Baba Mtakatifu Francisko asema, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko asema, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. 

Papa Francisko: Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mt. Yohane Paulo II!

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Yohane Paulo II alipozaliwa. Kanisa linatambua na kuthamini amana na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Tarehe 18 Mei 2020, Majira ya saa 1:00 za Asubuhi kwa saa za Ulaya, anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Altare ya Kaburi la Mt. Yohane Paulo II lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 17 Mei 2020 amesema, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Yohane Paulo II alipozaliwa. Kanisa linatambua na kuthamini amana na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, Jumatatu tarehe 18 Mei 2020, Majira ya saa 1:00 za Asubuhi kwa saa za Ulaya, anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Altare ya Kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ya Misa Takatifu itarushwa mubashara na vyombo mbali mbali vya mawasiliano, ili kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipozaliwa! Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Mtakatifu Yohane Paulo II huko mbinguni aliko aendelee kuwaombea watu wa Mungu pamoja na kuombea amani ulimwenguni.

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Katekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków.

Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane  Paulo II alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mei Mosi, 2011 akamtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia kuhusu Ibada ya Misa Takatifu inayoanza kuadhimishwa kwa ushiriki mkamilifu wa waamini katika nchi mbali mbali Barani Ulaya, ambazo zilisitisha huduma huu muhimu katika maisha ya waamini kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu amewasihi viongozi wa Kanisa na waamini kwa ujumla kuhakikisha kwamba, wanzingatia, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili kulinda na kudumisha usalama, afya na maisha ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Kuna baadhi ya nchi ambazo zinaendelea kufanya tathmini ili kuona uwezekano wa kurejesha tena huduma ya Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini katika nchi zao. Nchini Italia, kuanzia tarehe 18 Mei 2020 wanaweza kuanza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anapenda kuungana na waamini kumshukuru Mungu kwa kurejesha tena maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kati ya watu wa Mungu. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni alama ya matumaini na zawadi kwa watu wa Mungu. Kumekuwepo na Mapokeo pamoja na utamaduni kwenye majimbo mbali mbali, waamini kupokea Ekaristi Takatifu na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wakati wa Mwezi Mei wa kila mwaka. Lakini kutokana na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, maadhimisho haya yamesogezwa mbele ili kulinda usalama na maisha ya waamini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka watoto wote ambao walikuwa wamejiandaa kupokea Komunio ya Kwanza wakati huu. Anawaalika watumie muda huu wakati wa kungoja kupokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha yao, kwa kusali, kusoma na kutafakari vitabu vya Katekesi na kuendelea kuzama zaidi ili kuweza kumfahamu Kristo Yesu. Iwe ni fursa ya kukua na kukomaa katika utu wema na kuanza kujifunza kujisadaka katika huduma kwa ajili ya jirani zao.

Papa: Miaka 100 JPII

 

17 May 2020, 14:03