Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi kuendelea kujizatiti kudumisha ari na moyo wa sala kwa ajili ya amani duniani! Tarehe 8 Juni 2020 ni Siku ya Kuombea Amani. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi kuendelea kujizatiti kudumisha ari na moyo wa sala kwa ajili ya amani duniani! Tarehe 8 Juni 2020 ni Siku ya Kuombea Amani. 

Siku ya Kuombea Amani Duniani 8 Juni 2020: Umuhimu wa Sala!

Tarehe 8 Juni 2020 iwe ni Siku ya Kuombea Amani Duniani, kila mtu kadiri ya imani na Mapokeo ya dini yake. Wananchi peke yao, bila ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kamwe hawawezi kufua dafu kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani. Amani na utulivu wa ndani ni tunu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuombea amani katika Nchi Takatifu. Bado anakumbuka lile tukio la tarehe 8 Juni 2014 alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Hayati Rais Shimon Peres wa Israeli pamoja na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati! Baba Mtakatifu anasema baadhi ya watu wanaweza kufikiri kwamba, mkutano ule wa sala haukuwa na mafanikio yoyote, lakini hii si kweli, kwani Sala inawasaidia waamini kutokatishwa tamaa na hivyo kushindwa na ubaya, wala matumizi ya nguvu kushika hatamu; badala ya majadiliano na upatanisho. Baba Mtakatifu anawaalika wadau mbali mbali kuongeza juhudi zao katika kukomesha uadui na chuki kati ya watu, ili amani, ustawi na mafao ya wengi yaweze kushika mkondo wake.Ni kutokana na muktadha huu, Jukwaa la Umoja wa Vijana Wakatoliki Kimataifa, FIAC, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana ili kuombea amani duniani.

Maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 yamesababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani kiasi hata cha kugumisha mahusiano na mafungamano kati ya mtu na mtu na kati ya Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na kinzani pamoja na mipasuko ya hapa na pele, inayoweza kusababisha amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mataifa vikatoweka na kupotea. Tarehe 8 Juni 2020 iwe ni Siku ya Kuombea Amani Duniani, kila mtu kadiri ya imani na Mapokeo ya dini yake. Wananchi peke yao, bila ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kamwe hawawezi kufua dafu kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani. Amani na utulivu wa ndani ni tunu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Amani haina budi kupata chanzo chake kutoka katika undani wa mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu iliyoadhimishwa hapo tarehe Mosi Januari, 2020 yaliongozwa na kauli mbiu: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anapembua kwa kina na mapana dhana ya amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti pamoja na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbukumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu!  Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali kutumia hati hii kwa ajili ya tafiti na tafakari ya kina, ili kuunda familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kuheshimu na kuthamini tofauti zao msingi, amana na utajiri kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Siku ya Kuombea Amani 8 Juni 2020
08 June 2020, 13:59