Baba Mtakatifu Francisko: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa: Upadre na Maisha ya Wakfu yanahitaji ujasiri, udumifu na sala! Baba Mtakatifu Francisko: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa: Upadre na Maisha ya Wakfu yanahitaji ujasiri, udumifu na sala! 

Jumapili ya Mchungaji Mwema! Siku ya 57 ya Kuombea Miito!

Wito wa Upadre na Maisha ya Wakfu yanahitaji ujasiri, udumifu na sala. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mungu ili aweze kulipatia Kanisa lake watenda kazi: wema, hodari na watakatifu, watakaoweza kujisadaka kwa ajili ye ujenzi wa Ufalme wa Mungu, huku wakiwa na moyo na mikono wazi, tayari kunafsisha upendo wa Mungu katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani, ambayo imeadhimishwa tarehe 3 Mei 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya umeongozwa na kauli mbiu: “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope: Maneno ya Miito: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. Baba Mtakatifu mara baada ya tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu amewakumbusha waamini kamba, uwepo wote wa maisha ya Kikristo ni jibu muafaka wa wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaomwilishwa katika mifumo mbali mbali ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Siku ya kuombea Miito Duniani inawakumbusha waamini kwamba katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kuna kazi nyingi zinazopaswa kutekelezwa na kwamba, kuna haja ya kusali zaidi, ili Mwenyezi Mungu aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake. Rej. 9: 37-38. Wito wa Upadre na Maisha ya Kuwekwa Wakfu yanahitaji ujasiri na udumifu na bila sala hakuna kinachowezekana. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kulipatia Kanisa lake watenda kazi: wema, hodari na wachakapakazi, watakaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ye ujenzi wa Ufalme wa Mungu, huku wakiwa na moyo na mikono wazi, tayari kunafsisha upendo wa Mungu katika maisha na utume wao!

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo wake wa karibu kwa waathirika na wagonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Amewakumbuka na kuwaombea wale wote wanaowahudumia wagonjwa wa Corona. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu anaunga mkono na anapenda kuitia shime Jumuiya ya Kimataifa kushikamana na kushirikiana katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, ili kuweza kujibu kwa ukamilifu na ufanisi mkubwa Janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Ni muhimu kwa wanasayansi na watafiti kuunganisha nguvu zao za kisayansi katika ukweli na uwazi ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kupata chanjo na tiba dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni muhimu ikiwa kama, dawa, vifaa tiba na teknolojia muhimu katika mapambano haya itaweza kuwafikia watu walioambukizwa na ugonjwa wa Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia, ili hata wao waweze kufaidika na maendeleo ya huduma bora za afya!

Papa Siku ya Kuombea Miito 2020
03 May 2020, 14:04