Tafuta

Vatican News
Mchakato wa kuwatangaza wenyeheri na watakatifu unaendelea, lakini sherehe zimeahirishwa hadi mwaka 2021. Mchakato wa kuwatangaza wenyeheri na watakatifu unaendelea, lakini sherehe zimeahirishwa hadi mwaka 2021.  (Vatican Media)

Sherehe za Kuwatangaza Watakatifu na Wenyeheri hadi 2021

Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati na kwa kuzingatia maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, baada ya kushauriana na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, ameamua kuahirisha sherehe zote zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu hadi mwaka 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amekutana na kuzungumza na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Baba Mtakatifu ameridhia mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kuendelea kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Kanisa, lakini maadhimisho ya kuwatangaza kuwa wenyeheri na watakatifu kwa sasa yamehairishwa hadi mwaka 2021. Kanisa limetambua fadhila za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Francesco Caruso, Padre wa Jimbo kutoka Catanzaro- Squillace, aliyezaliwa tarehe 7 Desemba 1879 huko Gasperina, Italia na kufariki dunia hapo tarehe 18 Oktoba 1951. Kanisa limetambua fadhila za kishujaa zilizoneshwa na Mtumishi wa Mungu Carmelo de Palma, Padri wa Jimbo Kuu la Bari-Bitonto, Italia, aliyezaliwa tarehe 27 Januari 1876 na kufariki dunia tarehe 24 Agosti 1961. Kanisa limetambua pia fadhila za kishujaa zilizoshuhudiwa na Mtumishi wa Mungu Francis Barrecheguren Montagut wa Garcìa, Padre mtawa wa Shirika la Mkombozi, aliyezaliwa huko Lèrida, Hispania tarehe 21 Agosti 1881 na kufariki dunia huko Hispania tarehe 7 Oktoba 1957.

Mama Kanisa katika huruma na wema wake, ametambua na kuridhia fadhila za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Maria de la Concepciòn Barrecheguren wa Garcìa, Mwanamke mlei, aliyezaliwa huko Granada nchini Hispania tarehe 27 Novemba 1905 na kufariki dunia hapo tarehe 13 Mei 1927. Mwishoni, Kanisa limetambua pia fadhila za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Matteo Farina, aliyezaliwa huko Avellino, Italia tarehe 19 Septemba 1990. Alikuwa ni mwanafunzi aliyebahatika kuwa na kipaji cha akili, akaonesha upendo mkubwa kwa masomo ya sayansi pamoja na muziki. Alikuwa na ibada ya pekee kwa: Padre Pio wa Pietrelcina na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Katika ujana wake alipambana sana na ugonjwa wa Saratani ya ubongo kwa imani na matumaini makubwa. Tarehe 24 Aprili 2009 akaitupa mkono dunia!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati na kwa kuzingatia maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, baada ya kushauriana na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, ameamua kuahirisha sherehe zote zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu hadi mwaka 2021. Watumishi wa Mungu ambao walipaswa kutangazwa mwaka 2020 ni pamoja na: Mtumishi wa Mungu Lucia Dell’Imamacolata, aliyejulikana kama Maria Ripamont. Mtumishi wa Mungu Marie Louise wa Sakramenti Takatifu; Mtumishi wa Mungu Cayetano Gimènez Martìn na wenzake 15; hawa walikuwa wamepangwa kutangazwa kuwa Wenyeheri mwezi Mei 2020. Wengine ni Kardinali Stefan Wyszyński aliyekuwa atangazwe kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 7 Juni 2020 pamoja na Sandra Sabattini aliyekuwa anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 14 Juni 2020. Hadi wakati huu, hakuna tarehe rasmi ambayo imewekwa kwa ajili ya maadhimisho haya.

Wenyeheri na Watakatifu

 

 

12 May 2020, 12:44