Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu Sherehe ya Pentekoste amezungumzia: COVID-19 Ukanda wa Amazonia, Siku ya Faraja Kitaifa Italia na Umoja wa Mshikamano. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu Sherehe ya Pentekoste amezungumzia: COVID-19 Ukanda wa Amazonia, Siku ya Faraja Kitaifa Italia na Umoja wa Mshikamano. 

Papa Francisko: Ukanda wa Amazonia! Siku ya Faraja: Corona!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, 31 Mei 2020 amezungumzia kuhusu janga la maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 Ukanda wa Amazonia na umuhimu wa huduma kwa watu badala ya kutoa kipaumbele kwa ukuaji wa uchumi! Amegusia Siku ya Faraja Kitaifa Nchini Italia pamoja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikakama dhidi ya Corona!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 31 Mei 2020 amegusia mambo makuu matatu; Hitimisho ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia, Siku ya Faraja Kitaifa nchini Italia pamoja na matashi mema ya Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yalifanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". nBaba Mtakatifu Francisko anasema, imegota miezi saba tangu maadhimisho haya yalipofungwa rasmi mjini Vatican. Katika Sherehe ya Pentekoste, waamini wamwombe Roho Mtakatifu Mfariji aweze kulipatia Kanisa mwanga na nguvu ya kukabiliana na changamoto ya janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ukanda wa Amazonia umeguswa na kutikiswa sana. Kuna mamilioni ya watu walioambukiza na maelfu ya watu tayari wamepoteza maisha na kati yao, wamo pia watu mahalia! Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Amazonia, awaombee maskini na wale wote wasiokuwa na ulinzi katika eneo hili na sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anaialika Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, hakuna hata mtu awaye yote atakayekosa huduma ya afya kama sehemu ya mpango mkakati wa kupambana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Huduma ya afya kwa watu wa Munguinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si sera na mikakati ya kufufua uchumi. Binadamu ni Hekalu la roho Mtakatifu

Wakati huo huo, nchini Italia, tarehe 31 Mei 2020 wanaadhimisha Siku ya Faraja Kitaifa. Lengo ni kuwahamasisha watu wa Mungu kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na wagonjwa pamoja na wale wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya, ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Kwa hakika, wamekuwa ni mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo kwa jirani zao. Hawa ni watu ambao kwa hakika wamehatarisha na hata kutoa maisha yao kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa Virusi vya COVID-19. Baba Mtakatifu na waamini wamewakumbuka na kuwaombea katika ukimya.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Sherehe njema ya Pentekoste. Watu wa Mungu wanahitaji mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu. Kanisa linahitaji zawadi hii, ili liweze kudumisha umoja na kuendelea kusonga mbele kwa ujasiri, huku likitangaza na kushuhudia Injili. Zawadi hizi zinahitajika hata kwa familia ya binadamu katika ujumla wake, ili kuondokana na janga la maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, ikiwa imeungana na kushikamana kwa dhati na kamwe ubinafsi na utengano visipate nafasi tena katika Jumuiya ya Kimataifa! Baba Mtakatifu amewakaribisha waamini kwani kuanzia sasa ataendelea kutoa tafakari yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Matendo makuu ya Mungu.

Papa: Amazonia
31 May 2020, 13:52