Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika sala ya Malkia wa Mbingu siku ambayo Mama Kanisa anasheherekea Siku kuu ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni. Papa Francisko katika sala ya Malkia wa Mbingu siku ambayo Mama Kanisa anasheherekea Siku kuu ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni.  (ANSA)

Papa Francisko:Kanisa linasindikiza kila mtu katika njia!

Kutangaza,kubatiza na kufundisha kutembea katika nyayo za Injili kwa kutoa ushuhuda, ndiyo utume anaowakabidhi Yesu Mitume katika siku ya kupaa kwake.Amesema hayo Papa Francisko wakati wa tafakari yake kabla ya sala ya Malkia wa Mbingu na kusisitiza kuwa Kristo daima yupo pamoja nasi,tujifunza kutazama hali halisi katika mwanga wa Mfufuka.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Leo hii inchini Italia na Nchi nyingine, wanaadhimisha Siku kuu ya Kupaa kwa Bwana.  Sehemu ya Injili ya Matayo 28,16-20, inatuonesha Mitume ambao walikuwa wamekusanyika huko Galilaya “juu ya Mlima ambao Yesu alikuwa amewaelekeza”. Hapa ndipo walikuwa na mkutano wao wa  mwisho na Bwana Mfufuka na wafuasi wake. Mlima unabeba ishara nyingi zenye nguvu, kwani hapo: Juu ya Mlima Yesu alihubiri kuhusu Heri (Mt 5,1-12); Yesu alikuwa akijitenga peke yake juu ya mlima na kusali (Mt 14,23);  Katika mlima alikuwa akiwapokea umati mkubwa na kuponya wagonjwa (Mt 15,29). Lakini kwa mara hii akiwa mlimani Yeye siyo tena Mwalimu ambaye anatenda na kuwafundisha bali ni Yule anayewaomba wafuasi wake watende na kutangaza, akiwakabidhi kuendeleza utume wake.

Ndiyo mwanzo wa Tafakari ya Papa Francisko akiwa katika Maktaba ya Kitume Vatican, siku ya Jumapili  tarehe 24 Mei 2020 ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni. Kiini cha mahubiri yake ameonesha wazi kwamba  kutangaza, kubatiza na kufundisha kutembea katika nyayo za Injili kwa kutoa ushuhuda ndiyo utume ambao Yesu anawakabidhi Mitume katika siku ya kupaa kwake na vile vile kuwahakikishia kuwa Yeye yupo pamoja nasi na kwa maana hiyo, Papa ameongeza kuwa ni muhimu kujifunza kutazama hali halisi katika mwanga wa Mfufuka.

Kutoa ushuhuda wa sababu ya imani yetu

Papa Francisko akiendelea na tafakari zaidi amesema, Yesu anawakabidhi utume wake ili waupeleke kwa watu wote. “Haya basi Enendeni na mkawafanye wote kuwa wafuasi wangu, kwa kuwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, mkiwafundisha kutii kile nilicho waamuru”(Mt 28,19-20. Mantiki ya utume uliokabidhiwa kwa Mitume upo  katika mambo haya, kutangaza, kubatiza, kufundisha kutembea katika njia iliyopitiwa na Mwalimu, yaani ya Injili iliyo hai. Ujumbe huu wa wokovu awali ya yote unahitaji ushuhuda, ambao hata sisi, wafuasi wake leo hii, tunaalikwa kutoa sababu ya imani yetu, bila ushuhuda hatuwezi kutangaza”.

Hatustahili lakini tusikate tamaa

Na mbele ya zoezi lenye kina namna hii na kwa kufikiria udhaifu wetu, Papa Francisko anasema, tunahisi kutostahili, kama kwa hakika walivyohisi hata Mitume wenyewe”, Papa amesisitiza. Lakini hatupaswi kukata tamaa kwa kukumbuka maneno ambayo Yesu aliwambia wao kabla ya kupaa Mbinguni “Mimi niko pamoja nanyi hadi miisho ya ulimwengu” (Mt 28,20). Ahadi hii inahakikisha uwepo wake kila wakati na faraja ya Yesu kati yetu.  Lakini je uwepo wake huu unakamilika namna gani? Ni kwa njia ya Roho yake ambaye anafanya Kanisa litembee katika historia kama msindikizaji wa kila  mtu katika njia zake.

Roho wa Yesu na Baba anaondoa dhambi na kutakatifuza

Roho aliyeletwa na Yesu na Baba, anaondoa dhambi na kutakatifuza wote ambao wanatubu, wanajifungulia kwa imani zawadi yake, amesema Papa. Katika ahadi ya kutaka kubaki na sisi hadi miisho ya dunia, Yesu anazindua mtindo wa  uwepo wake ulimwenguni kama Mfufuka. Uwepo wake ambao unajifunua katika Neno, katika Sakramenti, katika matendo ya kila wakati na ule undani wa Roho Mtakatifu. Siku kuu ya Kupapa kwa Bwana inaeleza kuwa licha ya  Yesu kupaa Mbinguni ili kukaa katika  utukukufu yaani  kuume kwa Baba, bado yupo kati yetu daima. Na ndipo tunapata nguvu, uvumilivu wetu na furaha yetu, ambayo ni ni uwepo wa Yesu kati yetu na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Kwa kuhitimisha Papa Francisko anakimbilia ulinzi wa mama yetu na kusema  “Bikira Maria asindikize safari zetu kwa ulinzi wa umama wake. Kwake yeye tujifunze upole na ujasiri wa kuwa mashuhuda wa Bwana Mfufuka katika ulimwengu.

24 May 2020, 13:55