Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maskini ni amana, utajiri na sehemu ya maisha na utume wa Kanisa Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maskini ni amana, utajiri na sehemu ya maisha na utume wa Kanisa 

Papa Francisko: Maskini ni Amana, Utajiri na Utume wa Kanisa

Wawakilishi wa Chama cha Lazare, hivi karibuni walikutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu alikazia:: utu, heshima na haki msingi za binadamu; toba, wongofu na msamaha; maskini kama amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Chama cha Lazare, kinaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linajengwa na waamini wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu muhimu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili. Adui mkubwa wa Kanisa ni pale uchu wa mali na madaraka vinapoingia kwa kupitia mlango wa nyuma. Maskini ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa, hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Matendo ya huruma ndicho kigezo kikuu ambacho Kristo Yesu atakitumia Siku ya Hukumu ya Mwisho. Waamini wawe makini dhidi ya uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yanaweza kuhatarisha hata maisha yao ya kiroho na kujikuta wametumbukia katika kiburi, ubinafsi na hatimaye kumezwa na malimwengu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya kiroho! Hakuna kulala hadi kieleweke! Bwana Étienne Villemain ni mwamini mlei na baba wa familia ambaye tangu mwaka 2005 amekuwa akiishi na maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum nyumbani mwake. Ni mwanzilishi wa Chama cha Lazare kinachowahudumia maskini na watu wasiokuwa na makazi katika nyumba zake 18 wanamoishi watu zaidi ya 300.

Mwamini mlei huyu pia ndiye muasisi wa wazo la Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kama matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Wawakilishi wa Chama cha Lazare, hivi karibuni walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu alikazia kwa namna ya pekee: utu, heshima na haki msingi za binadamu; toba, wongofu wa ndani na msamaha; maskini kama amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu alitamani kukutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Lazare, kilichoanzishwa rasmi kunako mwaka 2011 na sasa kinaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chama ambacho kimeendelea kujipambanua kwa sadaka na majitoleo yake kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kutokana na kuzingatia itifaki ya kudhibiti maambuzi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, sehemu kubwa ya wanachama wake, wameshiriki tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kiasi hata cha kumuuliza Baba Mtakatifu maswali.

Baba Mtakatifu anasema, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kuendelezwa na wote. Haya ni mambo ambayo hayajalishi hata kidogo kuhusu: tabaka la mtu, hali ya afya yake na nafasi katika jamii. Utu wa mtu ni sharti muhimu la kuweza kuishi vyema ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anasema, toba, wongofu wa ndani na msamaha ni mambo muhimu sana katika maisha ya waamini. Watu wajifunze kutoa na kupokea msamaha na kwamba, hii ni hija ya maisha inayopaswa kutekelezwa kila kukicha kwa njia ya unyenyekevu, hadi kuhakikisha kwamba, moyo uliokuwa umevunjika na kupondeka umetibiwa na kupona kabisa! Huu ni mwaliko kwa waamini kuachana na kiburi cha kutaka kulipiza kisasi na mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha Injili. Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa kamwe haliwezi kupanuka na kuongezeka kwa njia ya wongofu wa shuruti! Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni mbolea tosha kabisa ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, kwa bahati mbaya sana kuna watu ambao wameelemewa na uchu wa fedha na mali, kiasi cha kumezwa na malimwengu, hali inayowafanya kumweka Mwenyezi Mungu kando ya maisha na vipaumbele vyao. Lakini pia, kuna watu wenye utajiri wa fedha na mali, wanaotumia neema na baraka hizi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Kwa maneno machache ni watu wanaotumia utajiri huku wakiongozwa na tunu msingi za Kiinjili. Utajiri wa wakleri na watawa unaweza kuonekana kuwa ni kashfa kwa watu wa Mungu. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni mseja, fukara na mtii. Ufukara ni nguzo ya maisha bora kwani hii ni chemchemi ya wema, ukarimu, sadaka na majitoleo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anasema, inawezekana kabisa kufungua nyumba ya maskini mjini Vatican, lakini kinachokosekana ni ujasiri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kutekeleza wazo na dhamana hii.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana jinsi ambavyo wanajitahidi kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa jirani zao kutokana na karama na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mmoja wao! Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Misericordia et misera” “Huruma na haki” ni mwaliko wa kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii kwa njia ya umoja na mshikamano wa upendo. Kanisa linapenda kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini ndiyo maana kila mwaka Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa itaadhimishwa Siku ya Maskini Duniani ili kutoa nafasi kwa Kanisa kutafakari kuhusu maskini ambao kimsingi ni amana, hazina na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kujenga misingi ya haki jamii kwani hakuna haki na amani ya kweli, ikiwa kama bado kuna makundi makubwa ya maskini wanaoteseka kwa baa la njaa, magonjwa, umaskini, ujinga, utupu na upweke katika maisha.

Huruma ni kielelezo makini cha imani na ushuhuda wa Kikristo. Huu ni mwaliko wa kutafakari dhana ya umaskini duniani kwa kutumia miwani ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia kadiri ya uwezo na fursa zilizopo.Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini, ndiyo maana baada ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya upendo wa Kristo kwa maskini na wahitaji zaidi. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha upendeleo wa Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasikiliza, kuwahudumia na hatimaye, kuwaonesha maskini upendo na mshikamano, kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa na wanapendwa na Baba wa mbinguni.

Siku ya Maskini Duniani, iwe ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Maadhimisho haya yakamilishwe kwa namna ya pekee Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Ufalme wa Kristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, ushuhuda wa utimilifu wa upendo wa Mungu, chemchemi ya maisha mapya wakati wa Pasaka. Siku ya Maskini Duniani iwe ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni, hali inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo. Watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, daima wakiwa tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu.

Iwe ni Siku ya kumwilisha Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, ambayo kimsingi ni sala ya maskini, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaohitaji mambo msingi katika maisha. Sala ya Baba Yetu inawawajibisha waamini kupokea na kugawana hata kile kidogo kilichopo, tayari kuvunjilia mbali ubinafsi, kwa kutoa nafasi ya kushirikisha furaha ya ukarimu. Siku ya Maskini Duniani iwe ni fursa makini ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; nafasi ya kutambua kwamba, maskini wanawasaidia waamini wenzao kutambua ukweli na tunu msingi za Kiinjili.

Papa: Maskini
09 June 2020, 14:01