Tafuta

Papa Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Pentekoste amegusia kuhusu: Athari za COVID-19 Ukanda wa Amazonia, Siku ya Faraja Italia na Umoja dhidi ya COVID-19. Papa Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Pentekoste amegusia kuhusu: Athari za COVID-19 Ukanda wa Amazonia, Siku ya Faraja Italia na Umoja dhidi ya COVID-19. 

Papa Francisko: Pentekoste: Amani! Msamaha na Umoja!

Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu matatu: Sherehe ya Pentekoste; Dhana ya Upatanisho na Utume wa Kanisa na Zawadi ya Roho Mtakatifu. Mwinjili Yohane katika sura 20: 19-23 anawakumbusha waamini, siku ile ya kwanza ya juma, pale wanafunzi wake walivyokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, Yesu alipowaambia: “Amani iwe kwenu”. Upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 31 Mei 2020, ameungana na waamini na watu wenye mapenzi mema, waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa Sala ya Malkia wa Mbinguni. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu matatu: Sherehe ya Pentekoste; Dhana ya Upatanisho na Utume wa Kanisa na Zawadi ya Roho Mtakatifu. Mwinjili Yohane katika sura 20: 19-23 anawakumbusha waamini, siku ile ya kwanza ya juma, pale wanafunzi wake walivyokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, Yesu alipokuja na kusimama kati yao na kuwaambia “Amani iwe kwenu”. Baba Mtakatifu anasema, haya ni maneno yanayobeba uzito wa pekee sana kwa sababu ni chemchemi ya msamaha uliotolewa na Kristo Yesu kwa wanafunzi wake, waliokuwa wamemsaliti na kumkimbia wakati wa mateso na kifo chake Msalabani.

Ni maneno yanayokita ujumbe wake katika upatanisho na msamaha kwa wanafunzi ambao walikuwa wamegubikwa kwa hofu na woga! Ni watu ambao walikuwa bado hawawezi kuyaamini macho yao kwamba Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na sasa amefufuka kwa wafu. Ni wanafunzi hawa, ambao asubuhi na mapema walikwenda na kushuhudia kaburi wazi, lakini bado walikuwa hawajaamini, licha ya ushuhuda uliotolewa na Maria Madgalene pamoja na wanawake wengine kwamba, walikuwa wamemwona Yesu Mfufuka! Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anawasamehe na kuwapatia rafiki zake zawadi ya amani. Baada ya wanafunzi kusamehewa, wakaungana na kumzunguka Kristo Yesu, na hivyo kujenga Kanisa: Jumuiya ya watu waliopatanishwa, tayari kujitosa kwa ajili ya utume. Tukio la wanafunzi kukutana na Kristo Mfufuka, linaleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa wafuasi wa Kristo, kiasi hata cha kuwatia shime, ili waweze kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa furaha ya Injili.

Yesu anawaambia kwamba, kama Baba yake wa mbinguni alivyomtuma, naye pia anawapeleka.Haya ni maneno yanayowakumbusha Mitume kwamba, wameteuliwa na kutumwa kuendeleza kazi ya ukombozi ambayo Mwenyezi Mungu alimkabidhi Mwanae wa pekee, Kristo Yesu. Huu si muda tena wa kujifungia ndani; wala si muda wa kulalama na kukumbukia ule muda ambao Kristo Yesu alikuwa pamoja nao. Furaha ya Fumbo la Ufufuko ni kubwa zaidi kwani hii ni furaha mtawanyiko, ambayo kamwe hawawezi kuibakiza ndani mwao, kwani wanapaswa kuwashirikisha wengine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mama Kanisa alipata nafasi ya kuyatafakari matukio yote haya katika maadhimisho ya Jumapili za Kipindi cha Pasaka. Jinsi ambavyo Kristo Mfufuka alivyokutana na kuambatana na Wafuasi wawili wa Emau; Kristo Yesu, Mchungaji mwema anapokutana tena na wanafunzi wake, anawapatia wosia na ahadi ya Roho Mtakatifu ili kuimarisha imani ya wafuasi wake.

Hii ndiyo imani ya Kanisa mintarafu maisha na utume wa Kanisa. Ili kuhamasisha utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia, Kristo Yesu, akawavuvia na kuwapatia Roho Mtakatifu. Huu ni moto unaounguza dhambi na kuwajenga watu wapya. Huu ni moto wa upendo ambao Mitume, watapaswa kuupeleka ulimwenguni. Ni moto wa huruma na mapendo unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini wamepokea zawadi ya Roho Mtakatifu walipobatizwa na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara. Na kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, Roho Mtakatifu akawajalia Mapaji yake saba nayo ni: Hekima yaani uwezo wa kupambanua kwa njia ya akili mema na mabaya, ukweli na uongo na kutoa hukumu kadiri ya sheria ya Mungu. Nguvu: ni kushinda magumu na kuvumilia mateso kwa nguvu na uwezo toka kwa Mungu. Shauri ni kushika njia njema. Akili ni kutetea na kutoa kweli kwa muono wa kina na kupenya kwenye ukweli wa Mungu. Elimu ni kuamua kwa usahihi juu ya kweli za imani kadiri ya chimbuko halisi na kanuni za kweli zinazofumuliwa. Ibada ni kumwona Mungu kuwa Baba wa wote.

Uchaji wa Mungu unamwezesha mwamini kumwabudu Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wote! Uchaji wa Mungu anasema Baba Mtakatifu ni kinyume kabisa cha woga na hofu iliyowaganda wafuasi wa Kristo Yesu. Uchaji wa Mungu ni upendo unaobubujika kutoka kwa mwamini, kama uhakika wa huruma na wema wake unaofumbatwa katika imani, ili kusonga mbele kwa kuzingatia dira na mwongozo wa maisha mintarafu mapenzi ya Mungu. Uchaji wa Mungu ni uhakika wa nguvu na uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Sherehe ya Pentekoste inapyaisha uelewa wa uwepo wa Roho Mtakatifu. Anawakirimia waamini ujasiri wa kutoka ndani ya kuta zinazowalinda na kuwafungia kwenye mazoea mgando! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, mdau kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, iliyoonja mang’amuzi ya Sherehe ya Pentekoste. Kanisa linamwomba, Bikira Maria ili aweze kuliombea kwa Mwanae wa pekee, liweze kupata ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!

Papa: Malkia wa Mbingu
31 May 2020, 14:13