Papa Francisko katika barua yake binafsi amechapisha sheria, kanuni na taratibu mpya kuhusu: ukweli, udhibiti na mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa mikataba ya manunuzi Vatican. Papa Francisko katika barua yake binafsi amechapisha sheria, kanuni na taratibu mpya kuhusu: ukweli, udhibiti na mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa mikataba ya manunuzi Vatican. 

Papa Francisko: Mapambano dhidi ya Rushwa: Ukweli na Uwazi

Barua Binafsi, “Motu proprio” amechapisha sheria, kanuni na taratibu mpya kuhusu: Ukweli, Udhibiti na Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa Mikataba inayotekelezwa na Vatican katika ujumla wake. Sheria zinapania kudhibiti hatari rushwa. Sheria hizi zimegawanyika katika Ibara 86 na nyongeza ya vifungu 12 mintarafu ulinzi wa kisheria pale kunapotokea upinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mfumo wa Barua Binafsi, “Motu proprio” amechapisha sheria, kanuni na taratibu mpya kuhusu: Ukweli, Udhibiti na Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa Mikataba inayotekelezwa na Vatican katika ujumla wake. Sheria hizi mpya zinapania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, zinadhibiti hatari ya saratani ya rushwa. Sheria hizi zimegawanyika katika Ibara 86 na nyongeza ya vifungu 12 mintarafu ulinzi wa kisheria pale kunapotokea upinzani. kwa Barua Binafsi ya Baba Mtakatifu inayopitisha Sheria hizi mpya ni chombo madhubuti kilichofanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, kinachotoa sheria na kanuni za kupambana na saratani ya rushwa.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanazingatia sheria, kanuni na taratibu hizi mpya, ili kuboresha mchakato wa utekelezaji wa dhamana na shughuli mbali mbali zinazofanywa na Vatican. Lengo ni kutaka kudumisha ukweli, uwazi na udhibiti wa mikataba inayotekelezwa na Vatican katika ujumla wake. Kwa wafanyakazi wanaosambaza bidhaa, huduma; wafanyakazi pamoja na shughuli mbali mbali zitahakikishiwa kwamba, kunakuwepo na usawa na uwezekano wa kushiriki kikamilifu katika shughuli hizi kwa kutumia matangazo maalum. Hatima ya sheria, kanuni na taratibu hizi ni kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha ya ndani, inatumika kwa ajili ya maendeleo fungamani; kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi katika mchakato wa maamuzi pamoja kwa kuwashughulikia wahusika wote wanaotaka kufanya tenda katika misingi ya haki na usawa pasi na upendeleo.

Kwa njia hii, kwa kiwango kikubwa, saratani ya rushwa inaweza kudhibitiwa. Lengo la Vatican ni kuhakikisha kuwa kunakuwepo na programu pamoja na mchakato bora zaidi wa manunuzi; kwa kuondokana na utendaji wa shughuli ambazo si muhimu sana; kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, ukweli, uwazi, haki bila upendeleo vinashamiri na kudumishwa. Vatican pia imeweka sera na mikakati ili kuepusha mgongano wa kimasilahi, mikataba haramu katika zabuni pamoja na kupambana na saratani ya rushwa. Bila kuathiri baadhi ya mambo ambayo yanatajwa kuwa “si ya kawaida”, kimsingi shughuli zote za manunuzi na huduma zinatolewa moja kwa moja na Utawala wa Hazina ya Vatican, APSA pamoja na Serikali ya mji wa Vatican. Hatimaye, kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican, kutawekwa orodha ya wafanyakazi na taaluma zao, ambao wamekabidhiwa kwa muda dhamana ya kupanga sera pamoja na majina ya wajumbe walioko kwenye jopo la maamuzi. Hawa watachaguliwa na kushiriki kwa njia ya mzunguko kwenye Tume mbali mbali mintarafu weledi na taaluma zao!

Barua Binafsi
01 June 2020, 14:09