Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni mwaliko kwa waamini kumtafakari Mungu Mmoja ambaye amejifunua katika Nafsi Tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni mwaliko kwa waamini kumtafakari Mungu Mmoja ambaye amejifunua katika Nafsi Tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. 

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Mungu Mmoja Katika Nafsi Tatu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mungu mwenyewe amelifunua Fumbo la Utatu Mtakatifu hatua kwa hatua katika historia ya wokovu; katika kazi ya Uumbaji, Ukombozi wa mwanadamu na katika Fumbo la kumtuma Roho Mtakatifu. Sherehe hizi zinawazamisha waamini katika maisha ya ndani kabisa ya Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu, kiini cha faraja, amani na utulivu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya Katekesi yake kuhusu Sala ya Abramu, Jumatano tarehe 3 Juni 2020 amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili tarehe 7 Juni 2020, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linakiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika Nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mungu mwenyewe amelifunua hatua kwa hatua katika historia ya wokovu; katika kazi ya Uumbaji, Ukombozi wa mwanadamu na katika Fumbo la kumtuma Roho Mtakatifu. Sherehe za Fumbo la Utatu Mtakatifu zinawazamisha waamini katika maisha ya ndani kabisa ya Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu, kiini cha faraja, amani na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea vijana, wagonjwa na wanandoa wapya na kuwataka kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu, Baba mleta uzima! Wawe tayari kufungua nyoyo zao na kuupokea upendo wake, unaoleta mabadiliko katika maisha yao kama mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Amewakumbusha watu wa Mungu kutoka nchini Poland kwamba, yuko pamoja na vijana watakaokutanika kwenye mkutano wa LEDNICA 2000, ambao kwa mwaka huu, unaingia awamu yake ya XXIV. Ni matumaini yake kwamba, vijana wengi wataweza kushiriki kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, ili kwa njia ya zawadi ya Roho Mtakatifu, vijana hawa waweze kupokea karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yanayowawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga angavu wa Kristo Mfufuka.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujiachilia kabisa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria “Totus tuus”. Wawe na ujasiri kwa sababu wanapaswa kuwa ni chemchemi ya baraka kwa wazazi wao. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana nao kwa njia ya sala. Ijumaa tarehe 5 Juni 2020, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Bonifasi, Mtume wa Ujerumani. Mtakatifu huyu awasaidie waamini kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yao kuwa ndiyo chemchemi ya maisha mapya, wokovu na matumaini. Waamini waendelee kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuwatumia kama mashuhuda wa imani tendaji katika jamii wanamoishi.

Papa: Utatu Mtakatifu

 

04 June 2020, 07:02