Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya waamini wanaomtegemea na kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Papa Francisko asema, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya waamini wanaomtegemea na kujiaminisha kwa Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Papa: Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Chemchemi ya Umoja na Wokovu

Papa: Ekaristi Takatifu inajenga Kanisa na ni chemchemi ya maisha na utume wake. Mtakatifu Paulo anasema, Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je, si ushirika wa Damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa Mwili wa Kristo? Baba Mtakatifu anasema, maneno haya yanaonesha Fumbo la Ekaristi Takatifu au kwa maneno mengine, maana ya Ekaristi Takatifu katika maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili tarehe 14 Juni 2020 wameadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo! Kwa lugha ya Kilatini Sherehe hii inajulikana kama Corpus Domini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 14 Juni 2020, amewaongoza waamini kwa tafakari ya kina kuhusu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho sura ya 10: 16-17 kuhusu Kikombe kile cha Baraka na Mkate ule mmoja unaomegwa kwa pamoja: hili ni fumbo na matokeo yake ujenzi wa Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kufafanua maana ya Kikombe cha Baraka na Ekaristi Takatifu kama chachu ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa Jumuiya unaowaunganisha na Kristo Yesu, Mkate wa maisha na uzima wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga Kanisa na ni chemchemi ya maisha na utume wake.

Mtakatifu Paulo anasema, Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je, si ushirika wa Damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa Mwili wa Kristo? Baba Mtakatifu anasema, maneno haya yanaonesha Fumbo la Ekaristi Takatifu au kwa maneno mengine, maana ya Ekaristi Takatifu katika maisha ya kiroho. Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai, anakuwa ni chemchemi ya wokovu wa watu wote. Kristo Yesu yuko katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kama chakula kinacholeta nguvu inayopyaisha maisha ya waamini na kuwapatia ari na moyo wa kuweza kusonga mbele, baada ya kusimama kitambo au kwa kuteleza na kuanguka. Ili Chakula hiki kiweze kufanya kazi inayotarajiwa, mwamini anapaswa kuwajibika barabata, kwa kufikiri na kutenda, vinginevyo maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ambayo waamini wanashiriki, zinabakia kuwa ni ibada tupu zisizo na mafao kwa waamini.

Kuhusu umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya waamini, Mtakatifu Paulo anakaza kusema, “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja”. 1 Kor 10:17. Kwa wale wanaoshiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu wanapaswa kushirikiana na kushibana kiasi cha kuwa ni mwili mmoja, kama ulivyo mkate unaomegwa na baadaye, waamini wanagawiwa! Kushiriki mwili wa Kristo ni alama ya umoja, ushirikiano na mshikamano, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Lakini, Kristo Yesu anatambua fika udhaifu na mapungufu ya waja wake kwamba, “hawawezi kufua dafu” kwa sababu daima wataendelea kukabiliana na vishawishi, kinzani, husuda pamoja na maamuzi mbele na matokeo yake ni mipasuko.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema hata katika muktadha huu, bado Kristo Yesu amethubutu kuwaachia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayoonesha uwepo wake wa daima, ikiwa kama wataendelea kushikamana na kufungamana naye. Ni kwa njia hii, hata waamini wataweza kupokea zawadi ya upendo wa kidugu! Hii inawezekana tu kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kumbe, Fumbo la Ekaristi Takatifu linawawezesha waamini kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano na Kristo Yesu sanjari na kujenga umoja miongoni mwa waamini. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, waamini wanalishwa chakula cha uzima, wanakua na kuendelea kupyaisha Jumuiya ya Wakristo.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kristo Yesu, Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Rej. LG. No.1. Kumbe ni kweli kabisa kwamba, Kanisa linatengeneza Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini Ekaristi Takatifu ni chemchemi na msingi wa Kanisa wa maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Mama wa Kanisa aweze kuwasaidia waamini, kuwa na moyo wa shukrani kwa zawadi kubwa ambayo Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake, yaani Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi.

Papa: Corpus Domini

 

14 June 2020, 14:02