Tafuta

Vatican News
Kanisa linasherehekea Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Anthony wa Padua alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Wokovu! Kanisa linasherehekea Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Anthony wa Padua alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Wokovu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Ujumbe Kwa Wafuasi wa Mt. Anthony wa Padua!

Papa Francisko ana tumaini kwamba, Jubilei ya Miaka 800 ya wito na maisha ya Mtakatifu Anthony wa Padua, itasaidia kupyaisha utakatifu wa maisha miongoni mwa Wafranciskani pamoja na wafuasi wa Mtakatifu Anthony wa Padua. Waamini wawe na kiu ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya matendo yao ambayo yanapaswa kuwa ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Anthony wa Padua alizaliwa tarehe 15 Agosti 1195 huko Lisbon nchini Ureno. Katika umri wa ujana wake, alijisadaka sana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina katika maisha yake, kiasi cha kuwavuta watu wengi kufanya toba na wongofu wa ndani. Alifariki dunia tarehe 13 Juni 1231, akiwa na umri wa miaka 35 tu, matendo makuu ya Mungu. Papa Gregori wa IX, hapo tarehe 30 Mei 1232, akiwa mjini Spoleto, Italia akamtangaza kuwa Mtakatifu. Tarehe 16 Januari 1246 Papa Pio XII akamtangaza kuwa Mwalimu wa Kanisa “Doctor Evangelicus” yaani “Mwalimu wa Injili”. Hii ni kutokana na amana na utajiri uliokuwa unabubujika kutoka katika mahubiri yake yaliyokuwa yanapata chimbuko lake katika Injili. Ibada kwa Mtakatifu Antony wa Padua imeenea sehemu nyingi za dunia. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Padre Carlos Alberto Trovarelli, Mkuu wa Shirika la Utawa wa Ndugu Wadogo Wakonventuali (Order of Friars Minor Conventual), kwa kifupi, OFM Conv., akiwapongeza kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Anthony wa Padua alipowekwa wakfu kama Padre.

Kutoka katika Shirika la Mtakatifu Augustino, akaguswa na mauaji ya kikatili dhidi ya Wafranciskani watano, waliouwawa huko nchini Morocco kutokana na chuki za kidini dhidi ya Wakristo. Tarehe 16 Januari 1220, Mtakatifu Anthony wa Padua “akaamua kupindua meza” ya maisha na wito wake. Akatubu na kumwongokea Mungu na kuanza “kuchanja mbuga” ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa akianzia nchini Morocco. Huko ndiko kulikokuwa kumetokea mauaji ya Wafranciskani watano kutokana na chuki dhidi ya imani: “Odium Fidei”. Akiwa njiani kuelekea Italia, chombo alichokuwa amepanda kikapigwa na dhoruba kali kwenye fukwe za Italia. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata leo hii, bado kuna watu wanazama na kufa maji wakiwa njiani kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kama wakimbizi na wahamiaji. Akiwa Kisiwani Sicilia, akapata nafasi ya kukutana na Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa pamoja wakashikamana kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo nchini Italia na Ufaransa. Hatimaye, Mtakatifu Anthony akaishia mjini Padua, mji ambao hadi leo umebeba umaarufu wa jina lake na mahali ambapo masalia ya mwili wake yamehifadhiwa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jubilei ya Miaka 800 ya wito na maisha ya Mtakatifu Anthony wa Padua, itasaidia kupyaisha utakatifu wa maisha miongoni mwa Wafranciskani pamoja na wafuasi wa Mtakatifu Anthony wa Padua, walioenea sehemu mbali mbali za dunia. Wote hawa wawe na kiu ya kutaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ya Kristo, si tu kwa maneno, bali kwa njia ya matendo yao ambayo yanapaswa kuwa ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Anthony wa Padua, alipenda kushirikiana na kushikamana na: familia, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni kijana aliyesimama kidete kutafuta, kutangaza na kushuhudia ukweli na haki. Msimamo huu, usaidie kupyaisha tena na tena mwamko wa watu kutaka kujisadaka bila ya kujibakiza kama alama ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Anthony wa Padua safari wanayopaswa kuifuata katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu anapenda kuungana kiroho na wale wote wanaoshiriki katika maadhimisho haya kwa njia ya sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ni vyema ikiwa kama kila mwamini ataweza kumwona Kristo Yesu kati ya jirani zake wanaowazunguka. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa faraja na matumaini kwa kutoa fursa kwa watu kusikia na kushuhudia Neno la Mungu, linalopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha kwa kila mwamini. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu amewapatia wote baraka zake za Kitume.  Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Anthony wa Padua amewahi kuandika kwamba, Wakristu ni lazima watabasamu na kufurahi pamoja na Bikira Maria kwa kumwilishwa kwake Kristo Yesu kwa ajili ya wanadamu, lakini pia ni lazima kushiriki mateso yake kama alivyoshiriki Bikira Maria akimuona mwanae akiuawa msalabani. Ni katika ushiriki wa yote hayo ambapo Mama huyu alibaki kuwa mwaminifu mpaka mwisho, ndio sababu mwanae alipenda kumpaliza mbinguni. Ni mwaliko kwa waamini wote kuvumilia kwa uaminifu taabu na mahangaiko mbali mbali ya maisha, ili siku moja waweze pia kushiriki furaha na utukufu katika jumuiya ya watakatifu mbinguni. Kama Kristo alivyomnyanyua Bikira Maria katika unyonge wake na kumpa utukufu mbinguni, ndivyo atakavyowanyanyua wanyonge katika taabu zao, kama anavyoimba Mama Bikira Maria mwenyewe kwenye utenzi wake “Magnificat”: “amewashusha wenye nguvu toka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu” (Luka 1: 52).

Mtakatifu Anthony wa Padua alijifunza unyenyekevu wa Mama Bikira Maria, akashinda vishawishi vya madaraka, majivuno na mambo ya dunia. Hakuna huduma ya siasa, elimu, afya, kazi yeyote au maisha ya familia yatakayoweza kuwa na mafanikio bila unyenyekevu. Kama vile Kristo anavyowaosha miguu mitume, ndivyo anavyoalika kila mmoja katika huduma yeyote, kuhangaikia wengine kwa unyenyekevu na sio kuwa na majivuno (Rej. Yohane 13:12). Kwa hali ya jamii leo, ni lazima kuwahudumia na kuwahangaikia kwa namna zote wakimbizi, wahamiaji na wasio na makazi, wapweke, wagonjwa, wafungwa, maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini watakuwa wafuasi kweli wa Kristo wenye kuzaa matunda bora na yanayodumu, iwapo watajifunza kujitoa kwa ajili ya wengine kwa unyenyekevu kama alivyofanya Mtakatifu Anthony wa Padua, hata ikibidi kujitoa sadaka kubwa, kama alivyojitoa Mtakatifu Maximilian Kolbe, akakubali kufa yeye ili aokoe maisha ya baba wa familia. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, na watakatifu Anthony wa Padua na Maximilian Kolbe, waamini wataweza kumshuhudia Kristo wa Msalaba, na kuleta utukufu wa Mungu kati ya watu katika dunia hii ya leo yenye changamoto nyingi ambapo wanyonge wanaonekana kuathirika zaidi.

Papa: Mt. Anthony wa Padua: Miaka 800

 

 

12 June 2020, 07:42