Kanisa linafanya Kumbu kumbu ya Miaka 39 tangu lilipotokea Jaribio la Kutaka Kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II hapo tarehe 13 Mei 1981 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Kanisa linafanya Kumbu kumbu ya Miaka 39 tangu lilipotokea Jaribio la Kutaka Kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II hapo tarehe 13 Mei 1981 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. 

Miaka 39 ya Jaribio la Kutaka Kumuua Papa Yohane Paulo II.

Mt. Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Mt. Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake. Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale alipoonekana yupo kwenye mahangaiko ya kuugua kwa muda mrefu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 13 Mei ya kila mwaka anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Kwa mwaka 2020, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Miaka 39 tangu Jaribio la kutaka Kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II lilipofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ilikuwa ni tarehe 13 Mei 1981, siku ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alipouona mkono wa Bikira Maria katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbali mbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Lucia na Yacinta. Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa. Hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa pamoja na kupandikiza mbegu ya kifo.

Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa nyakati tofauti. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga asilia, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia. Siri ya tatu hakikuweza kufunuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Askofu mahalia. Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa na alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Sala ni nguzo muhimu sana katika maisha dhidi ya wasi wasi wa kifo anasema Mtakatifu Yohane Paulo II.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake. Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale alipoonekana yupo kwenye mahangaiko ya kuugua kwa muda mrefu, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye amani, furaha na utulivu wa ndani. Ni mwamini ambaye alikuwa safarini kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele. Hiyo ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo katika maisha yao. Ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mnamo Mei 13 mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliendelea na maisha na utume wake katika hali ya utulivu na amani ya ndani.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu, kabla ya kukata roho, alipenda kuwakabidhi wanafunzi wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Ndiyo maana Mama huyu alikuwa na nafasi ya pekee sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Katika maisha kila mtu amekabidhiwa Msalaba wake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Msalaba huu unakuwa ni chemchemi ya upendo na mwanga angavu wa maisha! Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata katika dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Miaka 38 ya Jaribio la Mauaji ya Yohane Paulo II

 

12 May 2020, 13:21