Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mashemasi ndani ya Kanisa ni: Wahudumu wa Injili ya Upendo kwa watu wa Mungu katika Neno na mahitaji msingi ya watu wa Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mashemasi ndani ya Kanisa ni: Wahudumu wa Injili ya Upendo kwa watu wa Mungu katika Neno na mahitaji msingi ya watu wa Mungu! 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Mei 2020: Mashemasi wahudumu wa Injili ya Upendo

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu. Ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu imegawanyika katika Madaraja makuu matatu: Daraja ya Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Daraja ya Ushemasi “Diakonia” huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa: Shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu! Utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia katika huduma ya Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza. Huu ni wito na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake. Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2020 zinazosambazwa kwa njia ya video na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea Mashemasi ndani ya Kanisa. Hawa ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na wanajitahidi kuishi wito wao kwenye familia pamoja na familia zao. Ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni walinzi na wasimamizi wa huduma katika Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwaombea Mashemasi ili kwa njia ya uaminifu wao katika huduma ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kwa maskini, waweze kuwa kweli ni alama ya uhai wa Kanisa zima!

Padre Frèdèric Fornos, Mkurugenzi mkuu wa Utume wa Sala Kimataifa anakumbushia umuhimu wa kunafsisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama njia muafaka ya kumfuasa Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi. Kristo Yesu anaonesha kwamba, uongozi ndani ya Kanisa unapaswa kuwa ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Anakumbusha kwamba, “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” Mt. 20: 28. Mama Kanisa anawahimiza waamini wake kuwa na mwelekeo sahihi wa huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, Kanisa linawahitaji kwa udi na uvumba  Mashemasi ambao ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu.

Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019 iliongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani” inasema: Baada ya kusikilizana kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji na kitamaduni. Kanisa limeangalia pia njia mpya za wongofu Ukanda wa Amazonia pamoja na kutoa hitimisho la Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujizatiti katika mchakato wa “Diakonia” yaani huduma. Mashemasi wawe mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha ekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu, shughuli za kichungaji na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, Kanisa liwe ni shuhuda wa huduma kwa kuendelea kuwa “Mtumishi mwaminifu na Mwenye huruma, Msamaria mwema na zaidi kwa kuendelea kujenga na kuimarisha mshikamano kama kielelezo cha Ushemasi wa Kanisa.

Ni za Papa Mei 2020
06 May 2020, 06:54