Baba Mtakatifu Francisko amechangia kiasi cha Euro 25, 000 kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP ili kupambana na athari za Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko amechangia kiasi cha Euro 25, 000 kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP ili kupambana na athari za Corona, COVID-19. 

Papa Francisko achangia Kiasi cha Euro 25, 000 Kwa Shirika la WFP

Papa Francisko kupitia katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kushirikiana na Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD, amechangia kiasi cha Euro 25 Elfu katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wadau mbali mbali walijitokeza na kujifunga kibwebwe kupambana na janga kubwa la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa ukarimu na uwajibikaji mkuu. Hizi ni juhudi zilizowaunganisha watu katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii na kiroho. Madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wametekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu na ushupavu wa hali ya juu kabisa, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao na familia zao. Kuna baadhi yao wameambukizwa na wengine wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Janga la Corona, COVID-19 limegusa na kutikisa maisha ya watu na historia ya Jumuiya. Kuna kila sababu ya kuendelea kuenzi mateso ya wagonjwa na wale wote waliofariki dunia; hususan wazee. Hili ni kundi ambalo kamwe, uzoefu na mang’amuzi yao ya maisha hayawezi kusahauliwa, kwa ajili ya ujenzi wa kesho iliyo bora zaidi. Hii ni dhamana inayohitaji uwajibikaji na sadaka ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo wenye ukarimu pasi na makuu ambao umeacha chapa ya kudumu na isiyoweza kufutika kwenye dhamiri na mafungamano ya kijamii, kwa kuwafundisha watu umuhimu wa ujenzi wa ujirani mwema; huduma makini na sadaka kwa ajili ya kuhamasisha udugu wa kibinadamu na utulivu mkubwa. Inawezekana kabisa, watu wa Mungu kutoka katika kipeo hiki cha mahangaiko ya maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema, wakiwa imara zaidi, mambo yanayotegemea dhamiri nyofu na uwajibikaji wa kila mmoja, kwa kutegemea na kuambata neema ya Mungu. Ni wajibu wa waamini kutangaza na kushuhudia kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake, hata katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Msalaba, hata waamini nao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wanaweza kupambana na matatizo na changamoto pevu, hatimaye wakaweza kuibuka kidedea! Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili aweze kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na dhana ya uchoyo na ubinafsi, mambo yanayoonekana kuwa kama ni dira na mwongozo wa maisha ya walimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa angalisho kwa watu wote wa familia ya Mungu kutojisahau kwani mara tu baada ya kipeo cha janga la Corona, COVID-19 wakajikuta wakitumbukia katika ombwe na hali ya kufikirika. Ni rahisi sana kuwasahau majirani; au watu wengine wanaowahudumia. Daima wakumbuke kwamba, kuna watu wanaowatia shime na ujasiri wa kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kupitia katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kushirikiana na Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, amechangia kiasi cha Euro 25 Elfu katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa Baba Mtakatifu na Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya madhara makubwa yaliyosababishwa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Mchango huu ni ushuhuda wa uwepo na ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa wahanga wa Virusi vya Corona, COVID-19. Ni msaada unaolenga kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili kuweza walau kupata mahitaji yao msingi. Aidha, Baba Mtakatifu anatambua mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP.,  katika nchi zinazoendelea, kama sehemu ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushikamana ili kusaidia maboresho katika miundombinu ya sekya ya afya; kuendelea kuimarisha amani na utulivu pamoja na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Janga la Corona, COVID-19 limepelekea ukosefu mkubwa wa fursa za ajira, kiasi kwamba, kuna mamilioni ya watu ambao kila kukicha wanaendelea kutumbukia katika janga la umaskini wa hali na kipato. Hali hii inachangia pia kuporomoka kwa sera na mifumo ya uchumi wa nchi changa zaidi duniani!

Papa: Mchango WFP.

 

04 July 2020, 14:03