Tafuta

Papa Francisko asema Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni faraja na matumaini kwa watu wanaoteseka. Papa Francisko asema Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni faraja na matumaini kwa watu wanaoteseka. 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Juni 2020: Moyo Mtakatifu wa Yesu

Papa Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Juni 2020, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na Virusi vya Corona, COVID-19. Wale wote wanaoteseka kutokana na COVID-19 watambue kwamba, kuna watu wanaowasindikiza kwa sala na sadaka zao katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Mlimani Calvari, Kristo Yesu alipokuwa ametundikwa Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama na chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na wokovu wa binadamu. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margareta Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Ilikuwa ni tarehe 23 Agosti 1856, Papa Pio IX alipoeneza Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa Kanisa zima. Mtakatifu Faustina Kowalska ni Mtume hodari na maarufu wa huruma ya Mungu katika kipindi cha mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo. Kwa njia ya maisha, utume na maandiko yake, watu wengi wameguswa na kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kiasi cha kujiaminisha katika huruma ya Mungu ambayo imefikia kipeo chake katika maisha na utume wa Kristo Yesu aliyetobolewa ubavu kwa mkuki na humo zikatoka Sakramenti za Kanisa.

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiini cha huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Papa Pio wa XII katika Wosia wake wa Kitume “Haurietis aquas”: Yaani “Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu” uliochapishwa tarehe 15 Mei 1956 anakazia pamoja na mambo mengine: Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni zawadi ya mto wa rehema unaozima kiu ya upendo na maisha ya uzima wa milele na utakatifu. Hii ni Ibada inayopaswa kudumishwa kwa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kanisa, Kanuni maadili na utu wema. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu ni: Njia, Ukweli na Uzima. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, iwe ni chemchemi ya upendo kwa jirani, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya wokovu wa binadamu. Upendo huu kwa namna ya pekee kabisa unafumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wajenge pia Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria. Lengo ni kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Huu Ufalme wa haki na uzima, utakatitifu na neema, ufalme wa mapendo na amani.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Juni 2020, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote wanaoteseka kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 watambue kwamba, kuna watu wanaowasindikiza kwa sala na sadaka zao katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mahali ambapo kuna: mateso, mahangaiko na magonjwa, Kristo Yesu, yupo mahali hapa.

Na wala hakuna sababu ya mtu kujisikia pweke, kwa sababu, Kristo Yesu anataka kuwatuliza na kuwafariji waja wake kwa neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, chemchemi ya huruma, upendo na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wasisite kukimbilia hifadhi na tunza kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha wokovu wa binadamu. Kwa njia ya maneno na mtindo wake wa maisha, Kristo Yesu anaweza kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa huruma na mapendo, sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuonja na hatimaye, kumwilisha ndani mwao maendeleo mpinduka, ili kuambata na kukumbatia huruma na upendo wa Mungu. Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, Shirika la Wayesuit lilipewa dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kunako mwaka 1883. Lengo ni kuendeleza huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, Mwinjili Yohane ni kati ya wafuasi wa Yesu waliopendwa zaidi. Akabahatika kuwa ni Mtume wa kwanza kumtambua Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, inawasaidia waamini kuonja furaha ya Kristo Mfufuka, aliyeteswa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu na kwamba, bado yupo hai kati ya waja wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, iwasaidie watu kujenga moyo wa huruma, upendo na msamaha kwa jirani zao.Itakumbukwa kwamba, Utume wa Sala Kimataifa unakijumuisha pia Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi Takatifu, EYM. Utume wa Sala Kimataifa ulianzishwa kunako tarehe 3 Desemba 1844 huko Paris, Ufaransa na Padre Francesco Saverio Gaufrelet, SJ.

Papa: Nia Juni 2020
16 June 2020, 14:01