Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Mazingira Duniani, tarehe5 Juni 2020: Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ya wote! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Mazingira Duniani, tarehe5 Juni 2020: Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ya wote!  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Mazingira Duniani 2020

Papa Francisko anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na pamoja na kuheshimu masuala ya bayoanuai ni mambo yanayowaathiri watu wote. Dunia kamwe haiwezi kujidai kwamba, ina afya bora wakati inachechemea kwa kuathirika kwa majanga mbali mbali. Madonda ya Mama Dunia yanayoendelea kuchuruzika damu, yana athari zake pia katika maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Mazingira Duniani ilianzishwa na Umoja wa Mataifa na inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Juni. Ni maadhimisho yanayowashirikisha wadau mbali mbali ili kujizatiti kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Bayoanuai-suala linalopaswa kushughulikiwa kwa dharura”. Majanga mbali mbali ambayo yameikumba dunia kwa siku za hivi karibuni ni viashiria kwamba, wanadamu wanategemea na kukamilishana na viumbe wengine. Huu ni wakati muafaka wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwajibika barabara katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira.

Mji mkuu wa Bogotà nchini Colombia, ulipaswa kuwa ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa Mwaka 2020. Lakini kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 maadhimisho haya yanafanyika kwa njia ya mtandao. Changamoto hii ni kubwa kwa sababu inaonesha umuhimu wa watu kushirikiana na kushikamana katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Rais Iván Duque Márquez wa Colombia, akimpongeza kwa nchi yake kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na pamoja na kuheshimu masuala ya bayoanuai ni mambo yanayowaathiri watu wote bila ubaguzi.

Dunia kamwe haiwezi kujidai kwamba, ina afya bora wakati inachechemea kwa kuathirika kwa majanga mbali mbali. Madonda ya Mama Dunia yanayoendelea kuchuruzika damu, yana athari zake pia katika maisha ya mwanadamu. Utunzaji bora wa bayoanuai ni changamoto kubwa ya kuangalia masuala mapana ya mbeleni badala ya kujikita katika mchakato unaopania kupata faida kubwa na kwa haraka. Mtazamo huu anasema Baba Mtakatifu hauna budi kukita mizizi yake katika maisha ya binadamu na kujielekeza zaidi katika utunzaji bora wa mazingira kwa mafao ya wengi. Watu wanapaswa kuwa makini kutokana na athari kubwa za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote kwa sasa, ili kutenda kwa busara badala ya kuendelea kukaa kimya kana kwamba, hakuna jambo lolote lile linalotokea!

Uharibifu mkubwa wa mazingira unaendelea kusababisha gharama kubwa. Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya watu wenye uchu wa kupata faida kubwa, kwa kisingizio cha maendeleo, wanaendelea kuitumbukiza Jumuiya ya Kimataifa katika mahangaiko makubwa. Bado binadamu anayo fursa ya kurekebisha hali ya sasa, kwa kujizatiti zaidi ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili dunia iweze kuwa na afya bora zaidi na hatimaye, kizazi hiki kiweze kukirithisha kizazi kijacho dunia iliyo bora zaidi. Lakini kila kitu kinategemea, kile ambacho watu wanataka kwa wakati huu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi karibuni, Kanisa limeadhimisha kumbukumbu ya Miaka 5 tangu alipochapisha Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira yaani: “Laudato si”. Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa maendeleo fungamani yanayojikita katika kanuni maadili na utu wema, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza sanjari na kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Kilio cha Mama Dunia kinapaswa kusikilizwa na kupatiwa majibu muafaka.

Ni kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu ametangaza “Mwaka wa Laudato si”, fursa muhimu ya kutafakari kwa pamoja kuhusu amana na utajiri unaofumbatwa katika Waraka huu wa kitume, ili watu waweze kujizatiti zaidi katika kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Hii pia ni changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Rais Iván Duque Márquez wa Colombia, utekezaji mwema wa dhamana na majukumu yaliyoko mbele yake, ili kujenga na kudumisha mazingira bora, yatakayowawezesha watu kuishi vizuri zaidi, kila mtu akiwa na nafasi yake na wala asiwepo mtu hata mmoja anayebakia nyuma!

Papa: Colombia

 

 

 

06 June 2020, 09:22