Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Sala ya Abramu, Baba wa Imani na Matumaini thabiti! Baba Mtakatifu Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Sala ya Abramu, Baba wa Imani na Matumaini thabiti! 

Papa Francisko: Fumbo la Sala: Sala ya Abramu Baba wa Imani

Sala ya Abramu inasimikwa katika: Ukimya na uaminifu kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kusali kwa imani, kumsikiliza Mungu na kutembea katika njia zake, huku wakithubutu kuzungumza na Mungu katika maisha! Mwenyezi Mungu alimwita Abramu kutoka katika nchi yake, jamaa zake na kutoka katika nyumba ya baba yake na kwenda katika nchi ambayo atamwonesha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Juni 2020 ameendeleza mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Amekwisha kufafanua kuhusu mateso na sala ya mwadilifu. Tafakari ya Sala ya Abramu imeongozwa na maneno kutoka katika Kitabu cha Mwanzo sura ya 15: 1.3-6. Neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, “Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski. Nalo Neno la Bwana likamjia likinena…Tazama sasa mbingu, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu na akaongeza kusema… Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.

Baba Mtakatifu anasema Abramu alikuwa ni msikivu wa Neno la Bwana, aliyejitahidi kutembea katika njia ya Bwana na imani yake ikatengeneza historia inayomwilishwa katika maisha ya watu wake. Sala ya Abramu inasimikwa katika ukimya na uaminifu kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kusali kwa imani, kumsikiliza Mwenyezi Mungu na kutembea katika njia zake, huku wakithubutu kuzungumza na Mungu katika maisha! Mwenyezi Mungu alimwita Abramu kutoka katika nchi yake, jamaa zake na kutoka katika nyumba ya baba yake na kwenda katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu atamwonesha. Yote haya ni mambo ambayo yalikuwa yamesimikwa katika ahadi, iliyohitaji ujasiri na Abramu akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Maandiko Matakatifu hayazami sana katika historia ya Abramu kwa siku za nyuma, bali yanakazia kuhusu uzao wake utakavyokuwa kama nyota za angani. Abramu akasikiliza Neno la Bwana na kuliamini na huo ukawa mwanzo wa kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, Abramu anayo nafasi ya pekee kabisa kama Baba wa imani kwa Wayahudi, Wakristo na Waislam. Anayesabiwa kuwa ni mtu mwaminifu na mwenye haki aliyejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye wakati mwingine, ahadi zake zilikuwa kana kwamba, hazieleweki. Abramu alikuwa ni mtu wa neno aliyejitahidi kumwilisha neno lake katika uhalisia wa maisha. Haya ni mabadiliko makubwa katika safari ya maisha ya mwamini katika sala. Maisha hayana budi kufahamika kama wito na mahali ambapo Mwenyezi Mungu anatekelezea ahadi zake. Mwenyezi Mungu anatembea na waja wake, huku akitekeleza ahadi zake. Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, akatoka akaenda mahali pale atakapopapata kuwa urithi, akatoka asijue aendako. Rej. Ebr. 11.8.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kadiri ya Kitabu cha Kutoka, Abramu aliendelea kuwa ni mtu wa sala na mwaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye mara kwa mara alimtembelea katika hija ya maisha yake na kumwanzishia historia. Kwa hakika imani inaunda historia kwa njia ya mfano wa maisha yake, anawafundisha waamini jinsi ambavyo imani inaunda historia na Mwenyezi Mungu anakuwa karibu na waja wake kiasi cha kujisikia kuwa ni Mungu wake; Mungu anatengeneza historia ya mtu binafsi na kuongoza hatua mbali mbali za maisha na kamwe hawezi kumwacha mja wake. Hapa kila mwamini anapaswa kujiuliza kutoka katika undani wake, ikiwa kama anayo mang’amuzi kama haya katika maisha yake. Huu ni ushuhuda unaomwonesha Mungu kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.  

Baba Mtakatifu anaongeza kusema, huyu si Mungu wa wanafalasafa na wenyehekima. Huyu ni Mungu anayewahikikishia waja wake uwepo wake wa daima, chemchemi ya furaha na matumaini. Sala ya Ibrahamu inadhihirishwa kwanza kwa matendo: mtu mkimiya, kwa kila hatua anamjengea Bwana Altare, ili kukumbuka mapito ya maisha yake. Anaona majaribu ya imani katika uaminifu wa Mungu. Akawa tayari kumpokea mgeni wa ajabu hemani mwake. Anapokea kwa mshangao mkubwa habari za kuzaliwa kwa mtoto wake Isaka. Hata katika uzee wao, wakajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na Sara akapata mimba hata katika uzee wake. Huyu ndiye Mungu wa Ibrahimu anayewasindikiza waja wake. Ibrahimu akajenga mazoea na Mwenyezi Mungu kiasi hata cha kuthubutu “kulumbana” naye katika uaminifu. Akawa tayari kumtoa mtoto wake sadaka ya kuteketea, kielelezo cha imani hai, inayomwezesha hata kutembea katika giza totoro! Hii ni kutokana na imani thabiti kiasi hata cha kuthubutu kupambana na Mwenyezi Mungu. Rej. Mwa. 22:1-19.

Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka Ibrahimu, Baba wa imani jinsi ya kusali kwa imani thabiti; kumsikiliza Mwenyezi Mungu; kutembea, kuzungumza na hata kulumbana na Mungu katika maisha bila woga wala makunyanzi. Watu wanaweza hata kukasirikiana na Mwenyezi Mungu kwani hata huu ni mtindo wa sala unaopaswa kupokelewa na kumwilishwa katika matendo. Waamini wajifunze kuzungumza na Mwenyezi Mungu kama watoto wanavyozungumza na wazazi wao; wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kujibu kwa vitendo na kujadiliana naye kwa kina na mapana, daima wakijitahidi kuwa wazi na waaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Papa: Sala ya Abramu

 

 

03 June 2020, 14:28