Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni Mwaliko kwa Waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu wa Kristo Mfufuka! Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni Mwaliko kwa Waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu wa Kristo Mfufuka! 

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ushuhuda na Ukarimu!

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wakarimu wa Kristo Mfufuka anayewatuma kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi wake, kwa kuwabatiza na kuwafundisha kuyashika yote aliyowaamuru. Na tazama yeye yuko pamoja nao siku zote hata ukamilifu wa dahari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Mei 2020 mara baada ya Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, Mintarafu Kazi ya Uumbaji, amewashukuru waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, waliokuwa wanafuatilia katekesi hii kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Amesema, sala ni majadiliano ya kina kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya sala, mwanadamu anaweza: kumsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokuwa na kifani. Sala ni mahali muafaka pa mwanadamu kumtolea Mungu shida, wasi wasi na mashaka yake. Baba Mtakatifu amefanya rejea kwenye Kitabu cha Yoshua Bin Sira Sura 2:10 inayosema: “Angalieni vizazi vya kale mkaone: nani aliyemtumaini Bwana akaaibika? Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita kadharauliwa? Kwa kutafakari maajabu ya Kazi ya Uumbaji, mwanadamu anaweza kutambua ukuu, utukufu na upendo wa Mungu Muumbaji, anayeangalia yale yote aliyoyaumba. Furaha na sifa juu ya Kazi ya Uumbaji inamsaidia mwanadamu kupata utimilifu, amani na utulivu wa ndani.

Tarehe 21 Mei 2020 ni Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Lakini kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii inaadhimishwa Jumapili tarehe 24 Mei 2020, yaani Jumapili ya Saba ya Kipindi cha Pasaka, ili kuwawezesha waamini wengi kushiriki kikamilifu katika tukio hili muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa. Katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wakarimu wa Kristo Mfufuka anayewatuma kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi wake, kwa kuwabatiza na kuwafundisha kuyashika yote aliyowaamuru. Na tazama yeye yuko pamoja nao siku zote hata ukamilifu wa dahari. Na anaendelea kuwatia shime katika hija ya maisha yao hapa duniani. Rej. Mt. 28:19-20.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua uzuri wa Kazi ya Uumbaji inayoakisi utukufu na mng’ao wa Mwenyezi Mungu. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni, Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwaombea amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka! Amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Huyu ni kiongozi na mchungaji aliyekuwa na imani thabiti, alipenda kuliaminisha Kanisa na watu wote, mbele ya Mwenyezi Mungu. Akajikabidhi ya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa kusema: “Totus Tuus” kama nembo yake ya Kiaskofu.

Amewaambia waamini kwamba, hata katika shida na magumu kiasi gani, bado wanaweza kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, anayeweza kuwaombea mbele ya Mwenyezi Mungu. Maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II yalikita mizizi yake katika sala na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, mfano bora wa kuigwa na waamini wote! Mwanga wa Kristo Mfufuka uendelee kung’ara katika nyoyo za waamini. Mwezi Mei ambao umetengwa rasmi kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, iwe ni fursa ya kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa kazi nzima ya ukombozi, kila siku. Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria jinsi ya kuyatafakari matukio mbali mbali yanayoibuka katika hija ya maisha ya mwanadamu.

Papa: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni

 

20 May 2020, 13:36