Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: fumbo la Sala: Sala ya Musa Mtumishi wa Mungu: Mapambano katika maisha ya sala! Papa Francisko: fumbo la Sala: Sala ya Musa Mtumishi wa Mungu: Mapambano katika maisha ya sala!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Fumbo la Sala: Sala ya Musa Mtumishi wa Mungu

Baba Mtakatifu katika tafakari hii amegusia kuhusu: Matatizo na changamoto ambazo Musa Mtumishi wa Mungu alikumbana nazo katika maisha na utume wake; jinsi Musa alivyokuwa anasali; mahusiano na mafungamano yake na watu wa Mungu, Musa na Sala ya Mshenga kama daraja linalowaunganisha Waisraeli na Mwenyezi Mungu. Musa alionekana kuwa ni kiongozi aliyeshindwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Juni 2020 ameendeleza mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Amekwisha kufafanua kuhusu mateso na sala ya mwadilifu, Sala Abramu na Sala ya Yakobo aliyepambana na Mwenyezi Mungu hadi kikaeleweka. Sala ya Musa Mtumishi wa Mungu imeongozwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka sura 32:11-14- Hii ni Sala inayomwonesha Musa akiomba huruma ya Mungu kutokana na uasi wa Waisraeli, akamkumbusha Mwenyezi Mungu Agano lake na Mababa wa Imani na hatimaye, Mwenyezi Mungu akaughairi ule uovu aliosema ya kwanza atawatenda watu wake.

Baba Mtakatifu katika tafakari hii amegusia kuhusu matatizo na changamoto ambazo Musa Mtumishi wa Mungu alikumbana nazo katika maisha na utume wake; jinsi Musa alivyokuwa anasali; mahusiano na mafungamano yake na watu wa Mungu, Musa na Sala ya Mshenga kama daraja linalowaunganisha Waisraeli na Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wa kibinadamu, tangu mwanzo, Musa alionekana kuwa ni kiongozi aliyeshindwa na Kitabu cha Kutoka kinamwonesha kama mkimbizi hata kama alijipambanua kuwa ni mtetezi wa wale waliokuwa wanadhulumiwa na akawa ni sababu ya chuki na uhasama kati ya watu, kiasi kwamba, ile ndoto yake ya utukufu ikapotea kama umande wa asubuhi. Musa Mtumishi wa Mungu hakuonekana kupata mafanikio katika shughuli zake, lakini daima alipenda kutumia kila fursa kwa ajili ya kuboresha hali na mahusiano yake na Mwenyezi Mungu.

Musa Mtumishi wa Mungu akiwa katikati ya jangwa kubwa na lenye kutisha kutokana na kimya kikuu, wakati alipokuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani mkuu wa Midian, Mwenyezi Mungu akamtokea katika kijiti kilichokuwa kinawaka moto na hapo Mwenyezi Mungu akamfunulia uwepo wake kwamba, Yeye ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na ya Yakobo. Hapa Musa Mtumishi wa Mungu akagundua ni kwa sababu gani alificha uso wake, kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Mwenyezi Mungu anamwita na kumtaka Musa ajifunge kibwebwe, ili aweze kuwaongoza watu wa Mungu kutoka utumwani Misri. Musa akaweka pingamizi mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba hakuwa na sifa hata kidogo kuweza kuwaongoza wana wa Israeli!

Ni kwa nini umenichagua na kunituma mimi? Hii itakuwa ni sala ya Musa katika maisha yake yote mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kushindwa kuingia kwenye Nchi ya Ahadi. Sala ya Musa ni kielelezo tosha kwa kila mwamini anayeona na kuonja ugumu wa kusali mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika shida, hofu na wasi wasi mkuu wakati mwingine inakuwa si rahisi sana kuweza kusali. Lakini ni katika unyonge huu wa Musa, anaonesha ile nguvu ya kuweza kusali. Akakabidhiwa na Mungu mbao za Amri zake kwa ajili ya watu wake. Akawa muasisi wa Ibada Takatifu; Daraja na kiungo muhimu cha Mafumbo ya Mungu pamoja na kuendelea kuwa na mahusiano na mafungamano ya karibu na watu wa Mungu hasa wakati wa majaribu na dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.

Musa Mtumishi wa Mungu alikuwa na mizizi na kumbukumbu endelevu ya watu wake, kielelezo cha Mchungaji mkuu, kiasi hata cha kujenga urafiki na Mwenyezi Mungu hata kuweza kuzungumza naye uso kwa uso! Musa Mtumishi wa Mungu aliendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu na watu wake, ili aweze kuwaombea huruma na msamaha wakati wa vishawishi na hatimaye, kuanguka dhambini. Waisraeli waliyakumbuka “makapu ya nyama na vitunguu swaumu” wakasahau kwamba, huko walikuwa utumwani Misri. Musa akaendelea kushikamana na Mwenyezi Mungu pamoja na watu wake. Akawa msemaji mkuu wa watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Akaonesha unyenyekevu wa hali ya juu, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kuwa kweli ni mtu wa watu!

Katika muktadha huu Baba Mtakatifu Francisko anasema, sala ya Musa inakuwa ni mfano wa kustaajabisha wa sala na maombezi itatimilizwa katika mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu, yaani Kristo Yesu. Rej. KKK. 2574. Musa anaitwa na kutumwa, huku akiendelea kumhusianisha na huruma wenye upendo na kwa kazi yake ya wokovu. Musa anaendelea kuwa ni daraja na kiungo kati ya mbingu na dunia, hadi siku ile Wana wa Israeli walipomkana Mungu na kujitengenezea ndama ya dhahabu. Akatambua dhambi hii kubwa, lakini, bado akaendelea kufungamana na Mungu pamoja na watu wake. Anaendelea kuwa ni mshenga na mwombezi wa watu wake. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, viongozi wa Kanisa ni madaraja kati ya Mungu na waja wake. Wao ni waombezi wa huruma ya Mungu. Hiki ni kielelezo cha sala ya watakatifu wengi ndani ya Kanisa.

Kutoka urafiki huo na Mwenyezi Mungu mwaminifu, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa huruma, Musa akachota nguvu na ushupavu kwa ajili ya maombi yake. Akasali na kuliombea taifa ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amejipatia. Akasali kwa bidii zaidi, wana wa Israeli walipomwasi Mungu, akasimama mbele ya Mungu na kuwakoa watu wake. Mapambano katika sala ni kielelezo cha maisha yake. Mungu ni upendo na mwenye haki na daima ataendelea kubaki kuwa mwaminifu. Kristo Yesu ni daraja kati ya Mungu na binadamu, anaendelea kusali na kuwaombea waja wake mbele ya Baba yake wa mbinguni. Hii ni changamoto ya kuendelea kusali kwa ari, moyo, ibada na uchaji wa Mungu kama alivyofanya Kristo Yesu. Watu wote ni wa Mungu, wawe wadhambi au watakatifu. Watu wa Mungu wajifunze kusali vyema zaidi, kwa kuwaombea watu badala ya kuwalaani! Rej. KKK. 2577.

Papa: Sala ya Musa
17 June 2020, 14:28