2020.05-02  Papa Francisko  wakati akiwa katika ziara nchini  Paraguay  katika madhabahu ya Bikira Maria Caacupe julai 2015 2020.05-02 Papa Francisko wakati akiwa katika ziara nchini Paraguay katika madhabahu ya Bikira Maria Caacupe julai 2015 

Papa atuma baraka nchini Paraguay iliyowekwa wakfu kwa Bikira Maria wa Caacupé

Katika ujumbe mfupi wa Papa Francisko umewafikia watu wa Mungu na Kanisa zima la Paraguay akiwashukuru juu ya kuwa na ibada ya mama Maria ambapo katika kipindi hiki kama ilivyo hata katika dunia nzima maaskofu wengi wanafanya hivyo. Hivi karibuni Maaskofu nchini humo wameweka wakfu nchi kuwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria wa Caacupe.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Shukrani, baraka na sala ni mambo matatu ambayo yanaonekana katika ujumbe ambao Papa Francisko kwa njia ya Askofu Mkuu, Edgar Peña Parra, aliyekuwa Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican katika masuala ya nchi za nje, kwa Baraza la Maaskofu wa Paraguay ambao hivi karibuni waliweka wakfu Nchi hiyo kuwa Msimamizi wake Bikira Maria wa Miujiza wa huko Caacupé.

Papa kwa kuwapongeza katika juhudi hizo, anawabariki waamini wote na huku akiwaomba waweze kusali kwa ajili yake na kwa ajili ya matunda ya huduma yake kwa watu watakatifu wa Mungu. Na wakati huo huo, anamwomba Mama Maria wa  Caacupé ulinzi wake  na juu ya taifa zima. Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu wa Paraguay kupitia tovuti yao, ujumbe huo umeelekezwa kwa Rais wa Baraza la Maaskofu nchini humo, Askofu Adalberto Martínez Flores, na kutangazwa tarehe Mei Mosi.

Sherehe ya kuwekwa wakfu nchi ya Paraguay kwa Bikira Maria wa Caacupé ilifanyika kunako tarehe 3 Aprili, majari ya jioni, mahali ambapo walianza na milio ya pamoja wa kengele zote za Makanisa ya nchi nzima. Baadaye ilifuata sala ya jumuiya ya Roasari iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo la Caacupé, Askofu  Ricardo Valenzuela Rios, na kusindikizwa na maaskofu wote kwa njia ya mtandao kila mmoja katika makao makuu yao, mapadre, waseminari, mashemasi, watawa kike na kiume, waamini na wahamiaji wote wa Paraguay katika ulimwengu. Ibada yote hiyo  ilitangazwa moja kwa moja kwa njia ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwa sababu ya janga la virusi vya corona, na hapakuwapo uwezekano wa kuadhimisha kwa ushiriki kimwili kwa waamini.

Ikumbukukwe kunako tarehe 11 Julai 2015 katika fursa ya ziara ya Kitume nchini Paraguay, Papa Francisko aliadhimisha misa katika uwanja hatua chache kutoka katika Madhabau ya Mama Maria wa Caacupé. Katika mahubiri yake wakati huo alisema: “ kujikuta katikati yenu hapa ni kuhisi kuwa nyumbani, chini ya miguu ya Mama Yetu Bikira wa Miujiza ya Caacupé. Katika madhabahu ,sisi watoto tunakutana na Mama Yetu na kati yetu tunakumbushana kuwa sisi ni ndugu. Ni eneo la siku kuu, la mkutano na la familia. Tunakuja kuleta mahitaji yetu, tunakuja kushukuru na kuomba msamaha na kuanza kwa upya. Ni wangapi wamebatizwa, miito mingapi ya mapadre na watawa, ni wachumba wangapi na ndoa ambazo zimezaliwa nchini ya miguu ya Mama: Machozi na vilio vingapi chini ya miguu yako! Tunakuja daima na maisha yetu, kwa sababu hapa tupo nyumbani, jambo ambalo ni bora ni kujua kuwa hapa wewe unatusubiri”. Na mwezi Novemba 2017  katika bustani za Vatican, ilizinduliwa picha moja inayoonyesha Bikira Maria wa Caacupé.

02 May 2020, 15:36