Papa Francisko amewatumia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Papa Francisko amewatumia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mabaharia, Wavuvi na Familia Zao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha na kazi ya mabaharia pamoja na wavuvi imeonesha umuhimu wake wa pekee katika kipindi hiki, kwa sababu wamesaidia sana kutoa chakula pamoja na mahitaji msingi kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa mabaharia pamoja na familia zao anasema, Jumuiya ya Kimataifa inapitia kipindi kigumu katika historia yake kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Maisha na kazi ya mabaharia pamoja na wavuvi imeonesha umuhimu wake wa pekee katika kipindi hiki, kwa sababu wamesaidia sana kutoa chakula pamoja na mahitaji msingi kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao. Anatambua fika hatari za maisha wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Wametumia muda mrefu zaidi wakiwa kwenye vyombo vyao bila ya kuruhusia kutua nanga kwa hofu ya kusambaza maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19. Wameendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kutengwa na ndugu, jamaa, marafiki na hata nchi zao wenyewe.

Matatizo na changamoto zote hizi si rahisi sana kwa wao kuweza kuzibeba na hasa katika kipindi hiki! Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, wasidhani wako pweke na kwamba, wamesahauliwa. Kwa njia ya maisha na utume wao baharini unaweza kuwajengea mazingira kwamba, wako pweke, lakini watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawahifadhi na kuwaombea kila wakati kutoka katika undani wa moyo wake. Sala hii inasindikizwa pia na wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Utume wa Bahari, maarufu kama “Stella Maris” yaani “Nyota ya Bahari”. Injili Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, walikuwa ni wavuvi. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwapatia ujumbe; sala ya matumaini na faraja mintarafu matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao. Anapenda pia kuwatia shime, wahudumu wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea, wanaoshirikiana nao bega kwa bega katika utume wa bahari kwa ajili ya mabaharia na wavuvi.

Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea wote pamoja na familia zao, heri na baraka. Anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira maria, Nyota ya uinjilishaji. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume na kuendelea kuwahakikishia kwamba, daima wako kwenye mawazo na sala zake. Amewasihi wao pia kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Mabaharia
18 June 2020, 13:40