Papa Francisko:Maadhimisho ya Corpus Domini tarehe 14 Juni 2020!
Sr. Angela Rwezaula – Vatican
Papa Francisko anatarajia kuongoza ibada ya Misa Takatifu katika fursa ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Mwili na Damu ya Yesu au ‘Corpus Domini” katika Altare ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 14 Juni 2020. Kwa mujibu wa msemaji mkuu wa masuala ya kiliturujia anasema karibia waamini 50 watashiriki katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia saa 3.45 asubuhi majira ya Ulaya na kuhitimishwa kwa ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na mwisho atabariki kwa Ekaristi hiyo. Ni tendo ambalo litarudia kama alivyokuwa akifanya kila siku kwenye Misa za Mtakatifu Marta, zilizokuwa zinatangazwa moja kwa moja tangu tarehe 9 Machi hadi 17 Mei 2020, wakati wa kipindi ambacho nchini Italia na kwingineko hapakuwapo na uwezekano wa kuadhimisha misa na waamini kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Maadhimisho ya Papa Francisko
Mwaka jana Papa Francisko aliadhimisha Siku kuu ya Mwili na Damu ya Yesu katika Uwanja wa Mtakatifu Maria Consolata kwenye mtaa wa Casal Bertone Roma na kunako mwaka 2018 katika Parokia moja ya Mtakatifu Monika huko Ostia, Roma. Tangu 2013 hadi 2017 maadhimisho ya Misa yalikuwa yanafanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Yohane Laterano na baadaye kufuata maandamano ya Ekaristi hadi katika Kanisa Kuu la Maria Mkuu Roma.
Asili ya Siku kuu hii
Mzizi wa Sherehe ya Sikukuu ya Mwili na Damu ya Yesu au Corpus Domini, inaanzia mbali katika karne ya XIII. Kunako mwaka 1215 Mtaguso wa IV wa Laterano ulithibitisha ukweli wa uwepo wa Kristo katika Ekaristi, na baadaye katika Mtaguso wa Trento kunako 1551 ukadhihirisha kabisa kwamba kwa kubariki mkate na divai ubadilishwa kabisa ule mkate kuwa Mwili wa Kristo na divai kuwa kweli Damu yake. Huko Ubelgiji, baada ya kufuatia uzoefu wa ajabu wa Mtakatifu Juliana wa Cornillon, sherehe hii ilianzishwa kunako 1247 katika sikukuu mahalia kwenye mji wa Liègi. Baada ya miaka michache, kunako mwaka 1263, Padre mmoja wa Bohemia ambaye alifika Bolsena akiwa anasumbuliwa na shaka juu ya uwepo halisi wa Yesu, wakati wa kuadhimisha Misa yake na hasa alipofikia wakati wa matoleo ya kumega mkate, aliona matone machache ya damu yakitoka katika Ostia hiyo. Baada ya tukio hilo, Papa Urban IV aliamua kunako mwaka 1264 kulipanua tukio hili la maadhimisho katika Kanisa lote ulimwenguni katika Siku kuu ya Mwili na Damu ya Yesu au ‘Corpus Domini’ katika luhja ya kilatino.