Tafuta

Papa Francisko:Ni Roho Mtakatifu anaweza kusaidia kuondokana na janga na umaskini!

Mateso ya janga la wakati huu hayatasaidia kitu ikiwa hakuna mwelekeo wa kujenga jamii iliyo na haki zaidi na usawa.Ni maneno ya Papa Francisko wakati wa kutoa ujumbe wake kwa njia ya video katika lugha ya kispanyola kwenye fursa ya Kesha la Pentekoste kwa ngazi ya kimataifa iliyoandaliwa na CHARIS,Jumamosi usiku tarehe 30 Mei 2020.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Papa Francisko ametoa ujumbe wake kwa njia ya video kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki CHARIS” Ulimwenguni katika fursa ya Mkesha wa Pentekoste ulimwenguni ulioandaliwa na kufanyika kwa njia ya mtandaoni. CHARIS ilianzishwa rasmi  na Baraza la Kipapa la Familia, Ndoa na Maisha kunako madhimisho ya Pentekoste mwaka jana. Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Hayo ni maneno ya somo lililosomwa mwanzo wa sura ya pili ya kitabu cha Matendo ya Mitume Papa amesema. Hata leo hii shukrani kwa maendeleo ya kifundi, tumeunganishwa waamini wa pande tofauti za ulimwengu katika mkesha wa Pentekoste, ambapo  simulizi inaendelea kusema kuwa “kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao na wote wakajazwa Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu anatua juu yetu

Papa Francisko amebainisha kuwa Roho Mtakatifu anatua kwa kila mfuasi hata sisi. Roho aliyehaidiwa na Yesu anapyaisha, anatoa uongofu, anaponya kila mmoja wetu. Anakuja kuponyesha hofu, ni hofu ngapi tulizonazo, ukosefu wa uhakika; lakini yeye anakuja kutuponyesha majeraha, hata tunayomsababishia mwingine; na anakuja kutubadili kuwa wafuasi, wamisionari, mashuhuda waliojaa ujasiri. Ili kuweza  kuzungumza kwa lugha ya kitume, kuna  ulazima wa kuhubiri Injili ya Yesu kama tunayosoma, kwenye aya zinazofuata kwa kile kilichowatokea wanafunzi. Leo hii zaidi Papa Francisko amesema kuna haja kwamba Baba atutumie Roho Mtakatifu. Aidha  katika sura za kwanza za Kitabu cha Matendo ya Mitume, Yesu anawambia wanafunzi wake “ wasubiri ukamilifu wa ahadi ya Baba “ule ambao mlisikia kutoka kwangu ya kwamba “ Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi siku chache mtabatiza kwa Roho Mtakatifu”. Na katika haya ya nane anaongeza: “ Mtapokea nguvu ya Roho Mtakatifu ambaye atashuka juu yenu na mtakuwa mashuhuda huko Yerusalem, Uyahudi yote na Samaria hadi miisho ya Dunia”.

Ushuhuda wa Yesu

Roho Mtakatifu anatupelekea kushuhudia Yesu. Leo hii dunia inateseka na imejeruhiwa; tunaishi katika dunia ambayo umejeruhiwa sana na kuteseka hasa katika maskini zaidi na walio baguliwa, kwa sasa ambapo nguvu za kibinadamu zimepotea, ulimwengu unahitaji Yesu. Inahitajika ushuhuda wa Injili, Injili ya Yesu. Ushuhuda huu tunaweza kuuita tu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Tunahitaji kwamba Roho Mtakatifu atujalie macho mapya, atufungue akili zetu na mioyo yetu kwa ajili ya kukabiliana na wakati wa sasa  na ujao kutokana na funzo tuliopata. Sisi sote ni binadamu mmoja. Hakuna anayejiokoa mwenyewe. Mtakatifu Paulo katika barua kwa wagalatia anasema “Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. (Wagalatia 3, 28) na hiyo imewezekana kwa njia ya Roho Mtakatifu, katika Ubatizo wa Roho Mtakatifu ambao ulitangazwa na  Yesu.

Uwajibikaji wa kujenga hali halisi mpya

Tunajua na kutambua lakini katika janga hili ambalo tunaishi, tumekuwa na uzoefu kwa namna kuu sana. Uwajibikaji wa kujenga hali halisi mpya uko mbele yetu. Hata hivyo Bwana atafanya hivyo: sisi tunaweza kushirikiana, kwa maana anasema “tazama mimi ninafanya yote kuwa mapya (Ufunuo 21, 5).  Tutakapoondokana na janga hili Papa amesema hatuweza kuendelea kufanya kile tulichokuwa tunafanya awali, na kama tulivyokuwa tunafanya .Haitakuwa tofauti yote. Mateso yote haya hayatasaidia lolote ikiwa sisi hatutaweza kujenga pamoja jamii ya haki zaidi, yenye usawa zaidi, ya ukristo zadi, si kwa jina bali katika matendo, kwa hali halisi ambayo ipelekee mwenendo wa Kikristo. Ikiwa hatutafanya kazi pamoja ili kushinda janga hili la umaskini duniani, janga la umasikini katika nchi za kila mmoja wetu, katika mji ambao kila mmoja anaishi, kipindi  hiki kitakuwa ni cha bure. Papa Francisko amesisitiza kwamba katika majaribu makubwa ya ubinadamu, miongoni mwake kama hili la janga, kwa kawaida ni kuondokana kwa ubora zaidi au mbaya zaidi, haiwezekani kufanana.

Je tunataka kuondokana tukiwa bora zaidi au mbaya zaidi?

Papa Francisko amewauliza  swali kama wanataka kuondokana wakiwa bora au mbaya zaidi? Na ndiyo maana leo hii amesema tunataka kuomba kwa Roho Mtakatifu ili Yeye aweze kubadili mioyo yetu na kutusaidia kuwa bora zaidi. Ikiwa tutaishi kwa kuhukumiwa kwa mujibu wa kile ambacho Yesu anasema “kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. ( Mt 25, 35-36), kwa hakika tutatoka humo tukiwa bora zaidi. Papa Francisko amesema hiyo ndiyo kazi ambayo ni yetu sote na hata kwa CHARIS ambao ni wakarismatiki walioungana.

Maneno ya kinabii ya Papa Yohane XXIII

Katika hati ya Malines, iliyoandikwa miaka ya Sabini na Kardinali Suenens na  Askofu  Helder Camara, kwa kupewa jina la “ Upyaisho wa Karismatiki na huduma ya watu”  inatoa ishara hiyo ya safari kama chama cha neema. Muwe waaminifu kwa wito huu wa Roho Mtakatifu ! Papa amewahimiza. Aidha amekumbuka maneno ya kinabii ya Papa Yohane XXIII aliyehitisha Mtaguso wa Vatican II na ambapo Upyaisho wa Karismatiki unamkumbuka kwa namna ya pekee. Yeye alisema “Anastahili kuabudiwa Roho wa Mungu, ambaye anatoa matarajio kwa wote kwa kupokea maombi haya, ambayo kila siku yanatokea pande zote za ulimwengu: Pyaisha wakati huu wa zawadi karibu kama Pentekoste mpya, ulijalie Kanisa Takatifu ambalo kwa maombezi ya Maria Mama wa Yesu na kiongozi wa Mtakatifu Petro, ufalme wa Mungu mwokozi upanuke, ufalme wa ukweli na haki, ufalme wa upendo na wa amani! Kwa kuhitimisha Papa Francisko amewatakia kwamba mkesha huo uwe wa faraja ya Roho Mtakatifu na nguvu ya Roho Mtakatifu iwe kwa ajili ya kuondokana na wakati huu wa uchungu, wa huzuni na majaribu ambayo ni ya janga. Na ili kuondokana tukiwa bora zaidi.

 

31 May 2020, 09:33