Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani amekazia: Umoja na Unabii katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani amekazia: Umoja na Unabii katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. 

Papa: Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Umoja na Unabii!

Papa Francisko amekazia: mambo makuu mawili: Umoja unaofumbatwa katika upendo na utofauti; katika mateso na ushuhuda wa imani; maana ya Pallio takatifu wanazovishwa Maaskofu wakuu. Pili ni Unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu; unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Juni 2020, akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, walioyamimina maisha yao kama sadaka safi na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika mahubiri yake, amekazia mambo makuu mawili yaani: Mosi, ni Umoja unaofumbatwa katika upendo na utofauti; katika mateso, sala na ushuhuda wa imani; maana ya Pallio takatifu wanazovishwa Maaskofu wakuu. Pili, ni Unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu; unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu amesema, watakatifu Petro na Paulo, walikuwa wamoja, lakini ni watu waliokuwa na taaluma tofauti kabisa. Mtakatifu Petro alikuwa ni mvuvi na muda wake mwingi aliutumia kutengeneza nyavu zake, wakati ambapo Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa alikuwa anafundisha kwenye Masinagogi. Katika maisha na utume wao, Petro aliwaendea Wayahudi, wakati ambapo Paulo, alijielekeza zaidi kwa wapagani na watu wa Mataifa.

Kuna wakati walishindana kule Antiokia kuhusu: ukweli wa Injili na neema ya imani. Mtakatifu Paulo anasema bila kuficha kwamba, walishindana na Kefa uso kwa uso kwa sababu alistahili hukumu! Re. Gal. 2: 11. Hii inaonesha kwamba, hawa ni watu wawili waliokuwa na tofauti zao msingi, lakini walibahatika kuunganishwa na Kristo Yesu kwa njia ya upendo wake na wao wakaendelea kubaki katika tofauti zao msingi, chemchemi ya maisha ya Kanisa la mwanzo. Mkazo ni tofauti katika umoja! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, mateso, dhuluma na mauaji ya Mitume wa Yesu kama ilivyotokea kwa Yakobo ndugu yake Yohane aliyeuwawa kwa upanga wa Herode, Mtakatifu Petro naye alikamatwa na kutupwa gerezani. Haya ni matukio ambayo yalizua hofu na wasi wasi mkubwa miongoni mwa Wakristo, kila mwamini alihofia hatima ya maisha yake. Lakini hata katika dhuluma na mateso yote haya, bado wafuasi wa Kristo Yesu waliendelea kushikamana kwa sala.

Kanisa likaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu kwa juhudi kwa ajili ya Mtakatifu Petro. Huu ni umoja unaofumbatwa katika sala inayomwezesha Roho Mtakatifu kuingilia kati na hatimaye, kuwafungulia malango ya matumaini; kwa kufupisha mwendo sanjari na kuendelea kuwaunganisha katika shida na magumu ya maisha. Mitume wa Yesu waliyapokea madhulumu na nyanyaso kwa imani na matumaini bila hata ya kumlalamikia Mfalme Herode. Kwao malalamiko yangekuwa ni kupoteza muda, bali wakajikita zaidi katika kusali. Hawakutupiana lawama, kusengenyana “wala kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa”. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hiii kuwauliza Wakristo ikiwa kama wanajenga na kudumisha umoja kati yao kwa njia ya sala pamoja na kusindikizana kwa sala? Ni wakati wa kusali zaidi na kupunguza malalamiko, ili kwamba, Mwenyezi Mungu aweze kuwafungulia pingu mbali mbali za maisha zinazoendelea kuwafunga na kuwakandamiza chini.

Wakristo wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili awafundishe kusali vyema zaidi huku wakiombeana. Waamini wanapaswa kusali kwa ajili ya mahitaji yao, lakini pia wasisahau kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wao, kwani hii ni dhamana ambayo Mwenyezi Mungu amewadhaminisha katika maisha na utume wao. Ni mwaliko wa kusali na kuwaombea hata wale ambao wanaonekana kuwa na mawazo tofauti; watu waliowatenda ubaya na wale ambao bado inawawia vigumu kuwasamehe na kusahau. Ni sala peke yake inayoweza kuvunjilia mbali mnyororo wa utengano na hivyo kuanzisha mchakato wa umoja na mshikamano wa upendo. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa: Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Maaskofu wa Majimbo makuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2019-2020. Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya waamini na Mchungaji wao mkuu, kama Kristo Yesu, anapenda kuwabeba mabegani mwake, ili waendelee kuunganika pamoja naye. Hii ni alama ya umoja wa Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kumekuwepo na utamaduni wa ujenzi wa umoja na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox. Makanisa haya mawili yanatambua kwamba, Petro na Andrea walikuwa ni ndugu wamoja. Pale mazingira yanaporuhusu, kumekuwepo na mabadilishano ya wajumbe na wawakilishi wa Makanisa haya mawili katika hali ya udugu wa kibinadamu, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya watakatifu Petro na Andrea. Lengo ni kuwawezesha waamini wa Makanisa haya mawili kutembea kwa pamoja, huku wakiwa wameungana ili hatimaye, siku moja kadiri ya mapenzi ya Mungu waweze kuwa na umoja kamili. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kueleza mambo msingi yanayofumbatwa katika umoja amesema jambo la pili ni Unabii unaosimikwa katika ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu; unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Mitume waliulizwa maswali magumu katika maisha yao na Kristo Yesu, na Mtakatifu Petro akajibu na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai.

Na uamuzi wake wa kumfuasa hakuwa na mashaka hata kidogo, licha ya yale ambayo watu walisema kumhusu Kristo Yesu. Hata wito wa Sauli aliyekuwa anatisha, kwa dhuluma, nyanyaso na mauaji ya wafuasi wa Kristo, alibahatika kukutana na Kristo Mfufuka akiwa njiani kuelekea Dameski na kumwita kwa jina “Sauli, Sauli mbona waniudhi?”. Rej. Mdo. 9:4. Huu ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wa ndani, uliomwezesha Sauli mdhalimu kutoka kwenye udhalimu wake na akawa mtu mwema zaidi. Paulo maana yake ni “mtu mdogo”. Baada ya mtikisiko katika maisha ya Mitume hawa, ukafuatia unabii! “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu”. Rej. Mt. 16:18. Paulo Mtume, akawa ni chombo kiteule cha Kristo Yesu, ili achukue Jina la Yesu mbele ya Mataifa, na Wafalme na Wana wa Israeli. Rej. Mdo 9:15. Unabii anasema Baba Mtakatifu Francisko unapata chimbuko lake, pale mwamini anapojiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kumwachia dhamana ya kuratibisha maisha yake na wala si pale mtu anapodhani kwamba, anaweza kuratibu maisha yake kama anavyotaka!

Jambo la msingi kwa waamini ni kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya kushangazwa na Mungu kama ilivyokuwa kwa Mitume Petro na Paulo, ambao waliwezeshwa kuwa na Unabii kiasi hata cha Mtakatifu Petro kutamka kwamba, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”. Mt. 16:16 na Mtume Paulo anatabiri hatima ya maisha yake anaposema wakati wa kufariki kwangu umefika “baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile”. 2Tim 4:8. Unabii wa kweli ni ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha muujiza wa upendo wa Mungu. Muujiza huu si kielelezo cha nguvu, bali uhalisia wa maisha unaofumbatwa katika sala, huduma na ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hakuna sababu ya kuwa ni matajiri wa kutupwa, bali watu wenye uwezo wa kuwapenda na kuwahudumia maskini; si kwa ajili ya kutaka kujilimbizia mali na utajiri wa ulimwengu huu, bali kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Si kwa ajili ya kumezwa na malimwengu, bali kwa ajili ya furaha katika ulimwengu ujao.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, haitoshi kuwa na sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji, jambo la msingi ni kwa wachungaji kujisadaka na kuonesha upendo mkubwa zaidi kwa Mungu, kiasi hata cha kuthubutu kutundikwa Msalabani, kichwa chini na miguu juu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, Mtume. Kwa upande wake, Paulo Mtume, kabla ya kukatwa kichwa, anasema sasa anamiminwa na wakati wa kufariki kwake umefika. 2Tim 4:6. Huu ni Unabii ambao umeleta mageuzi makubwa katika historia. Mwishoni mwa mahubiri yake Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alimwambia Mtume Petro: “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu”. Rej. Mt. 16:18. Hata kwa Wakristo wa nyakati hizi nao pia wamepewa unabii unaopatikana katika Waraka kwa Kanisa la Pergamo “Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea”. Ufu 2:17.

Kama vile Kristo Yesu alivyoleta mageuzi makubwa kutoka kwa Simone na kwenda kwa Petro, hivi ndivyo ilivyo kwa kila Mkristo kwani anapaswa kugeuka na kuwa ni jiwe hai la ujenzi wa Kanisa na utu wa binadamu uliopyaishwa. Daima kutakuwepo na watu wanaoharibu umoja wa Kanisa na wale wanaotaka pia kuzimisha unabii. Lakini, Kristo Yesu anawaaminia waja wake na anapenda kuwaulizia, ikiwa kama wako tayari kujenga umoja na kuendeleza unabii. Waamini wanapaswa kujiaminisha mikononi mwa Kristo Yesu, ili waweze kuwa na ujasiri wa kusema, “Ndiyo, ninataka”.

Papa: Sherehe: Petro na Paulo Miamba wa Imani

 

29 June 2020, 14:13