Papa Francisko asikitishwa na hali tete ilivyo nchini Libya, awataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya amani na utulivu, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu! Papa Francisko asikitishwa na hali tete ilivyo nchini Libya, awataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya amani na utulivu, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Papa Francisko asikitishwa na hali tete nchini Libya!

Familia ya Mungu nchini Libya anasema Baba Mtakatifu imekuwa katika sala zake katika kipindi cha hivi karibuni. Ametumia fursa hii, kuwaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wale wote wenye dhamana ya kisiasa na kijeshi nchini Libya, kuanza kwa ari na mwamko mpya mchakato wa kusitisha mapambano ya kivita, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Jumapili tarehe 14 Juni 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, anaendelea kufuatilia kwa wasi wasi na uchungu mkubwa hali tete ya kisiasa nchini Libya. Familia ya Mungu nchini Libya anasema Baba Mtakatifu imekuwa katika sala zake katika kipindi cha hivi karibuni. Ametumia fursa hii, kuwaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wale wote wenye dhamana ya kisiasa na kijeshi nchini Libya, kuanza kwa ari na mwamko mpya mchakato wa kusitisha mapambano ya kivita, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa amani, utulivu na umoja wa kitaifa. Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji; watu wasiokuwa na makazi pamoja na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.

Janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, limeendelea kuhatarisha hali ya watu hawa wanaoendelea kunyonywa, kudhulumiwa huku wakifanyiwa ukatili wa kutisha.Baba Mtakatifu anapenda kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia mahangaiko ya watu hawa, kwa kupembua njia zitakazosaidia kutoa ulinzi na usalama; kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu kama chachu ya matumaini ya ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu amewaalika waamini kusali kwa ukimya ili kuwaombea watu wa Mungu nchini Libya, kwani kila mtu anawajibika kikamilifu.

Kila mwaka ifikapo tarehe 14 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani. Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa kuhusu huduma ya damu salama, kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari na pamoja na kuwatambua na kuwaenzi watu ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu. Hawa ni watu walioathirika kutokana na vita, magonjwa ya milipuko, ajali pamoja na majanga asilia. Aidha, Siku ya Wachangia Damu Duniani ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa ya Ndugu Karl Landsteiner, ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi ya damu ya “A”,”B” na “O”, na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo.

Siku ya Wachangia Damu Duniani kwa Mwaka 2020. Baba Mtakatifu amesema, hiki ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa kijamii, kwa kutambua na kuguswa mahitaji ya damu safi na salama kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa watu wa kujitolea damu safi na salama. Ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa sadaka na majitoleo kwa jirani zao. Ni jambo la kawaida, lakini lina maana na uzito wa pekee katika kuokoa maosha ya watu kwa kutoa damu. Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka wale wote waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na wale wote waliokuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo vya mawasiliani na mitandao ya kijamii.

Papa: Libya 2020
14 June 2020, 13:45