Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani. 

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani, 29 Juni!

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 Baba Mtakatifu anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa Saa za Ulaya. Katika Ibada hii, atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa: Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Maaskofu wakuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2019-2020.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa Saa za Ulaya. Katika Ibada hii, atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa: Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Maaskofu wakuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2019-2020. Pallio takatifu  ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume kwa mwaka 2019 alikazia mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha ambayo yalisimikwa katika maisha ya kiroho kwani walikuwa ni wachamungu! Ni watu ambao walionesha udhaifu mkubwa wa kibinadamu, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kumkana Kristo Yesu mara tatu wakati ambapo Mtume Paulo alilidhulumu Kanisa la Kristo. Lakini wote hawa wakaoneshwa na kuonjeshwa upendo wa Kristo hasa pale Yesu alipomuuliza Mtume Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda, Petro akasononeka sana. Mtume Paulo akaulizwa kwanini alikuwa analidhulumu Kanisa lake? Wote wawili waliitwa kwa majina yao, hali ambayo iliwaletea toba na wongofu wa ndani.

Hawa ni wadhambi wawili waliotubu, ni watu ambao walitambua kwamba ni wadhambi na Yesu akachukua fursa hii kuwafanyia miujiza, kielelezo cha upendo wake, kwa wale wote wanaothubutu kumfungulia hazina ya nyoyo zao, kwa kujiweka mbele ya Kristo, ili aweze kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wake. Ni watu walioonesha moyo wa unyenyekevu hadi dakika ya mwisho wa maisha yao, kiasi hata cha Mtume Petro kusulubiwa miguu juu, kichwa chini! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, jina Paulo maana yake ni “mtu mdogo”, kielelezo cha unyenyekevu uliomfanya hata watu kusahau jina lake la asili, Saulo, aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli.

Mitume hawa wakatambua kwamba, utakatifu wa maisha unafumbwa katika unyenyekevu, kwa kutambua udhaifu na umaskini wao, kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyewatendea miujiza kwa kuwanyanyua juu, kwa njia ya Msamaha unaoganga na kuponya! Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa msamaha wa Kristo Yesu, uliowajalia toba na wongofu wa ndani, wakabahatika kuwa watu wapya, wenye furaha na amani ya ndani. Wakasahau ya kale na kuanza kuyaambata maisha mapya yaliokuwa yameboreshwa kwa upendo wa Kristo uliokuwa na nguvu kubwa kupita hata mapungufu na makosa yao ya kibinadamu. Huruma ya Mungu inawajalia waamini kuwa na maisha mapya, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao!

Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; mashuhuda wa msamaha unaoganga na kuponya na hatimaye, wakawa ni mashuhuda wa Masiha, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, nyakati zote ni zake; chemchemi ya upendo wa kweli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni ushuhuda unaobubujika kutokana na Mtume Petro kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake kama ilivyokuwa hata kwa Mtume Paulo anayelitaja jina la Kristo mara 400 katika nyaraka zake mbali mbali. Kwa Mtume Paulo, Kristo kwake ni nguzo ya maisha, kiasi kwamba, mambo yale yaliyokuwa faida kwake akayahesabu kuwa ni hasara kwa ajili ya Kristo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuwaangalia Mashuhuda hawa wa imani, ili kupyaisha maisha yao, hatimaye waweze kumfahamu Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao na wala wasikomee tu kwa yale yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii au kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kweli Kristo Yesu aweze kuwa ni nguzo ya maisha yao, tayari kuwasamehe, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha, kiasi hata cha kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda hai wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtaakatifu Francisko ametambua uwepo wa ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, mwendelezo wa mapokeo kwa Makanisa haya mawili. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza  hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko!

Watakatifu Petro na Paulo Mitume

 

27 June 2020, 09:22