Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS anakazia kuhusu ari na mwamko mpya wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa! Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS anakazia kuhusu ari na mwamko mpya wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!  (Pe. Josiah K´Okal) Tahariri

TAHARIRI: Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mashirika ya PMS

Mafanikio ya kimisionari ni furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni matunda ya Roho Mtakatifu. Kiwango hiki cha furaha hakuna mtu anayeweza kujitwalia mwenyewe. Kuwa mmisionari maana yake ni kujisadaka kama ushuhuda wa utume unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Wamisionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, uliokuwa umepangwa kufanyika mjini Roma tarehe 21 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbingu, uliahirishwa na badala yake, Baba Mtakatifu Francisko akawatumia Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, ujumbe maalum. Katika ujumbe, huu, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya Injili, kama mashuhuda wa zawadi ya imani. Wawe ni watu wenye mvuto kutokana na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mihimili ya uinjilishaji iwe ni kielelezo cha shukrani na sadaka inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Wasaidie kurahisisha mambo na wala wasiyagumishe hata kidogo, daima wakijitahidi kuwa karibu na maisha ya waamini wanaowainjilisha kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei”. Wajitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anayataka Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuondokana na dhana ya kutaka kujitafuta yenyewe, kwa ajili ya kujiendeleza, hali ambayo inaweza kufananishwa na watu “wanaotaka kujipigia debe ili kukuza shughuli zao kwa mafao yao binafsi”.Mashirika haya yawe mstari wa mbele katika sala sanjari na kukusanya fedha kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni huduma muhimu kwa ajili ya utume wa Makanisa mahalia, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni mtandao wenye sura na tamaduni nyingi, changamoto na mwaliko ni kuhakikisha kwamba, imani ya Wakristo inashuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni vyombo vya Injili ya huruma na upendo inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni katika muktadha huu, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, katika Tahariri yake kuhusu Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, anakazia umuhimu wa ujumbe huu kama chemchemi ya ari na mwamko mpya wa shughuli za kimisionari. Baba Mtakatifu amegusia mambo msingi ambayo Kanisa halina budi kuyaacha pamoja na magonjwa ambayo yanaweza kuhatarisha maisha na utume wa Mama Kanisa. Anasema, utume wa Kanisa si matokeo ya utumiaji muafaka wa mifumo na mantiki za ulimwengu mamboleo au ufanisi wa matumizi ya weledi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mafanikio ya kimisionari ni furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa hakika ni matunda ya Roho Mtakatifu. Kiwango hiki cha furaha hakuna mtu anayeweza kujitwalia mwenyewe. Kuwa mmisionari maana yake ni kujisadaka bila ya kujibakiza kama ushuhuda wa utume unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Wamisionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Yesu Mfufuka na Roho Mtakatifu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linaendelea kuishi na kumwilisha neema za Kristo Yesu. Kanisa halina mng’ao wake binafsi, vinginevyo, litaishia kujitafuta lenyewe na hivyo kujiamini kupita kiasi. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawaalika waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya wenye mhuri wa furaha ambayo daima ni mpya na ambayo waamini wanapaswa kuwashirikisha jirani zao, baada ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Hii ni furaha inayoinjilisha, inayopendeza na kufariji. Furaha ya Injili ni chachu ya kutangaza na kushuhdia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakazia ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa; mambo yanayopaswa kujikita katika shughuli za kichungaji zinazofumbatwa katika majadiliano, toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari.

Kuna tofauti kubwa kati ya kutangaza na kushuhudia imani pamoja na wongofu wa shuruti unaoweza kujikita katika masuala ya kisiasa, kitamaduni, kisaikolojia au kidini. Kanisa litaendelea kustawi na kuchanua kama “mtende wa Lebanoni” ikiwa kama litamfuata Kristo Yesu, chemchemi ya furaha; kwa kuvutwa naye, kiasi kwamba, hata watu wengine pia wakaweza kuona mwelekeo huu, kiasi hata cha kushika tama kwa mshangao mkubwa! Baba Mtakatifu anawataka wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, kutambua kwamba, utume wa Kanisa si kwa ajili ya wateule wachache ndani ya Kanisa, au jambo la binafsi linaloweza kutendeka kwa kujiwekea sera na mikakati mezani kwao. Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kutambua kwamba si tu kwa njia ya upembuzi yakinifu, wito, ujasiri pamoja na kujiongeza mambo yanaweza kuwa shwari.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hii ni hatari kubwa inayoweza kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, unavuka mipaka ya wakurugenzi hawa na kuliambata Kanisa zima. Utume wa Kimisionari ambao ndio unaoelekezewa ujumbe huu, ni changamoto kwa mihimili ya uinjilishaji kutojitafuta yenyewe. Waamini wamebatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika maisha yao. Baba Mtakatifu anataja baadhi ya sifa maalum kwa utume wa Kikristo: ni moyo wa shukrani na sadaka; unyenyekevu, ujirani mwema na uwepo wa karibu katika maisha ya watu, jinsi walivyo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.

Tahariri: Tornielli
28 May 2020, 06:54