Baba Mtakatifu Francisko ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inadumisha utu, heshima, haki msingi, ustawi na mafao ya wafanyakazi wote! Baba Mtakatifu Francisko ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inadumisha utu, heshima, haki msingi, ustawi na mafao ya wafanyakazi wote! 

Papa Francisko: Dumisheni: Utu, Heshima na Haki za Wafanyakazi

Baba Mtakatifu anasema, ameguswa zaidi na ujumbe uliotolewa na wafanyakazi wa kutwa wanaotumikishwa kwenye sekta ya kilimo nchini Italia, na wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu wanaonyonywa na kudharirishwa utu, heshima na haki zao msingi. Papa anasema, binadamu anapaswa kuwa ni kiini na hatima ya sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafafanua kwamba, kazi inaeleza upande wa uwepo wa mwanadamu ulio wa muhimu kabisa wa ushiriki na sio tu katika tendo la uumbaji, bali pia katika tendo la Ukombozi. Wale wanaopokea ugumu wa kazi kwa kuunganisha na Yesu wanashiriki kwa namna fulani na Mwana wa Mungu katika kazi yake ya Ukombozi na kuonesha kwamba ni wanafunzi wa Yesu, ndio wanaochukua msalaba wake, kila siku, kwa njia ya kazi waliyoitwa kuifanya. Katika mtazamo huu, kazi inaweza kuchukuliwa kama njia ya kutakatifuza na kuchochea mambo halisi ya kidunia kwa njia ya Roho wa Kristo. Kwa kueleweka hivi, kazi inaelezea utu kamili wa mwanadamu, katika hali ya kihistoria na katika mtazamo wa kitaalimungu wa mambo ya kifo na hukumu ya mwisho. Vitendo vya kiuwajibikaji na kiuhuru vya mwanadamu vinaonyesha uhusiano wake wa asili na wa ndani na Mungu na uwezo wake wa uumbaji. Wakati huohuo, kazi ni msaada wa kila siku katika kukabiliana na aibu na uharibifu wa dhambi, hata kazi inapokuwa ni kwa njia ya jasho mtu anapata riziki yake.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Mwanadamu aliye sura na mfano hai wa Mungu katika ulimwengu huu amekabidhiwa ulimwengu na yote yaliyoko ndani yake ili ayamiliki na kuyatiisha kwa kufanya kazi. Kazi ndicho kipimo cha utu wa mtu, mwenye mahusiano na binadamu wengine. Lengo la kazi ni kumsaidia mwanadamu na sio mwanadamu ageuke kuwa mtumwa wa kazi. Mahusiano yake na mwanadamu mwingine yasigeuke kuwa ni chukizo mbele ya Mungu, badala ya kuwa furaha, faraja na utimilifu wa utu wa mtu mwenyewe! Kwa ufupi kabisa, haki msingi za binadamu zinafumbatwa katika utu na heshima ya kila mwanadamu. Kazi ni utimilifu wa utu wa mwanadamu na inapaswa kuheshimiwa kwa kuzingatia pia utu wa mfanyakazi. Kuchechemea kwa uchumi wa kitaifa na kimataifa kutokana na athari za homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni changamoto katika ulimwengu wa wafanyakazi, unaotishia nafasi za kazi na ajira kwa mamilioni ya watu duniani sanjari na usalama wa maisha yao. Kazi inayozingatia utu wa mwanadamu itatoa fursa kwa wafanyakazi kuweza kutekeleza majukumu yao msingi ndani ya familia na kumwakikishia mfanyakazi maisha yenye heshima baada ya kustahafu kazini. Kazi ni msingi wa maendeleo, ndiyo maana kazi inakwenda sanjari na: utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Mei 2020 amewashirikisha waamini na watu wenye mapenzi mema, ujumbe na matashi mema katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Ulimwenguni, maarufu kama Mei Mosi. Ujumbe wa Siku kuu ya Wafanyakazi Ulimwenguni kwa mwaka 2020 umegusia changamoto mamboleo katika ulimwengu wa wafanyakazi. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, ameguswa zaidi na ujumbe uliotolewa na wafanyakazi wa kutwa wanaotumikishwa kwenye sekta ya kilimo nchini Italia, na wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu wanaonyonywa na kudharirishwa utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna athari kubwa za myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, lakini binadamu anapaswa kuwa ni kiini na hatima ya sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anapenda kuunga mkono wito uliotolewa na wafanyakazi wa kutwa, wanaonyonywa na kudharirishwa, ili kwamba, kipeo hiki iwe ni fursa ya kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza, ili utu, heshima na haki msingi za binadamu na utu wa kazi uweze kupewa kipaumbele cha kwanza!

Papa: Wafanyakazi
06 May 2020, 14:19