Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kuongezwa kwa vifungu vitatu kwenye Litania ya Bikira Maria: Mama wa Huruma; Mama wa Matumaini na Mfariji wa Wakimbizi au "Msaada wa Wakimbizi. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kuongezwa kwa vifungu vitatu kwenye Litania ya Bikira Maria: Mama wa Huruma; Mama wa Matumaini na Mfariji wa Wakimbizi au "Msaada wa Wakimbizi.  (AFP or licensors)

Litania ya Bikira Maria: Nyongeza: Huruma! Matumaini na Faraja!

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, katika Litania ya Bikira Maria wa Loreto inayojulikana na kupendwa na wengi, viongezwe vifungu vitatu. Yaani: “Mater Misericordiæ”, yaani “Mama wa huruma; “Mater Spei”, yaani “Mama wa Matumaini na hatimaye “Solacium Migrantium” yaani “Mfariji wa wakimbizi” sehemu hii inaweza pia kutafsiriwa kuwa ni “Msaada wa Wakimbizi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Safi wa Bikira Maria, tarehe 20 Juni 2020, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, katika Litania ya Bikira Maria wa Loreto inayojulikana na kupendwa na wengi, viongezwe vifungu vitatu. Yaani: “Mater Misericordiæ”, yaani “Mama wa huruma; “Mater Spei”, yaani “Mama wa Matumaini na hatimaye “Solacium Migrantium” yaani “Mfariji wa wakimbizi” sehemu hii inaweza pia kutafsiriwa kuwa ni “Msaada wa Wakimbizi”. Uamuzi huu wa Baba Mtakatifu umetolewa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa chini ya uongozi wa Kardinali Robert Sarah pamoja na Askofu mkuu Arthur Roche, viongozi wakuu wa Baraza hili katika barua waliyowaandikia Marais wote wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza anasema, sala inabubujika kutoka katika matatizo na changamoto za maisha ya waamini. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho1975, kuliadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Litania ya Bikira Maria wa Loreto ikaongeza heshima hii katika Litania. Kwa sababu, Bikira Maria, Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Wakristo wote. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Ndio maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wot wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Familia Takatifu, Mtakatifu Yohane Paulo II aliongeza kwenye Litani ya Bikira Maria, “Mama wa familia”. Itakumbukwa kwamba, Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Baba Mtakatifu Francisko ametunga sala ifuato: “Tunakimbilia ulinzi wako, Mama Mtakatifu wa Mungu, katika hali tete na majonzi ambayo yameugubika ulimwengu mzima, tunakimbilia kwako Mama wa Mungu na Mama yetu, tunatafuta usalama chini ya ulinzi wako. Ee Bikira Maria, utuangalie kwa macho yako yenye huruma katika Janga hili la Virusi vya Corona, na uwafariji wale wanaohuzunika na kuomboleza kutokana na vifo vya ndugu zao; waliozikwa hata wakati mwingine katika mazingira yanayo uchoma moyo. Wahurumie wale wote wanaoteseka kwa ajili ya wagonjwa, ili kuzuia maambukizi hawawezi kuwa nao karibu. Wajalie imani watu wenye hofu kwa kutokuwa na uhakika wa maisha yao kwa siku za mbeleni kutokana na athari za kiuchumi na kazi. Mama wa Mungu na Mama Yetu, tuombee kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa huruma, ili kwamba, majaribu haya mazito yaweze kufikia ukomo na kuanza kurejea tena upeo wa matumaini na imani. Kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya, ingilia kati na uwaombee mbele ya Mwana wa Mungu, ili aweze kuzifariji familia zenye wagonjwa na waathirika; afungue nyoyo zao ili ziweze kuwa na imani.

Walinde madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea ambao katika Janga hili wamekuwa mstari wa mbele, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao, ili kuokoa maisha ya wengine. Wasindikize katika mahangaiko yao ya kishupavu; wajalie nguvu, wema na afya. Uwe pembeni mwa wale wote ambao usiku na mchana wanawasaidia wagonjwa, na mapadre wakisukumwa na ari ya kichungaji na utume wa Kiinjili, wanajitahidi kuwasaidia na kuwahudumia wote. Bikira Maria angaza akili za wanasayansi, ili waweze kupata suluhu ili kushinda Virusi hivi. Wasaidie Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, ili waweze kutenda kwa hekima, huruma na ukarimu, kwa kuwasaidia wale wote wanaokosa mahitaji msingi ya maisha; kwa kuandaa programu zitakazotoa suluhu za kijamii na kiuchumi kwa kuwa na malengo ya muda mrefu wakiwa na moyo wa mshikamano.

Bikira Maria Mtakatifu, gusa dhamiri za watu ili kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kutengeneza na kuboresha silaha za maangamizi, badala yake, fedha hii, itumike katika tafiti muhimu ili kuzuia majanga kama haya kwa siku za usoni. Bikira Maria Mama mpendelevu, saidia kukuza ulimwenguni utambuzi kwamba, watu wote wanaunda familia kubwa ya binadamu; ili kwamba, wote wakiwa wameunganishwa na mshikamano na udugu waweze kusaidia kupambana na umaskini na hali mbaya ya maisha ya mwanadamu. Waimarishe waamini katika imani, daima wakidumu katika sala na huduma. Bikira Maria Faraja ya wanaoteseka, wakumbatie wanao wote wanaoteseka, waombee kwa Mwenyezi Mungu ili kwa mkono wake wenye nguvu aweze kuwaokoa watu wake kutoka katika Janga hili, ili hatimaye, maisha yaweze kuanza tena katika hali ya kawaida na utulivu. Tunakutumainia, ili katika safari yetu uwe ni alama ya wokovu na matumaini, Ee mpole, Ee mwema Ee mpendevu, Bikira Maria. Amina.

ITANIA YA BIKIRA MARIA

Baba wa mbinguni Mungu                                                               Utuhurumie.

 Mwana, Mkombozi wa dunia, Mungu,                                            Utuhurumie.

 Roho Mtakatifu, Mungu,                                                                  Utuhurumie.

 Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja,                                                    Utuhurumie.

Maria Mtakatifu,                                                                                Utuombee.

 Mzazi Mtakatifu wa Mungu,                                                           Utuombee.

 Bikira Mtakatifu, mkuu wa mabikira,                                             Utuombee.

 Mama wa Kristo,                                                                              Utuombee.

 Mama wa neema ya Mungu,                                                          Utuombee.

 Mama wa matumaini                                                                    Utuombee.

 Mama wa Kanisa utuombee                                                           Utuombee.

 Mama wa huruma                                                                             Utuombee

 Mama mtakatifu sana,                                                                    Utuombee.

 Mama mwenye moyo safi,                                                              Utuombee.

 Mama mwenye ubikira,                                                                  Utuombee.

 Mama usiye na dhambi                                                                  Utuombee.

 Mama mpendelevu,                                                                        Utuombee.

 Mama mstaajabivu,                                                                        Utuombee.

 Mama wa shauri jema,                                                                   Utuombee.

 Mama wa Mwumba,                                                                      Utuombee.

 Mama wa Mkombozi,                                                                    Utuombee.

 Bikira mwenye utaratibu,                                                                Utuombee.

 Bikira mwenye heshima,                                                                Utuombee.

 Bikira mwenye sifa,                                                                       Utuombee.

 Bikira mwenye huruma,                                                                  Utuombee.

 Bikira mwaminifu,                                                                         Utuombee.

 Kioo cha haki,                                                                               Utuombee.

 Kikao cha hekima,                                                                         Utuombee.

 Sababu ya furaha yetu,                                                                   Utuombee.

 Chombo cha neema,                                                                       Utuombee.

 Chombo cha heshima,                                                                    Utuombee.

 Chombo bora cha ibada,                                                                  Utuombee.

 Waridi lenye fumbo,                                                                      Utuombee.

 Mnara wa Daudi,                                                                           Utuombee.

 Mnara wa pembe,                                                                           Utuombee.

 Nyumba ya dhahabu,                                                                     Utuombee.

 Sanduku la Agano,                                                                         Utuombee.

 Mlango wa mbingu,                                                                        Utuombee.

 Nyota ya asubuhi,                                                                           Utuombee.

 Afya ya wagonjwa,                                                                        Utuombee.

 Kimbilio la wakosefu,                                                                    Utuombee.

 Mfariji wa wakimbizi                                                                    Utuombee.

 Mfariji wa wenye uchungu,                                                            Utuombee.

 Msaada wa Wakristo,                                                                     Utuombee.

 Malkia wa Malaika,                                                                       Utuombee.

 Malkia wa Mababu,                                                                       Utuombee.

 Malkia wa Manabii,                                                                        Utuombee.

 Malkia wa Mitume,                                                                        Utuombee.

 Malkia wa Mashahidi,                                                                    Utuombee.

 Malkia wa Waungama,                                                                   Utuombee.

 Malkia wa Mabikira,                                                                      Utuombee.

 Malkia wa Watakatifu wote,                                                           Utuombee.

 Malkia uliyeumbwa pasipo dhambi ya asili,                                    Utuombee.

 Malkia uliyepalizwa mbinguni,                                                      Utuombee.

 Malkia wa Rozari takatifu,                                                              Utuombee.

 Malkia wa amani,                                                                            Utuombee.

 Malkia wa familia,                                                                         Utuombee.

 

Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, UtusameheEe Bwana.

Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, Utusikilize Ee Bwana.

Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, Utuhurumie Ee Bwana.

Litania ya Bikira Maria 2020

 

22 June 2020, 13:55