka kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo, ili waweze kuonja tena amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Anawashukuru wakleri kwa sababu wamesimama imara na kutembea bega kwa bega na waamini wao bila ya kuwatelekeza. Wakleri wameguswa na kuonja mateso, mahangaiko na mauti ya watu wa Mungu katika Parokia zao. Kwa hakika wamejaribiwa na kutikiswa katika undani wa maisha na imani yao, lakini bado wamebaki kuwa imara katika imani, matumaini na mapendo.

Kama Jumuiya ya waamini wameomboleza na kulia kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro. Fumbo la Msalaba, bado linaendelea kuwagusa hata watu wasiokuwa na hatia. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu ni watu wa Mungu kuendelea kuwa macho kwa kufuata ushauri wa madaktari na wataalamu wa afya. Kanisa liendelee kujikita katika kipaji cha ugunduzi katika maisha na utume wake, ili liendelee kuwa ni chombo cha wokovu na matumaini. Kristo Mfufuka kama alivyofanya kwa wale Wafuasi wa Emau, anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Watu wa Mungu wawe na ujasiri wa kukabiliana na hali halisi ya maisha yao kwa jicho la imani, waomboleze na wale wote wanaoomboleza kwa sababu hata machozi ni kielelezo cha utakatifu. Wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia ujasiri na mwono mpana zaidi wa kukiishi kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19, kwa imani na matumaini; kwa kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zinazomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kila mwamini ajitahidi kuwa ni Msamaria mwema kwa jirani zake. Wakleri wasimame imara katika imani, wawe wanyenyekevu, ili waweze kushiriki pia mateso ya watu wa Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jambo la msingi ni kupenda na kuhudumia kwa dhati kabisa!

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wanachama wa Chama cha Kitume cha Wafokolari. Chama hiki cha kitume kilianzishwa kunako mwaka 1964 na kimekuwa ni maabara ya umoja na udugu wa kibinadamu, unaowaunganisha watu zaidi ya 850 kutoka katika mataifa 65. Hiki ni kitovu cha: udugu, upendo, ukarimu na majadiliano katika uhalisia wa maisha ya watu yanayofumbatwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Chama ambacho kimeendelea kujizatiti  katika malezi na majiundo ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Makao makuu ya Chama hiki huko Loppiano ni kitovu cha karama, maisha na utume wa Chiara Lubich. Hapa ni mahali ambapo tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ni mahali ambapo waamini walei kwa njia ya ushuhuda wa maisha, wanajitahidi kuyatakatifuza malimwengu. Ni mahali pa sala, tafakari, maisha na kazi.

Papa: Idara ya Afya Roma

 

 

13 July 2020, 07:49